Mwalimu mkuu aliyehukumiwa kwa madai ya kumbaka mwanafunzi aachiwa huru

Muktasari:

  •  Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyamkende alihukumiwa kifungo kwa kosa la kwanza la kumbaka mwanafunzi wake wa miaka 16 na la tatu la kumpa dawa za kutoa mimba na la pili la kumtia mimba

Bukoba. Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyamkende iliyopo Kijiji cha Nyamkende Wilaya ya Ngara, Enock Mabula, aliyefungwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kumbaka mwanafunzi wake, ameachiliwa huru na Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba.

Mwalimu huyo alihukumiwa kifungo hicho kwa kosa la kwanza la kumbaka mwanafunzi wake mwenye umri wa miaka 16 na la tatu la kumpa dawa za kutoa mimba, ambayo iliharibika ikiwa na miezi miwili, na kumwachia huru kosa la pili la kumjaza mimba.

Makosa hayo alidaiwa kuyatenda Oktoba 10,2022 saa 1:00 usiku katika Kijiji cha Nyankende Wilaya ya Ngara Mkoa wa Kagera.

Alikamatwa na polisi Desemba 12,2022 baada ya mwanafunzi huyo kumtaja mwalimu huyo kuwa mhusika wa ujauzito.

Hata hivyo, mwaka 2024 kupitia kwa mawakili Baraka Samula na Pauline Michael, alikata rufaa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba akiegemea sababu za rufaa.

Jana,  Aprili 25,2024 Jaji Imaculeti Banzi alikubali rufaa hiyo na kumwachia huru.

Maelezo ya kosa yalivyokuwa

Ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashitaka ulidai kuwa  Oktoba 10,2022 saa 1:00 usiku, mwanafunzi huyo alikwenda nyumbani kwa mshitakiwa baada ya kumuita walikula kisha mshitakiwa alidaiwa kumpeleka chumbani kwake.

Katika ushahidi huo ulidai kuwa siku hiyo alilala huko huko kwa mwalimu wake na kurudi nyumbani siku iliyofuata.

Novemba 2022, alienda tena nyumbani kwa mrufani na kuishi kama mke na mume na mwezi huo ndipo aligundua kutoziona siku zake.

Ilidaiwa kuwa alimweleza mrufani ambaye alimpa vidonge vinne kwa ajili ya kutoa mimba, na baada ya hapo aliona siku zake lakini zikaacha na baadaye akarudi nyumbani na Desemba 2,2022 alirudi tena kwa mrufani na waliishi pamoja hadi Desemba 6,2022.

Siku hiyo alirudi nyumbani baada ya mrufani kumpa dawa baada ya uwepo wa taarifa kuwa wazazi wa mtoto huyo walikuwa wakimtafuta, na aliporudi nyumbani, aliulizwa mahali alipokuwa na ndipo aliposema alikuwa nyumbani kwa mrufani.

Hapo ndipo alipopelekwa Kituo cha Polisi Rulenge, alipatiwa fomu ya polisi (PF3) na kwenda Hospitali ya Rulenge.

Baada ya kufanyiwa uchunguzi alibainika kuwa na ujauzito wa miezi miwili ambapo alimtaja mrufani kuwa ndio mhusika wa ujauzito.

Mrufani alikamatwa siku iliyofuata na kupelekwa Kituo cha Polisi Rulenge ambako hata hivyo alikanusha tuhuma hizo na Desemba 8,2022, mimba ya mtoto huyo ilitoka na kurudishwa tena hospitali alikolazwa hadi  Desemba 12, 2022 aliporuhusiwa.

Alivyojitetea mahakamani

Katika utetezi wake mbele ya Mahakama ya wilaya ya Ngara, mrufani ananukuliwa akikanusha tuhuma hizo na kuiambia Mahakama kuwa Desemba 6,2022 alipigiwa simu na polisi aliyemtaja kwa jina la Athman, akimtaka afike Polisi kuna mashitaka dhidi yake.

Alipofika Kituo cha Polisi, alihojiwa kuhusiana na tuhuma za kujaza mimba mwanafunzi wake, tuhuma alizozikanusha na baadaye alifikishwa kortini kwa tuhuma hizo.

Hata hivyo, katika utetezi wake, alikiri kuwa ni mwanafunzi wake na kueleza kuwa ingawa siku inayotajwa na upande wa mashitaka mkewe alikuwa amesafiri kwenda Kahama mkoani Shinyanga, alikuwa akiishi na watoto wengine wa kike wawili.

