Nape: Uhuru wa habari sasa kulindwa kisheria

Wadau wa sekta ya habari wakifuatilia kongamano la maendeleo ya sekta hiyo katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam juzi. Picha ya Ericky Boniphace

Muktasari:

  • Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema Serikali imeanza kuwezesha kulinda uhuru wa habari kwa mujibu wa sheria na si utashi wa viongozi.

Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema Serikali imeanza kuwezesha kulinda uhuru wa habari kwa mujibu wa sheria na si utashi wa viongozi.

Kauli hiyo ya Nape imewaridhisha wadau wa sekta ya habari kwa jitihada zinazofanywa kuhakikisha kunakuwa na uhuru wa vyombo vya habari kwa kuweka mazingira wezeshi na salama ya kufanya yanayokusudiwa na jamii.

Nape alisema hayo jana, wakati wa kongamano la maendeleo ya sekta ya habari lililoandaliwa na wizara yake, akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan aliyealikwa kuwa mgeni rasmi.

Waziri huyo alisema safari ya kuboresha mazingira ya habari inaanza kwa kuifanyia marekebisho Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 kuanzia Januari mwakani.

Alisema marekebisho ya sheria hiyo ni mwanzo wa safari ya kuwezeshwa uhuru wa habari kulindwa kwa mujibu wa sheria na si utashi na kila kiongozi atakayekuja atapaswa kuheshimu yaliyoainishwa kwenye sheria.

Waziri huyo alieleza kuwa ili Taifa liwe na maendeleo, furaha na amani ni lazima kuwe na uhuru wa habari hivyo maboresho hayo yanalenga kuuimarisha kwa maslahi mapana ya Taifa.

“Hakuna furaha, amani na maendeleo kama uhuru wa habari katika jamii hiyo haupo, hivyo ni muhimu kulinda uhuru wa habari ili vitu hivi viwepo kwenye jamii.Hilo linawezekana na huo ndio msingi wa kongamano hili ambalo linalenga kuleta maendeleo, furaha na msingi wa Taifa letu,” alisema Nape.

Waziri huyo alisisitiza kuwa sheria na kanuni mbalimbali zinaendelea kufanyiwa mabadiliko kuhakikisha kunakuwa na uhuru wa habari unaopaswa kulindwa kisheria, si utashi wa viongozi.

“Kiongozi yeyote atakayekuja atalazimika kuulinda uhuru huu kwa mujibu wa sheria hata kama hataki,” alisema Nape.

Waziri huyo pia aliwataka wadau wa sekta ya habari kuwa kichocheo cha kukua kwa sekta nyingine, akieleza kuwa uhusiano kati ya Serikali na vyombo vya habari unaendelea kuimarika.

“Zile kelele zimepungua, kama zipo basi ni kidogo. Hakuna mtu anafungwa mdomo, hakuna anayezuiwa kusema, lakini hili litakwenda kukamilika pale litakapolindwa kisheria na kazi hiyo inakwenda kufanyika Januari. Serikali iko tayari kupeleka marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari bungeni. Sambamba na hili tunaona haja ya kuifanyia mapitio sera ya habari,” alisema.

Akizungumza katika kongamano hilo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile alisema licha ya vyombo vya habari kuonekana kuwa huru hivi sasa, wadau wanaamini uhuru zaidi utapatikana pindi sheria itakapofanyiwa marekebisho.

Balile alisema Serikali imelegeza ugumu uliokuwa unaikabili sekta hiyo na kuvifanya vyombo vya habari kuanza kupumua.

