Mtumishi Hanang atupwa jela miaka 20 kwa wizi wa sh3.5 milioni

Muktasari:

  • Muray aliyekuwa mkusanya mapato kwa kutumia mashine ya POS wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang', amehukumiwa adhabu hiyo na Mahakama ya Wilaya ya Hanang' baada ya kumtia hatiani kwa kosa hilo katika kesi ya uhujumu uchumi iliyokuwa ikimkabili mahakamani hapo.

Hanang'. Mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang' mkoani Manyara, Petro Muray amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela, baada ya kupatikana na hatia ya ubadhirifu wa mali ya umma.

 Pamoja na adhabu hiyo, Muray ametakiwa kurejesha Sh3.5 milioni alizoisababishia hasara halmashauri hiyo.

Muray aliyekuwa mkusanya mapato kwa kutumia mashine ya POS wa halmashauri hiyo, amehukumiwa adhabu hiyo na Mahakama ya Wilaya ya Hanang' baada ya kumtia hatiani kwa kosa hilo katika kesi hiyo.

Hukumu hiyo ilitolewa jana Ijumaa Aprili 19, 2024 na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Anorld Kileo aliyeisikiliza kesi hiyo.

Katika kesi hiyo ya  uhujumu uchumi namba 03/2023, Muray alikuwa akikabiliwa na shtaka moja la ubadhirifu wa mali ya umma kinyume na kifungu cha 28(1) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa,  Sura ya 329 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Muray alitenda kosa hilo kwa nyakati tofauti kuanzia Juni hadi Desemba mwaka 2023.

Ilielezwa kuwa katika kipindi hicho, mshtakiwa alikuwa akikusanya fedha zilizotokana na vyanzo vya misitu wilayani Hanang na alikusanya jumla ya Sh3.5 milioni, lakini hakuziwasilisha fedha hizo kwa halmashauri hiyo.

Mahakama hiyo baada ya kusikiliza ushahidi, imeridhika kuwa upande wa mashtaka umethibitisha shtaka hilo dhidi ya mshtakiwa kwa kiwango kinachotakiwa kwa mujibu wa sheria, yaani bila kuacha mashaka yoyote.

"Kwa kuzingatia ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka, Mahakama hii imeridhika na ushahidi, hivyo inakutia hatiani kwa kosa la ubadhirifu kama alivyoshtakiwa,” amesema Hakimu Kileo na kuongeza;

"Kwa hiyo Mahakama inakuhukumu mshtakiwa Petro Muray adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela na pia urejeshe fedha alizoisababishia hasara mamlaka ya Serikali (Halmashauri ya Wilaya ya Hanang') kiasi cha Sh3.5 milioni.”

Tayari Muray ameshapelekwa gerezani kuanza kutumikia adhabu yake hiyo.

Wakizungumzia adhabu hiyo, baadhi ya wakazi wa mji mdogo wa Katesh wamedai adhabu kama hizo zinakuwa funzo kwa watumishi wengine kufanya ubadhirifu wa fedha za umma.

Aloyce Nade, amesema matukio ya watumishi wa Serikali kufanya ubadhirifu yamekithiri nchini, hivyo adhabu kama hizo zinasababisha hofu na uadilifu.

"Mahakama imefanya kazi yake ipasavyo, kwani watumishi wa halmashauri wamezoea kuwa na tamaa na kufanya ufisadi ila hukumu kama hizi zinawapa onyo wengine," amesema Nade.