Alisema watoto hao wawili, walikuwa wakimsaidia katika shughuli za kilimo na kazi za nyumbani na kulingana na utetezi wake, tuhuma hizo zilikuwa ni za kupandikizwa kwa sababu tu ya chuki na kwamba mtoto huyo alipewa Sh55,000 ili amkandamize.

Mwisho wa kesi hiyo, Mahakama ya Wilaya ya Ngara ilimtia hatiani kwa kosa la kwanza la kubaka na kumhukumu kifungo cha miaka 30 na kosa la tatu la kumpa dawa za kutoa mimba na kumhukumu miaka mitatu lakini ikamwachia huru kosa la kumpa mimba.

Sababu za rufaa zilizomtoa gerezani

Mwalimu huyo mkuu hakuridhika na hukumu hiyo,  kupitia kwa mawakili wake, Baraka Samula na Pauline Michael alikata rufaa akiegemea sababu saba  ikiwamo kuwa hakimu alikosea kumtia hatiani kwa mashitaka ambayo hayakuthibitishwa.

Hoja nyingine ni kuwa hakimu alishindwa kuutilia maanani ushahidi mzito wa upande wa utetezi kulinganisha na ule wa upande wa mashitaka na pia alikosea kumtia hatiani bila daktari aliyempima mtoto na kubaini ana ujauzito kutoa ushahidi wake.

Pia, alisema hakimu huyo alikosea kufikia uamuzi wa kumwachia huru katika kosa la pili la kumpa mimba mtoto huyo na kumtia hatiani katika kosa la kubaka bila kuzingatia na kuthibitisha vigezo vya lazima kuthibitishwa vya kosa la kubaka kwa mujibu wa sheria.

Hoja nyingine ni kuwa Mahakama ilikosea kisheria kutafsiri na kuutilia manani ushahidi uliotolewa na mtaalamu wa utabibu kuhusiana na mashitaka, ilimtia hatiani huku taarifa ya kubaka ilichukua muda mrefu kuripotiwa na pia haikuchunguza tabia ya mwathirika.

Upande wa Jamhuri, ulitaka hoja hizo zitupwe na kwamba mashitaka dhidi ya mshitakiwa yalithibitishwa na wala kulikuwa hakuna kujikanganya kwa mashahidi.

Jaji alivyomwachia huru

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Jaji Immaculate Banzi alisema ni wajibu wa Mahakama hiyo kupima kama kesi dhidi ya mshitakiwa ilikuwa imethibitishwa bila kuacha shaka na kwa viwango vinavyokubalika kisheria kumtia hatiani.

Kwa kuanzia, Jaji Banzi alisema hakuna ubishi kuwa ushahidi wa upande wa utetezi haukuzingatiwa kabisa na hakimu aliyesikiliza shauri hilo kwa kuwa, baada ya kuchambua kwa kirefu ushahidi, hakimu aliyesikiliza kesi hakugusa kabisa ushahidi wa utetezi.

Jaji alisema ni msimamo wa sheria kuwa kabla ya hakimu kuuamini ushahidi wa mwathirika wa tukio la ubakaji, ni lazima ahakikishe ushahidi wa mwathirika kama ilivyo katika kesi hiyo, unapaswa uwe ni wa ukweli na ukweli mtupu na si vinginevyo.

Kulingana na Jaji, hakimu aliyesikiliza kesi hiyo alipaswa kuchambua na kupima ushahidi wa pande zote mbili kabla ya kufikia hitimisho kuwa kesi ya upande wa mashitaka ilikuwa imethibitishwa pasipo kuacha shaka, wajibu ambao hakimu aliukwepa.

Kuhusu kama kesi ya upande wa mashitaka ilithibitishwa, Jaji alianza na suala la umri wa mtoto linapaswa kuthibitishwa na mtoto mwenyewe, baba au mama yake na katika kesi hiyo, mtoto alisema alizaliwa Juni 30,2006 hivyo hana ubishi na umri wa mtoto.

Jaji akazungumzia hoja ya kwamba mtoto aliingiliwa kama ilithibitishwa, na  katika ushahidi wake mtoto alieleza alifanya mapenzi na mrufani siku tofauti tofauti kuanzia Oktoba 10,2022  na kuna wakati walifikia mahali waliishi kama mume na mke.

Kutokana na mahusiano hayo kwa mujibu wa Jaji, Novemba 2022 mtoto huyo hakuona siku zake hivyo akashuku ana mimba na baada ya mrufani kujulishwa hilo ndio akampea vidonge vinne ili atoe mimba hiyo lakini mimba hiyo haikutoka kwa siku iliyotarajiwa.

