Mvua yasababisha vifo 33 Morogoro, Pwani

Muktasari:

  • Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetabiri mvua kubwa katika mikoa 14 ya Tanzania Bara na Zanzibar kuanzia leo Aprili 12, 2024

Dar es Salaam. Mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini, zimesababisha vifo vya watu 33 katika mikoa ya Morogoro na Pwani.

Kwa mujibu wa Msemaji wa Serikali, Mobhare Matinyi, mkoani Morogoro watu 28 wamepoteza maisha na wengine watano wamefariki mkoani Pwani.


Waandishi wa habari wakifuatilia mkutano wa Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi leo Aprili 12, 2024. Picha na Maelezo

Matinyi amesema hayo wakati Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ikitabiri uwepo wa mvua kubwa katika mikoa 14 ya Tanzania Bara na Zanzibar kuanzia leo Aprili 12, 2024.

Utabiri huo wa TMA ulitolewa Aprili 10, ikielezwa mvua kubwa inatarajiwa kunyesha kwenye maeneo ya Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, Pwani, Lindi, Mtwara, Rukwa, Iringa, Mbeya, Songwe, Njombe, Ruvuma na visiwa vya Unguja na Pemba.

"Athari zinazotegemewa ni mafuriko na kuathirika kwa shughuli za kiuchumi katika maeneo hayo," ilieleza taarifa ya TMA.

Hivi sasa mikoa inayopata mvua mara mbili kwa mwaka iko katika msimu wa mvua za Masika, zinazotarajiwa kumalizika Mei, 2024 kwa maelezo ya TMA.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 12, 2024 jijini Dar es Salaam, Matinyi amesema athari nyingine zilizotokea ni nyumba 1,035 kubomolewa na nyingine 6,874 kuzingirwa na maji.

“Ekari 34,970 za mazao yakijumuisha mahindi, mpunga, ufuta, pamba na mazao mchanganyiko zimeathirika, pia mifugo 1,466 imeathirika,” amesema.

Amesema miundombinu ya reli, barabara, makalavati na madaraja imeharibika katika Halmashauri za Malinyi, Mlimba, Ifakara, Mji wa Ulanga na Manispaa ya Morogoro.

Kwa mujibu wa Matinyi, kamati za maafa za wilaya na mikoa zinaendelea kufanya tathmini ya uharibifu na kuangalia kinachohitajika ili Serikali Kuu itoe misaada.

Amesema misaada imeanza kutolewa kutoka kwa wadau na imekuwa ikipelekwa kwa waathirika, ikiwamo ya dawa tiba ya maji, vyakula na huduma zingine.

Matinyi ametaja maeneo yaliyoathirika katika Mkoa wa Morogoro kuwa ni Halmashauri ya Mlimba na Mkoa wa Pwani, ni Kibiti na Rufiji.

Amesema kutokana na mafuriko yaliyotokea Morogoro, upo uhusiano kati ya bonde la Mto Kilombero na Mto Rufiji, akisema maji yanayotokea Kilombero yanachangia asilimia 62 ya maji ya Mto Rufiji.

Kuhusu athari mkoani Pwani, amesema mpaka sasa kuna vifo vya watu watano, viwili vikitokea Wilaya ya Rufiji na viwili Kibiti, huku Kisarawe kikitokea kimoja.

Amesema majeruhi walikuwa wawili wilayani Kibiti na wengine watatu Kisarawe.

“Lakini kuna uharibifu wa mazao mengi ya chakula, hasa mahindi, mpunga, ufuta, ndizi, mihogo na mtama pamoja na makazi, barabara, madaraja, nguzo za umeme, shule na Kituo cha Afya Mohoro, Rufiji,” amesema.