Mtanzania ashinda tuzo ya Bima Uingereza

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima Zanzibar (ZIC), Arafat Haji

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima Zanzibar (ZIC), Arafat Haji ameibuka kidedea katika tuzo za jarida la Global Brands zilizofanyika Uingereza  katika kipengele cha Mtendaji Bora wa Sekta ya Bima kwa mwaka 2023.

Mbali na Arafat pia Shirika la Bima Zanzibar (ZIC), limeibuka mshindi katika kipengele cha shirika la bima la kuaminika zaidi (Most Reliable Insurance Corporation) katika tuzo hizo.

Katika orodha iliyotolewa ya washindi mbalimbali wa tuzo hizo iliyotolewa jana

Novemba 14, 2023, chapa ya ZIC imeonekana kuwa iliyoaminika zaidi kwa mwaka 2023 upande wa sekta ya bima.

Akizungumzia ushindi wake na ZIC katika tuzo hizo, Arafat amesema kuwa umetokana na juhudi za pamoja za kuhakikisha shirika hilo linapiga hatua.

"Nimefurahia kupigiwa kura kuwa Mkurugenzi Mtendaji Bora wa Mwaka wa Shirika la Bima na ZIC kama Kampuni ya Bima inayotegemewa zaidi Tanzania katika tuzo zinazotolewa na Global Brands Magazine.

"Haya ni matokeo ya Uchapakazi na kujitolea kwa timu nzima ya ZIC na Bodi yetu," amesema Arafat.

Global Brands ni jarida ambalo limekuwa likijihusisha na utoaji habari na tuzo mbalimbali zinazohusu chapa za sekta tofauti duniani.