Ndugu wanne wa familia moja waliofariki ajalini kuzikwa tofauti

Waombolezaji wakiwa Mbezi Beach jijini Dar es Salaam nyumbani kwa marehemu Dk Norah Msuya ambaye ni mmoja wa wanafamilia wanne waliofariki kwenye ajali Chalinze Mkoa wa Pwani. Picha na Michael Matemanga. 

Muktasari:

  • Waliofariki kwa ajali kuzikwa tofauti, Neech ataagwa kesho na kuzikwa Ugweno mkoani Kilimanjaro.

Dar es Salaam. Miili ya ndugu wanne wa familia moja waliofariki Agosti 2 katika ajali ya gari iliyotokea wilayani Chalinze mkoani Pwani inatarajiwa kuzikwa tofauti, mmoja akisafirishwa kwenda Ugweno na wengine watatu wakitarajiwa kuzikwa hapa Dar es Salaam.

 Kaka wa familia hiyo Neech Msuya ndiye atakazikwa Ugweno mkoani Kilimanjaro ambapo shughuli ya kumuaga zitafanyika kesho katika Hospitali ya Lugalo.

Msemaji wa kamati ya maandalizi ya mazishi, Aminata Juma amesema baada ya wanafamilia kurejea kutoka Ugweno taratibu za mazishi ya waliosalia zitafanyika kwa Diana, Sia na Dk Norah kuzikwa katika makaburi ya Kondo jijini Dar es Salaam.

“Kesho (Jumamosi) tutakutana saa sita kamili Lugalo kwa ajili ya kumuaga Neech ambaye atapelekwa Ugweno saa nane mchana kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika Jumapili.

“Tarehe 6 walioenda kuzika watarudi na wazazi baba na mama kuja Dar kwa ajili ya shughuli za waliosalia.

Imekubalika Sia na Norah wataagwa hapa katika nyumba ya Dk Momburi.

Amesema Diana atapelekwa Toangoma kwa familia ya mumewe aitwaye Mageta kabla ya siku ya mazishi kuungana na ndugu zake wengine.

“Agosti 8 tutakuwa na ibada ya pamoja kwa wote wa tatu hadi sasa imekubalika viwanja vya gofu Kawe kisha wote watazikwa makaburi ya Kondo Ununio,” amesema Aminata.