Mwananchi, Aga Khan Foundation wapanda miti Dar

Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Ltd, Bakari Machumu (mwenye fulana ya bluu), akishiriki shughuli ya upandaji miti katika Shule ya Msingi Kilimani, iliyopo  Manispaa ya Ubungo jijini Dar es Salaam. Picha na Bakari Kiango.

Muktasari:

Awamu ya kwanza ya kupanda miti katika shule za msingi za Ubungo jijini Dar es Salaam inayotekelezwa na Mwanachi Communications Ltd (MCL) na Aga Khan Foundation (AKF), imekamilika kwa kuzifikia shule 25 zilizootesha misitu midogo inayorekebisha hali ya hewa na kukabiliana na hewa chafu.

Dar es Salaam. Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa ushirikiano na Aga Khan Foundation (AKF),  wamekamilisha awamu ya kwanza upandaji wa miti katika shule msingi 25 katika Manispaa ya Ubungo jijini hapa.

Hatua ya upandaji wa miti inayounda msitu midogo ndani ya shule inalenga kuleta faida mbalimbali, ikiwemo kuboresha mazingira ya kujifunza na kufundishia pamoja na kuboresha hali ya hewa na kukabiliana na hewa chafu.

Akizungumza na wanahabari leo Ijumaa Machi 22, 2024 baada ya kupanda miti hiyo katika shule ya msingi Kilimani, Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Bakari Machumu amesema misitu midogo ni suluhisho kwa maeneo ya mijini yenye nafasi finyu katika kuotesha miti.

 “Wezetu wa AKF wamekuja na huu ubunifu na sisi tukasema tuungane nao, upandaji hauchukui nafasi kubwa, lakini unaweza kutengeneza msitu mdogo. Ukiangalia hapa shule ya Kilimani ni kama hatua 10 kwa 10, ni eneo dogo lakini inapandwa miti 210.

“Miongoni mwa miti hiyo ni ya matunda, dawa na ile inayofyonza hewa ya ukaa. Ukiweza kuwa na kitu kama hiki kila ofisi au eneo, basi katika mji utaona ndani ya muda itakavyoweza kufyonza hewa ukaa,” amesema Machumu.

Amebainisha kuwa mpango wa MCL mwaka huu ni kupanda miti 15,000 kwa mfumo wa msitu mdogo na awamu ya kwanza wamepanda miti 5,000 katika shule za msingi 25, akisema wataendelea na mchakato huo hadi kufikisha idadi walioipanga.

“Unaweza kusema ni midogo, lakini tulikuwa hatufanyi kabisa ila tumeanza na tutatumia vyombo vya habari kuelemisha, tunaamini sisi kama daraja la wananchi kwa kuonyesha kwa vitendo maana yake wengine watapata ufahamu zaidi,” amesema Machumu.

Amesema MCL ni chombo cha habari kinachotoa taarifa zake kupitia magazeti na mitandao ya kijamii, hivyo wanapofanya uchapishaji wanatumia karatasi zinazotokana na miti.

“Tulijitafakari tukasema katika vuguvugu lote la kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, sisi watumiaji tunafanyaje ili kurudisha ile sehemu tunayoichukua.

“Tuliamua badala ya kuendelea kutoa habari, tushiriki kwa vitendo kwa kuungana AKF ili kuja na dhana mpya ya misitu midogo,” amesema Machumu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa AKF nchini, David Siso amesema lengo la taasisi hiyo ni kukabaliana na mabadiliko ya tabia ya nchi, hivyo wamekuwa mstari wa mbele kushiriki katika shughuli za upandaji miti katika maeneo mbalimbali.

“Mkakati wa Aga Khan Foundation katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi tunajihusisha na upandaji wa misitu midogo, kupanda mikoko katika maeneo ambayo yameharibiwa na usafishaji wa bahari,” amesema Siso.

Amesema katika miti iliyopandwa kwenye shule ya msingi Kilimani ipo ya maua na ile itakayowasaidia wanafunzi hao kujifunza kwa vitendo kuhusu miti katika somo  la bailojia.

Naye Ofisa elimu ya awali na msingi wa Manispaa ya Ubungo, Denis Nyoni, amesema hatua hiyo inalenga kutengeneza mazingira rafiki katika ujifunzaji na ufundishaji.

“Faida ya kupanda miti ni pamoja na kutunza mazingira kwa sababu itapunguza joto wakati wa mchana wanafunzi wanapokuwa darasani na kuboeresha hali ya hewa,” amesema Nyoni.

Mkuu wa shule ya Kilimani, Zubeda Jane amesema watahakikisha wanaitunza miti ili malengo yaliyowekwa yafikiwe.

Amesema miti waliyopanda imeshawekwa mbolea kazi yao ni kuilinda, kuitunza na kuimwagilia maji.

Mkurugenzi wa Shirika la Utu na Mazingira (Hudefo) lililoshiriki shughuli hiyo, Sarah Pima amesema wanashirikiana na AKF na MCL katika kuhakikisha miti inayopandwa inatunzwa na kustawi.

Pima amesema kila shule inayopandwa, Hudefo inahakikisha kunakuwa na usimamizi mzuri, sambamba na kuwajengea uwezo wanafunzi kuhusu hatua mbalimbali za upandaji wa miti na faida zake.