Mradi uvunaji maji ya mvua wakamilika, utahifadhi lita milioni 166.3

Muktasari:

  • Bwawa la kuvuna maji ya mvua kisha kusambazwa katika vijiji vinne vilivyoko Kata ya Ndalambo, wilayani Momba, Mkoa wa Songwe, limezinduliwa na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, huku ikitarajiwa litahudumia wakazi zaidi ya 11671 wa vijiji hivyo.

Songwe. Bwawa la kuvuna maji ya mvua kisha kusambazwa katika vijiji vinne vilivyoko Kata ya Ndalambo, wilayani Momba, Mkoa wa Songwe, limezinduliwa na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, huku ikitarajiwa litahudumia wakazi zaidi ya 11671 wa vijiji hivyo.

 Akisoma taarifa ya mradi huo Mhandisi wa maji kutoka Bonde la Ziwa Rukwa Jackson Waredi amesema bwawa hilo linauwezo wa kuhifadhi zaidi ya lita milioni 166.3 za maji, na kwamba lina uwezo wa kudumu katika kipindi cha zaidi ya miaka 50 iwapo litatunzwa.

Amesema katika bwawa hilo, pia imewekwa miundombinu ya kunyweshea mifugo bila kuingiliana na binadamu, wala kuharibu mazingira ya bwawa lenyewe.

Akizungumza kabla ya kufanya uzinduzi Wazir Aweso amesema: “Niwaombe wataalamu mnapokwenda kwenye maeneo ya watu kuanzisha miradi ya maji, shirikianeni na wazee wa maeneo husika ili wawape baraka zao," amesema Aweso.

Aidha Aweso amesema kutokana na hali ngumu ya upatikanaji wa maji kwenye kata hizo, wizara imeongeza Sh500 milioni kwaajili ya kuongeza mtandao wa mabomba na hivyo kuongeza idadi ya vijiji vitakavyonufaika.

Mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Ndalambo, Juliana Siwakwi, amesema bwawa hilo litaleta ukombozi mkubwa kwa jamii hiyo na hasa wanawake ambao wamekuwa wakiteseka kutembea mwendo mrefu kutafuta maji.

"Tunashukuru Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kutuchimbia bwawa hili na kutuwekea mabomba kwenye makazi yetu," amesema Siwakwi.

Naye Mbunge wa Jimbo la Momba, Condester Sichalwe, amesema licha ya kuzinduliwa kwa mradi huo, bado Wilaya ya Momba inakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa maji safi na salama na kuiomba Serikali kuendelea kuisaidia ili kumaliza tatizo hilo.

" Mheshimiwa Waziri, kaka yangu Aweso, sisi wakazi wa Momba tuna uhaba mkubwa wa maji, kwa kipindi kirefu tumekuwa tukichangia maji pamoja na mifugo, tumechoshwa na hilo, lakini pia tumechoshwa kushuhudia wenzetu wakipoteza maisha wakati wakisaka maji kwenye mito kwa kuliwa na Mamba," amesema Condesta.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Momba, Fakii Lulandala, amesema mpaka sasa halmashauri ya wilaya ya Momba inajumla ya miradi 20 ya maji, kati hiyo, miradi mipya ni 14, na kwamba iliyosalia ni ya zamani.