Mufti atoa wito kwa Watanzania kuiombea nchi

Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir

Muktasari:

Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir amewahimiza Watanzania na waumini wa dini kuendelea kufanya maombi kwa Mungu ili aipushe nchi na majanga mbalimbali ikiwemo ukame uliopo unaosababisha uhaba wa maji.

Dar es Salaam. Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir amewataka waumini wa dini hiyo na Watanzania kuendelea kufanya maombi na ibada ili Mungu aliepushe Taifa na changamoto ya ukame na joto kali yaliyopo sasa.

Katika maelezo yake, Sheikh Zubeir amesema Tanzania ipo katika kipindi kigumu cha ukame na joto kuwa kali, sio taifa hili pekee bali katika mataifa mbalimbali ulimwenguni yanakabiliana na hali hiyo.

Ametoa wito huo leo Jumatano Novemba 9, 2022 wakati akizungumza na wanahabari kuhusu mwenendo wa hali ya hewa uliopo Tanzania hasa changamoto ya ukame na ukosefu wa mvua katika baadhi ya mikoa.

“Mungu anatakiwa kuombwa hasa katika kipindi hiki mtu anatakiwa kujipinda zaidi, Mungu ndiye kumuitikia mtu aliyesikika, siku tano zilizopita nilizungumza suala la ukame, leo narudia tena kwa kuagiza Ijumaa ya wiki Waislamu kuomba ili tupate mvua yenye heri, isiyokuwa na madhara.

“Mikoa yote na wilaya zote tunaagiza maimamu wa misikiti na masheikh wa taasisi na maulamaa, tuiweke Ijumaa hii kuwa siku maalumu ya kumuomba Mungu, kwa pamoja na kila mtu atakapokuwepo,” amesema Sheikh Zubeir.

Sheikh Zubeir amesema Ijumaa Novemba 11 itakuwa siku maalumu na baada ya hapo wataendelea kumuomba kama kawaida katika utaratibu uliozeleka, kwani Mungu amehimiza kukitokea ukame basi watu wahimizwe kumuomba ili aweletee mvua.

“Tufanye wingi wa kumtaja Mungu na kumtaka msamaha, kujinyenyekeza na kujitupa kwake kwa kumuomba kwa wingi kwa sababu ni mwepesi wa kuitikia dua za waja wake,” amesema Sheikh Zubeir.


Amesema Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), makao makuu litatakeleza suala la kumuomba Mungu ili mvua inyeshe baada ya swala la Ijumaaa itakayofanyika katika msikiti wa kisasa wa Mohammed VI uliopo Kinondoni.

Amewataka Waislamu wa maeneo mbalimbali kuhudhuria ibada hiyo, akisema hali ya sasa inahitaji kumuomba na kumlilia Mungu ili kuletea ahueni.

Pia amesema misikiti yote ya mikoani iendelee kumuomba Mungu katika ibada zao kwa kuunganisha na masuala ya mvua na kutuepusha na majanga.