Mvuvi aeleza alivyokutwa na kimbunga baharini, ataja dalili zake

Mvuvi Ali Ramadhani akielezea mkasa wake wa kukutwa na kimbunga baharini, katika shughuli zake za uvuvi miaka iliyopita.  Picha na Rajabu Athumani

Muktasari:

  • Miongoni mwa dalili ambazo ukiziona ni ujio wa kimbunga ni wingu jeusi na giza muda huohuo ikiambatana na upepo wenye nguvu, hapo kama mvuvi  yupo baharini anatakiwa kutoka haraka.

Tanga. Mikoa ya ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi imeendelea kushuhudia uwepo wa kimbunga Hidaya na kuzua sintofahamu katika baadhi ya maeneo.

Kufuatia hali hiyo, Mwananchi Digital imezungumza na wavuvi akiwamo Ali Ramadhani (70) mkazi wa jiji la Tanga, anayesema alianza kuifanya kazi hiyo akiwa na miaka minane ya kuzaliwa akiambatana na a na baba yake, hivyo ana uzoefu wa kutosha na anajua vimbwanga vyote vilivyoko baharini.

Ramadhani anasema alishawahi kukutana na kimbunga akiwa baharini kwenye shughuli za uvuvi na wenzake watatu, lakini kabla hakijawakuta na kusomba mtumbwi wao, waliona dalili ya dhoruba kali.

Anasema wakiwa ndani ya jahazi, waliona wingu zito jeusi upande wao wa kulia na mara ukaanza kuvuma upepo mkali uliosababisha bahari kuchafuka.

“Na baada ya bahari kuchafuka chombo  (mtumbwi) kilichukuliwa na mawimbi kikawa kinasukumwa kuelekea upepo ulikokuwa unaelekea, hatukuwa na namna yoyote ya kujiokoa zaidi ya kushikilia mtumbwi kila mmoja asijue cha kufanya,” anasimulia Ramadhani na kuongeza;

“Kwa wale ambao hawajui dalili zake hasa wavuvi, utaona wingu jeusi na dunia yote itafunga giza saa ileile, halafu utaona kitu kama upepo unapuliza kama una jaribu vile halafu unakuja kwa nguvu sana, ukiona hivyo ujue hicho ni kimbunga.”

Hivyo anasema katika msukosuko ule, walijikuta wakitupwa ufukweni kwenye moja ya kisiwa kiko pwani ya bahari ya Hindi mkoani Tanga, na mtumbwi wao ulitupwa kwenye mchanga.

Anasema walijitahidi kuutoa mchanga na kuurudisha tena kwenye maji wakati huo hali ilikuwa imetulia kidogo, hivyo wakajisogeza hadi ng'ambo ya pili ya kisiwa hicho (hata hivyo hajakitaja jina).

Ramadhani anasema wakati huo wote watatu nguo zao zilichanwa chanwa na hekaheka za maji, na kule kung'ang'ania mtumbwi hivyo walibakia na nguo za ndani pekee na  walipofika ng'ambo ndio walisaidiwa na wavuvi wenzao nyingine wakavaa.

Anasema tangu siku hiyo mpaka leo, akisikia kuna tahadhali imetolewa kuhusu uwepo wa kimbunga, hawezi kuingiza mtumbwi baharini akihofia kukutana na dhoruba kama ile iliyotaka kuchukua maisha yake.

"Siku hiyo ndio nilipokoma nikisikia neno lolote kuhusu dhoruba za baharini siendi hata kidogo kuvua,” anasema mzee huyo.

Akisimulia kisa mkasa kilichomkumba naye akiwa baharini, Idd Omary ambaye anafanya biashara ya mkaa, anasema alikuwa anatokea Bagamoyo mkoani Pwani kuelekea Pemba kupeleka magunia ya mkaa kwa kutumia usafiri wa mtumbwi.

Omary anasema wakiwa wanaendelea na safari, mtumbwi huo ulipigwa na dhoruba ukapinduka na wao wakatupwa majini, hata hivyo anasema walifanikiwa kupanda juu ya mtumbwi huo uliokuwa unaendelea kupigwa na dhoruba.

Anasema kwa kuwa walikuwa wazoefu, walikaa juu ya mtumbwi ule mchana kutwa huku ukisukwa na upepo, kabla ya kuja kuokolewa na wenzao.

"Nilizama baharini Bagamoyo kipindi kirefu kidogo baada ya mtumbwi wetu kusukumwa na upepo na kupigwa na wimbi, hali ya hewa ilikuwa mbaya, kumbe kilikuwa kimbunga mtumbwi wetu ulibinuka ikabidi tukae kwa juu mpaka tunafika Pwani ya bahari, ila hali yetu ilikuwa mbaya kwa sababu ya baridi,” amesema Idd.

Wakati watumiaji hao wa vyombo vya majini wakisimulia hayo, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inatoa taarifa ya mwenendo wa kimbunga hicho kila mara kwa lengo la kuwapa tahadhari watu wananchi wakiwamo wanaofanya shughuli zao baharini.

Mwenyekiti wa mazingira wa soko la Deep Sea jijini Tanga, Hamisi Said amesema wavuvi wachache wameingia baharini leo lakini kwa tahadhari kubwa.

"Wenzetu wachache wameingia baharini kwa ajili ya kuendelea na shughuli za uvuvi ila tulichosisitiza ni kuzingatia suala la usalama wao, kama mamlaka zilivyotoa tahadhali kuwa inawezekana kutokea dhoruba baharini, hivyo wamebeba majaketi ya wokozi kama hali itabadilika waweze kujiokoa haraka,” amesema Said.

Naye kiongozi anayesimamia wavuvi, Ali Salehe amesema mpaka jioni hii, upepo uliokuwa ukivuma kwa kasi umeanza kutulia.

Anasema hata wale walioingia baharini kwenda kuvua wanaamini watarejea salama.

Mfanyabiashara wa samaki sokoni hapo, Salehe Jumanne amesema mpaka sasa upatikanaji samaki umeshuka kutokana na wavuvi wengi kuogopa kwenda kuvua,  hali iliyochangia bei kupanda maradufu.