Mrufani alikanusha kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwathirika na kwamba kipindi mkewe amekwenda kujifungua Kahama, pale nyumbani kwake alikuwa akiishi na watoto wengine wawili wa kike na wa kiume mmoja aliyekuwa akifanya kazi saluni.

Hata hivyo Jaji alisema katika makosa ya kujamiiana, ushahidi bora unapaswa kutoka kwa mwathirika mwenyewe lakini ni kanuni za sheria kuwa maneno yanayotoka kinywaji mwake na hayawezi kuchukuliwa kama ya Injili bali ni lazima yapitie vipimo vya ukweli.

“Kama mrufani angekuwa anaishi na mwathirika (mtoto) ni lazima kuna watu wangefahamu maisha yao kwa sababu maisha ya mume na mke hayawezi kuwa ya kificho bila wao kuonwa na watu wengine,”alisema Jaji Banzi katika hukumu hiyo.

“Badala yake kuna ushahidi wa utetezi kuwa wakati mkewe ameenda kujifungua Kahama, mrufani alikuwa akiishi na shahidi wa 3 na wa 4 wa upande wa utetezi na hakuna hata mmoja wao alimuona mrufani akiishi na mtoto huyo,”alieleza Jaji.

“Kwa kuongezea, kulikuwa hakuna uwezekano wa mrufani na mwathirika kuishi pamoja kama mke na mume bila mashahidi hao wawili kubaini mahusiano hayo”

Jaji alisema ushahidi wa shahidi wa 4 wa Jamhuri ambaye ni mama wa mtoto, alisema mwanaye aliondoka nyumbani Desemba 2,2022 akiaga anakwenda kwa rafiki yake lakini hakusema kama kuna siku nyingine aliondoka nyumbani wala kushuku uhusiano wao.

“Wala hakusema chochote kuwa mwanaye alilala nje ya nyumbani kwao usiku wa tukio. Ushahidi wake ulijikanganya na ushahidi wa mtoto ambaye simulizi zake zilikuwa zinabadilika mara kwa mara katika tukio moja analolielezea,”alieleza Jaji Banzi.

“Mwanzo alisema alikuwa nyumbani kwa mrufani kuanzia Oktoba 3,2022 lakini baadae akaja kusema alianza kuishi na mrufani Novemba 2022 na kulikuwa hakuna uthibitisho kuwa siku alipoaga anakwenda kwa rafiki yake kama alikwenda kwa mrufani.

“Yote hayo yanatia shaka juu ya ukweli wa ushahidi wake kwamba siku ya tukio alienda nyumbani kwa mrufani na walifanya mapenzi lakini lalamiko lingine la mrufani ni namna mwathirika alivyochukua muda mrefu kumtaja mrufani kuwa ndiye aliyembaka.

“Kulingana na mwathirika mwenyewe, alidai alibakwa Oktoba 10,2022 na siku iliyofuata alirudi nyumbani. Hata hivyo, baada ya kufika nyumbani hakusema chochote juu ya kubakwa achilia mbali kumtaja mrufani kuwa ni mbakaji,”alisema Jaji.

“Aliendelea kukaa kimya hadi Novemba 6, 2022. Hatuwezi kudhania kuwa hakumtaja mrufani katika tarehe za mwanzoni kwa sababu ya ahadi ya kuolewa kama Jamhuri wanavyoeleza kwa sababu hata mtoto mwenyewe hakueleza kwanini alichelewa”

Kuhusu kosa kuwa Oktoba 10,2022 mrufani alimpa mtoto huyo dawa za kutoa mimba, Jaji alisema katika ushahidi wake mtoto alieleza ni mwezi Novemba ndio mrufani alimpa vidonge hivyo na akameza vidonge viwili na viwili aliviingiza kwenye uke wake.

Pia, alieleza katika ushahidi wake kuwa Desemba 6,2022 mrufani alimpa tena vidonge vinne hivyo Jaji akasema ukiacha kutofautiana huko, kulikuwa hakuna ushahidi wowote wa kitaalumu kuwa vidonge alivyopewa vingeweza kutoa mimba.

Baada ya uchambuzi huo, Jaji Banzi alisema anaona upande wa mashitaka haukuweza kuthibitisha mashitaka hayo bila kuacha shaka hivyo Mahakama inabatilisha kutiwa kwake hatiani na adhabu aliyopewa na kuamuru aachiliwe mara moja kutoka gerezani.