Mwenyekiti wa kitongoji aliwa na mamba akivua samaki

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Kitongoji cha Chapuya, kata ya Migoli Laurent Sigala amekufa akidaiwa kuvamiwa na mamba wakati akivua samaki katika Bwawa la Mtera.

Iringa. Mwenyekiti wa Kitongoji cha Chapuya Kata ya Migoli, Wilayani Iringa Laurent Sigala amepoteza maisha baada ya kuvamiwa na mamba wakati akivua samaki katika Bwawa la Mtera.

Chapuya ni Kitongoji kilicho pembezoni mwa Bwawa la Mtera linalodaiwa kuwa  na mamba pamoja na viboko wengi ambao huambaa kutoka Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, mkoani Iringa.

Hata hivyo, shughuli kuu ya wakazi wa Chapuya ni uvuvi licha ya kuwapo kwa wanyama hao wakali kwenye bwawa hilo.

Akizungumza na Mwananchi leo Desemba 11, 2023 Diwani wa Kata ya Migoli, Benitho Kayugwa amesema tukio hilo limetokea mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya mvuvi huyo kuingia bwawani kwa ajili ya uvuvi

"Sigala aliaga kwenda bwawani kuvua samaki lakini ikatokea hajarudi na hii haikuwa kawaida yake. Wananchi na familia yake wakaanza kumtafuta bila mafanikio," amesema Kayugwa na kuongeza:

"Kumbe eneo alilokuwa anavua kulikuwa na mto unaingia kukawa na kasi ya maji hivyo mamba alipovamia mtumbwi alishindwa kujinusuru. Alikatwa kiwiliwili ikabaki sehemu ya juu na maji yakampelela ng'ambo nyingine. Tuliokota tu sehemu ya juu na tumeshamzika."

Kayugwa amekiri kuwepo kwa mamba na viboko kwenye bwawa hilo ambalo ni tegemeo la wakazi wanaolizunguka kutokana na kuwepo kwa shughuli za uvuvi.

Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, Allan Bukumbi amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo mwishoni mwa wiki iliyopita.


Baadhi ya wakazi wa Chapuya wameiomba Serikali kuweka utaratibu wa kuvuna wanyama hao ili kuepusha hatari ikiwemo kujeruhiwa au kuuawa.

"Haya ndio maisha yetu, tunaomba Serikali itusaidie, ivune hawa wanyama hatari. Wapo watu walio nusurika," amesema Joyce Ntali mkazi wa eneo hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego  akiongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama walienda Chapuya kutoa pole kwa msiba huo na kuona mazingira ya uvuvi.