“Kuna wakati sheria zilikuwa kitanzi kwa magazeti, yalifungiwa na uhuru ukapotea kabisa. Ilipokuja Serikali ya awamu ya sita yamefanyika maboresho makubwa. Rais aliondoa mtanziko uliokuwepo na sasa tuna raha kwa kweli. Hata hivyo, tunaamini utulivu huu utalindwa kisheria baada ya kufanyika marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari kama ambavyo tumeahidiwa, ingawa kwa sasa wadau tunafurahia kiwango cha uhuru wa habari kilichopo,” alisema Balile.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (Misa) Tanzania, Salome Kitomari alisema kwa muda mrefu haijasikika kauli kama hiyo kutoka kwa msimamizi wa sekta ya habari, tofauti kama anavyofanya waziri mwenye dhamana aliyesema hakuna amani, furaha wala maendeleo bila uhuru wa vyombo vya habari.

“Hii inakwenda kufungua ukurasa mpya kwa sababu kwa muda mrefu waandishi wa habari tumeonekana wachochezi kila tunapoandika habari za kukosoa.Wanahabari tunafanya kazi kwa kuzingatia misingi ya taaluma yetu, tunapokwenda sehemu na kuripoti kuhusu ubovu wa barabara, uhaba wa maji, ukosefu wa shule lengo letu sio kuisumbua Serikali wala kutaka uadui nayo, tunachotaka ni uwajibikaji na si vinginevyo,” alisema Salome.

Mwanahabari mkongwe nchini, Kibwana Dachi alisema kauli ya waziri inaonyesha Serikali imeamua kuviacha vyombo vya habari kufanya kazi kwa uhuru na kutekeleza misingi ya kazi yao ya kuuhabarisha umma bila kuhofia chochote.

“Kiukweli kuna kipindi sekta ya habari ilipitia sintofahamu, uhuru haukuwepo, lakini tuna mambo yanabadilika, Serikali inaonyesha kutambua umuhimu wa vyombo vya habari na wanahabari kuwa huru. Kitendo cha waziri kutambua changamoto za wanahabari, likiwamo suala la maslahi linaonyesha sasa tuko pamoja,” alisema Dachi.

Suala la maslahi ya wanahabari lilizungumziwa pia na Mkurugenzi wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Kenneth Simbaya aliyesema lilichangia kwa kiasi kikubwa kwenye ukiukwaji wa maadili ya uandishi.

Alisema idadi kubwa ya waandishi waliopo nchini hawajaajiriwa na wanalipwa kutegemea habari wanazoandika kwa mwezi, hali inayowaweka katika hatari ya kukiuka misingi ya kazi yao kwa masilahi binafsi na si ya umma.

Hoja ya maslahi ya waandishi ilizungumziwa pia na Waziri Nape, ambaye aliahidi kuanzia mwakani wizara itaweka nguvu za kutosha kulifuatilia jambo hilo, akieleza kuwa halipaswi kuachwa kama lilivyo sasa.

Akiwasilisha mada kwenye kongamano hilo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga alisema sekta ya habari inakabiliwa na changamoto ya kuwapo kwa sheria zenye vipengele visivyo rafiki na matumizi mabaya ya sheria yanayonyima uhuru wa wanahabari, akitolea mfano zuio la utoaji wa taarifa.


MCL yang’ara

Katika kongamano hilo, mwandishi wa gazeti la The Citizen linalochapishwa na kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Jacob Mosenda alitunukiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na teknolojia kwa mchango wake anaoutoa kwenye sekta hiyo kupitia kazi zake za habari.

Utambuzi huo wa Mosenda ulienda sambamba na kukabidhiwa tuzo ya mwandishi bora wa habari za elimu pamoja na waandishi wengine watano.

Licha ya tuzo hizo za waandishi, wizara zinazoongoza kwa kutoa taarifa, kushirikiana na vyombo vya habari na kutumia mitandao ya kijamii nazo zimepewa tuzo ambapo Wizara ya Afya iliibuka kidedea kati ya wizara 10 zinazoongoza kwa kutoa taarifa na habari kwa umma.

Wizara nyingine zilizofuata ni Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mazingira, Maliasili na Utalii, Mambo ya Ndani, Kilimo na Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto. Nafasi ya 10 ilishikwa na Wizara ya Habari.