Mtanzania ang’ara tuzo za utafiti Marekani

Muktasari:

  • Mtafiti kutoka Taasisi ya Afya Ifakara Health (IHI) ameshinda tuzo ya Mtafiti Mdogo ya Marekani ya ASTMH (American Society of Tropical Medicine and Hygiene) 2023 huko Chicago nchini Marekani na kuandika historia ya kuwa Mtanzania wa pili kushinda tuzo hiyo baada ya miaka 15 kupita.

Dar es Salaam. Mtafiti kutoka Taasisi ya Afya Ifakara Health (IHI), Issa Mshani (29) ameshinda tuzo ya Mtafiti Mdogo ya Marekani ya ASTMH (American Society of Tropical Medicine and Hygiene) mwaka 2023 huko Chicago nchini Marekani.

Issa anakuwa Mtanzania wa pili kushinda tuzo hiyo, tangu ilipotolewa kwa Profesa Fredros Okumu miaka 15 iliyopita ambaye ni ni Mtafiti Kiongozi IHI, pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Glasgow, Scotland, Uingereza.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumanne, Oktoba 24, 2023 na taasisi hiyo, imeeleza kuwa tuzo hiyo imetolewa kwa Issa ambaye kwa sasa yupo masomoni akiendelea na Shahada ya Uzamivu London nchini Uingereza.

Mtafiti huyo Issa amesema tuzo hiyo ni ushuhuda wa kujitolea kwa wanasayansi wa Ifakara kwa kufanya tafiti za ndani na nje bila kujali mipaka,

“Hizi ni habari njema kwa watafiti wachanga wote nchini Tanzania na ni ya kihistoria na ni wakati sasa wa kusherehekea.”

Amesema tuzo ni ishara ya ubora katika uwanja wa tafiti za kitropiki, inahitaji kujitolea, uvumilivu, na utafiti wa msingi.

Kila mwaka, ASTMH huchanganua michango ya watafiti wa kipekee wa taaluma ya tafiti na kutoa tuzo ya mtafiti mchanga. Tuzo hii hutolewa kama sehemu ya shindano la kila mwaka linalofanywa siku ya uzinduzi wa mkutano huo.

Kusudi la tuzo hii ni kuhamasisha na kusaidia wanasayansi wachanga katika harakati zao za kazi katika nyanja tofauti ndani ya utafiti wa magonjwa ya kitropiki