Mrundi alivyomuua mwenzake, kumzika na kupanda mazao juu ya kaburi lake

Muktasari:

  • Jaji Nkwabi amhukumu kunyongwa hadi kufa na kwa mshtakiwa wa pili asema upande wa mashtaka umethibitisha shtaka dogo la kusaidia baada ya tukio, hivyo anamhukumu kutumikia kifungo cha miaka minne jela.

Kigoma. Licha ya Bandyeekela Janwary, raia wa Burundi kushikilia msimamo kuwa ndugu yake Kwizera Kamazi alikufa kifo cha kawaida kutokana na ugonjwa, Mahakama imethibitisha kuwa hakufa kifo cha kawaida, bali aliuawa kwa kupigwa kwa jembe kichwani.

Baada ya kumuua kwa jembe, raia huyo wa Burundi akishirikiana na mshtakiwa namba mbili, Ndayikengurukiye Stanslaus naye raia wa Burundi na watu wengine wanne kumzika, kisha Bandyeekela akapanda mazao juu ya kaburi.

Ni kutokana na waliyoyafanya, Jaji John Nkwabi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma kupitia hukumu yake aliyoitoa Aprili 29, 2024, amemhukumu Bandyeekela kunyongwa hadi kufa huku Ndayikengurukiye akimfunga kiufungo cha miaka minne jela.

Kwa mujibu wa ushahidi, akiwa na dhamira ya kuishi maisha mazuri, Kwizera ambaye alikuwa raia wa Burundi, alisafiri kutoka nchuni mwake hadi Tanzania na baada ya kufika nchini aliajiriwa na Bandyeekela kama kibarua huko Nyarugusu Wilaya ya Kasulu.

Baada ya kukamilisha mkataba wake wa kibarua na mshtakiwa huyo wa kwanza, alidai alipwe ujira wake lakini dai lake hilo halikupokelewa vizuri na mshtakiwa huyo, ambaye alimpiga kwa jembe kichwani na kwa kushirikiana na Ndayikengurukiye, waliuzika mwili wake.

Tukio hilo lilitokea tarehe isiyojulikana Septemba 2022 eneo la Rusekwa, Kijiji cha Nyarugusu Wilaya ya Kasulu Mkoa wa Kigoma ambapo washtakiwa walikamatwa huku mshtakiwa wa kwanza akifunguliwa mashtaka ya mauaji na wa pili kwa kusaidia kuzika mwili.


Utetezi wao ulivyokuwa

Raia hao wa Burundi walikanusha masitaka hayo ambapo mshtakiwa wa kwanza, Bandyeekela katika utetezi wake alikiri kusafiri kutoka Burundi hadi Tanzania akiwa na marehemu ambaye ni ndugu yake, kwa lengo la kutafuta mashamba Nyarugusu.

Alijitetea, kuwa  baadaye alirudi Burundi na akiwa huko alipata taarifa kuwa Kwizera alikuwa ni mgonjwa na ikamlazimu kurejea Tanzania na akamkuta akiwa katika hali mbaya na kuwa alinunua dawa mbalimbali na kumpatia ili kuokoa maisha yake.

Alidai hakumpeleka hospitali kwa kukosa nyaraka za kumuidhinisha kuishi nchini na kwamba ndugu yake huyo alikufa wakati wakijaribu kumrudisha nyumbani Burundi kwa ajili ya matibabu, ndipo alishauriwa kumzika bila kuujulisha uongozi wa kijiji.

Akaeleza kuwa alikamatwa Desemba 13, 2022, akapigwa na polisi ndipo aliwapeleka mahali walipomzika Kwizera na kuwa mwili wake ulifukuliwa na kufanyiwa uchunguzi na daktari aliyesema kiini cha kifo ni kupigwa na kitu kichwani.

Wakati akidodoswa maswali na mawakili wa Jamhuri, mshtakiwa alikiri mshtakiwa wa pili alimsaidia kwa kushirikiana na watu wengine kumzika marehemu, lakini akakanusha kuotesha mazao juu ya kaburi, akisema ni wafanyakazi wa mmiliki wa shamba.

Mshtakiwa wa pili kwa upande wake, alieleza kuwa naye ni raia wa Burundi na kueleza kuwa alikuja Tanzania kutafuta maisha kama kibarua katika mashamba huko Nyarugusu lakini akakanusha maelezo kuwa alikuwa kibarua wa mshtakiwa wa kwanza.

