Mvua zinavyoitesa Dar, barabara zafungwa

Maji yakiwa yamefurika eneo la Jangwani barabara ya Kigogo kufuatia mvua zinazoendelea jijini Dar es Salaam jana.Picha na Omari Fungo

Muktasari:

Mamlaka ya hali ya hewa yabainisha sasa mvua kuendelea hadi Jumapili

Dar es Salaam. Si jambo la kushangaza mvua zinaponyesha kukuta maeneo mengi ya Jiji la Dar es Salaam yakiwa yamefurika maji.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam walisema wamechoka na hali hiyo.

“Nakwambia ipo siku hili jiji litaelea, angalia mvua kidogo hakuna pa kupita,” alisema Jackson Muhingo aliyelazimika kubadili njia baada ya eneo la Temeke kwa Sokota kujaa maji na wananchi kushindwa kupita.

Shule yaathirika

Pia, mvua hizo zilisababisha usumbufu kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Msasani kutokana na madarasa matano ya shule hiyo kujaa maji.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Edward Mollel, alisema kutokana na hali hiyo mahudhurio ya wanafunzi yamepungua kati ya wanafunzi 647, waliohudhuria ni 160.

Mollel alisema kawaida maji ya mvua hujaa kwenye madarasa matatu, lakini hizi zinazoendelea kwa siku tatu mfululizo, madarasa matano yamejaa maji na ofisi yake.

Barabara yafungwa

Hali hiyo ilisababisha barabara ya Morogoro eneo la Jangwani kufungwa kwa saa tatu kutokana na daraja kujaa maji, huku yakipita juu kwa kasi juu.

Barabara hiyo ilifungwa saa 5:40 asubuhi na kufunguliwa saa 8:48 mchana baada ya maji kupungua.

Kamanda wa polisi kikosi cha usalama barabarani Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Marson Mwakyoma alisema: “Tulilazimika kufunga barabara kipande cha Magomeni na Jangwani baada ya maji kupita juu ya daraja, jambo ambalo lingeweza kusababisha maafa.

Sido yazingirwa maji

Mvua hizo zimesababisha ofisi za Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido) iliyopo Kipawa Ilala, kuzingirwa na maji huku baadhi ya vifaa muhimu ikiwamo kompyuta na nyaraka zikiloa.

Tukio lilitokea saa 9:00 alasiri jana baada ya maji yanayodaiwa kuvunja ukuta unaotenganisha ofisi hiyo na reli ya Vingunguti eneo la Kipawa.

Mwananchi lilishuhudia baadhi ya wafanyakazi wa Sido wakiokoa vifaa na maji hayo yakiwa yamefika kimo cha kiuno, huku baadhi wakionekana kupanda mtumbi uliobuniwa na vijana wa maeneo hayo.

Diwani wa Kivule (Chadema), Wilson Mollel alisema barabara Kitunda Kivule haipitiki kutokana na uharibifu uliofanywa na mvua hizo.

Kauli ya TMA

Meneja wa kituo kikuu cha utabiri cha Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Samwel Mbuya alisema mvua zinazoendelea Pwani ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki na Kanda ya Ziwa Victoria ni sehemu ya mvua za masika.

Mbuya alisema zinatokana na kuimarika kwa ukanda wa mvua (ITCZ).

“Vipindi vya mvua za mfululizo baada ya kumalizika Jumapili vinatarajiwa kujirudia kuanzia katikati ya Mei 2019,” alisema Mbuya.