Mtazamo wa Jaji Warioba miaka 60 ijayo ya Muungano

Muktasari:

  • Warioba amesisitiza mijadala kuhusu Muungano isijikite kwenye siasa, bali ilenge katika kuona namna bora ya kuwahudumia wananchi, ili wote wajione Watanzania badala ya kujitofautisha.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Warioba amesema msingi wa kuimarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar katika miaka 60 ijayo ni kuhakikisha sera na mipango inayowekwa kwa pande zote mbili inajali masilahi ya wananchi kwa usawa, badala ya madaraka.

Amesema msisitizo wa mijadala kuhusu Muungano isijikite kwenye siasa, bali ilenge katika kuona namna bora ya kuwahudumia wananchi, ili wote wajione Watanzania badala ya kujitofautisha.

Warioba ametoa kauli hiyo katika kipindi ambacho Tanzania inakaribia kuadhimisha miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, wakati akifafanua nini kifanyike katika kipindi kama hicho kijacho.

Tanganyika na Zanzibar ziliungana Aprili 26, 1964, chini ya Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume mtawalia.

Jaji Warioba alieleza hayo nyumbani kwake jijini Dar es Salaam jana, alipozungumza na waandishi wa habari katika mahojiano maalumu kuhusu miaka 60 ya Muungano.


Muungano uwaguse wananchi

Kwa mtazamo wa Jaji Warioba, kipindi kijacho Serikali inapaswa kujikita katika kuimarisha haki za Watanzania ndani ya Muungano.

Katika utekelezaji wa hilo, kiongozi huyo, aliyewahi kuwa makamu wa kwanza wa Rais, alisema ni vema kuangalia mambo ya maendeleo yenye utofauti ili hatua zichukuliwe kuweka usawa.

Ametolea  mfano upatikanaji wa huduma za afya, ingawa si jambo la Muungano, lakini mwananchi kutoka upande wowote anapaswa kuwa na uhuru wa kupata huduma hiyo popote bila kikwazo.

“Inatakiwa mwananchi wa bara akiwa na bima ya afya itumike hata atakapokwenda hospitali ya Zanzibar na bima ya Zanzibar itumike hata bara,” amesema.

Msingi wa Muungano kwa mujibu wa Jaji Warioba ni kuwaunganisha watu wa pande zote ili kila mmoja ajione yupo nyumbani anapokuwa popote na awe huru kufanya shughuli yoyote.

“Kama ni kilimo anaweza akaenda popote kufanya shughuli yoyote na hiyo ndiyo faida ya Muungano, wananchi wapate umoja,” amesisitiza.

Ukiachana na sekta ya afya, mkongwe huyo wa siasa ametaja uchumi wa buluu na utalii kuwa unapaswa kuwekewa sera moja na utekelezwaji wa mipango yake uwe shirikishi kwa Serikali zote.

“Kama kuna mtu ametoka nje anataka kwenda mbugani aanzie huko kisha ataenda kwenye fukwe Zanzibar, ndiyo vizuri, kwanza tutahamasisha utalii na kutengeneza ajira zaidi," amesema.

Amesisitiza mambo yote yanayowahusu wananchi lazima yaunganishwe kuwa kitu kimoja, ili kuimarisha Muungano.

Alisema hata rasimu ya mabadiliko ya Katiba inayoeleza kuhusu uwepo wa Serikali tatu, imebainisha uwepo wa tume itakayounganisha nchi na kushauri kuhusu mambo ya kisera.

“Usipokuwa na sera moja, mambo yatakuwa tofauti, mambo yote yanayohusu shughuli za wananchi lazima yaunganiashwe kuwa moja,” amesema.


Kero za Muungano

Kuhusu kero za Muungano, Jaji Warioba alionyesha mtazamo tofauti, akisema nyingi zinazozungumzwa ni masuala ya kisiasa na madaraka, haziwahusu wananchi wa kawaida.

Amekwenda mbali zaidi na kueleza hata Serikali inapotangaza kufuta baadhi ya kero, mara nyingi wananchi hawafahamu ni zipi na hawapaswi kuhusishwa nazo.

“Ukiuliza wananchi wanazijua hizo kero, ni Serikali pekee ndiyo inayozungumza na haielezi ni zipi. Nataka watu watoke kwenye kuzungumzia madaraka wakati wote, tayari uhusiano wa wananchi umeimarishwa, ni vema kuimarisha zaidi ili wajione kuwa wote ni Watanzania,” amesema.


Lugha za viongozi

Katika mahojiano hayo, Warioba aligusia kile alichokiita kauli za baadhi ya viongozi, akisema nyingi zinaleta mgawanyiko badala ya kutengeneza umoja.