Badala yake, alijitetea kuwa alikuwa anajishughulisha kubeba mizigo ya watu kwa kutumia baiskeli na kwamba siku moja alipokwenda kumtembelea mshtakiwa wa kwanza, alimkuta Kwizera akiwa mgonjwa na baadaye alifariki kwa maradhi.

Alieleza kuwa aliombwa kusaidia kuzika mwili wa marehemu, ombi ambalo alilikubali na wakati akidodoswa na mawakili wa Jamhuri, alieleza idadi ya walioshiriki kuzika mwili walikuwa watu sita na kwamba yeye alifika wakati wanamalizia kufukia.


Hukumu ya Jaji Nkwabi

Katika hukumu yake, Jaji Nkwabi alisema wakati mshtakiwa wa kwanza akishikilia msimamo kuwa Kwizera alikufa kutokana na maradhi, mashahidi wa Jamhuri walieleza kuwa kifo chake hakikutokana na maradhi bali kupigwa kwa jembe kichwani.

Jaji alisema daktari aliyeuchunguza mwili wa marehemu alieleza kuwa mwili wa marehemu ulikuwa na jeraha kwenye fuvu ambalo lilisababishwa na kupigwa na kitu butu kichwani, ushahidi ambao uliunganika na ule wa mashahidi wengine wa Jamhuri.

“Kutokana na ushahidi huo wa Jamhuri, hakuna mashaka kuwa marehemu hakufa kifo cha kawaida. Ninaona marehemu alikutana na kifo katika njia isiyo ya asili ambayo ni kupata jeraha lililotokana na kupigwa kwa jembe na kupasua fuvu,”alisema Jaji.

“Katika mazingira haya, naona hoja ya kama marehemu alikufa kifo kisichokuwa cha kawaida, jibu ni ndio na hoja ya pili kama mshtakiwa wa kwanza ndio alisababisha kifo na alikuwa na nia ovu jibu liko wazi kuwa yai ni yai”alisema Jaji na kuongeza:-

“Mshtakiwa wa kwanza hakufurahishwa pale marehemu alipodai amlipe ujira wake kwa kazi ambayo alikuwa amekwishaifanya, hapo ni wazi kulikuwa ni nia ovu ya kufanya mauaji. Kwa hiyo mshtakiwa alikuwa na nia ovu ya kufanya tendo la kuua.”

Kuhusu mshtakiwa wa pili, Jaji Nkwabi alisema huyo anakiri kushiriki kuuzika mwili wa marehemu lakini katika hatua za mwisho mwisho za ufukiaji, lakini akajikanganya baadae na kusahahau kuwa uongo ni kama mdudu mende.

Kwamba kila unapomgundua mmoja, wapo wengine wengi waliojificha na Jaji akafafanua kuwa uongo mmoja unafanya utilie mashaka ukweli wote uliosemwa na mtu, kama ilivyotokea kwa washtakiwa hao wawili.

Jaji alifafanua kuwa utetezi wake unaongezewa utata na utetezi wa mshirika wake ambaye ni mshtakiwa wa kwanza, ambaye alisema mshtakiwa huyo wa pili alishiriki katika kumzika marehemu baada ya umauti kumkuta huko kijiji cha Nyarugusu.

Kulingana na Jaji, baada ya upande wa mashtaka kuishawishi mahakama kuwa washtakiwa wana kesi ya kujibu, ulikuwa ni wajibu wa washtakiwa kuleta maelezo ya nani hasa alisababisha jeraha baya kichwani kwa marehemu na kusababisha kifo.

Badala yake, Jaji alisema katika hukumu hiyo kuwa badala ya washtakiwa kuleta maelezo hayo, washtakiwa walitoa utetezi wa uongo kuhusiana na jambo hilo na uongo wa utetezi uliunga mkono ushahdi wa upande wa mashtaka.

Kutokana na uchambuzi huo, Jaji alisema upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha shitaka la mauaji ya kukusudia dhidi ya mshtakiwa wa kwanza, Badyeekela Janwary hivyo anatiwa hatiani na kuhukumiwa adhabu pekee ya kosa hilo ambayo ni kifo.

Kwa upande wa mshtakiwa wa pili, Jaji Nkwabi alisema ameridhika kuwa upande wa mashtaka umethibitisha shtaka dogo la kusaidia baada ya tukio, hivyo anamhukumu kutumikia kifungo cha miaka minne jela.