“Kinachopaswa kuangaliwa ni masilahi ya nchi na hata viongozi kwa sasa wamekuwa na lugha za kuzungumzia pande mbili ilhali wanapaswa kuzungumza kuhusu Tanzania kwa ujumla.

"Wanataka kama tusiendelee, mimi nasema tukitatua changamoto za wananchi wa kawaida wao hawataangalia wako upande gani," amesema.

Ametaka yaangaliwe mambo yanayoimarisha Muungano, si yale yanayofanya nchi zitengane kabisa.


Mwelekeo uchaguzi Z’bar

Akijibu swali kuhusu uchaguzi, Jaji Warioba amesema umefika wakati wa Zanzibar  kufanya mabadiliko ya kisiasa kwa masulahi ya Muungano.

“Umefika wakati Zanzibar sasa ingeanza kufanya mabadiliko ya kisiasa, kwa sababu ya mazingira ya Mapinduzi, ililazimika kuweka mambo fulani fulani, ilikuwa ni muhimu kwa wakati huo,” amesema.

Miongoni mwa mambo aliyosema yanapaswa kubadilishwa ni sheria inayomtambua Mzanzibari aliyeishi kwenye eneo husika kwa miaka mitatu, kuwa ndiye anayepaswa kupiga kura katika eneo hilo.

Amesema hilo linawabagua Wazanzibari wanaoishi nje ya visiwa hivyo, akisisitiza ni vema kufanyia mabadiliko.

“Kwa sasa kuwe na masharti nafuu kwa diaspora, wawe na haki ya kupiga kura na kuna nchi kukiwa na uchaguzi unawaona raia wao wanaoishi Tanzania wanapiga kura, nasi tuwe na hiyo,” amesema.

“Zanzibar waanze kufikiria kuona kama utaratibu huo wanapaswa kuendelea nao au wasiendelee nao, hayo ndiyo mambo yanayohusu wananchi na yanapaswa kutatuliwa,” amesema.

Amesisitiza kila kinachofanyika, mwelekeo wake uwe kwenye kuwaunganisha wananchi ili hata ikifika miaka 100 wote wajione ni Watanzania.


Uzoefu wa mataifa mengine

Baada ya uchaguzi wa mwaka 1980, Warioba alisema Mwalimu Nyerere alimtuma yeye na Pius Msekwa kwenda kujifunza kuhusu muungano katika mataifa yenye uzoefu.

Katika safari hiyo, alisema walikwenda Uingereza ambako pamoja na kukuta kila eneo lina utamaduni wake, wananchi wote walitambulika kwa taifa moja.

Hali kama hiyo, amesema aliikuta Marekani na hata Canada na India walikokwenda kutekeleza maelekezo hayo ya Mwalimu Nyerere.

"Serikali yoyote ile lazima ihudumie wananchi, kwa wananchi tazameni haki zao si kutazama mambo ya Muungano, hata lisipokuwa jambo la Muungano lazima muangalie,” amesema.


Changamoto zilizokuwepo

Amesema baada ya Tanganyika na Zanzibar kuungana, changamoto iliyokuwepo ni katika kukusanya mapato na kuyagawa kwa ajili ya Serikali ya Muungano na kuacha mengine kwa ajili ya Zanzibar.

Changamoto hiyo, amesema ilisababisha kufanywe mabadiliko yaliyoiruhusu Zanzibar kukusanya kodi hizo, kisha yenyewe iwasilishe mchango wa Muungano.

Pamoja na mabadiliko hayo, alisema bado kulikuwa na changamoto kwa sababu Zanzibar haikuwa inawasilisha fedha hizo.

“Matatizo yalibaki hapo kwa kuwa Zanzibar haikuwa inaleta mchango na sina uhakika kama hilo limerekebishwa,” amesema.

Hata hivyo, alieleza Muungano umeunganisha wananchi na ndiyo iliyokuwa sababu ya kuungana.

Amesema ili kuupima muungano, ni vema kuangalia faida kwa wananchi na ikitokea wananchi hawajalalamika ujue hakuna tatizo.

Amesema ushahidi wa uimara wa Muungano ni uwepo wa mwingiliano wa wananchi, akifafanua kuna Wazanzibari wengi wanaoishi bara.

Jaji Warioba amesema kitu pekee kinachozungumzwa na wananchi katika Muungano ni muundo wake, akisisitiza umuhimu wa kuamua kuhusu hilo.

"Watanzania wote wanapenda Muungano, nilipata bahati ya kuzunguka nchi hii wakati wa kutafuta maoni ya wananchi, moja ya mambo yaliyozungumzwa ilikuwa ni muundo wa muungano," amesema.