NIT yawaita Watanzania kwenda kukagua magari yao

Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, (katikati mwenye suti) akipokea maelekezo kutoka kwa mmoja wa wakaguzi wa magari waliopo kituo cha ukaguzi wa magari NIT baada ya kukitembelea leo hii, kulia kwake ni Mkuu wa chuo hicho Profesa Zacharia Mganilwa. Picha na Sute kamwelwe.

Muktasari:

  • Hatua hiyo imetajwa kuwa na umuhimu mkubwa kwa wasiofanya ukaguzi wa magari yao mara kwa mara kwani kufanya hivyo kunapunguza ajali ambazo zimekuwa mithili ya jinamizi linaloendelea kuwatafuna Watanzania walio wengi.

Dar es Salaam. Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), kimewataka Watanzania kwenda kufanya ukaguzi wa magari yao ikiwa ni njia moja wapo ya kuzuia hatari ya kutokea kwa ajali.

Hatua hiyo imebainishwa kuwa na umuhimu mkubwa kwa wasiofanya ukaguzi wa magari yao mara kwa mara kwani kufanya hivyo kunapunguza ajali ambazo zimekuwa kama jinamizi linaloendelea kuwatafuna Watanzania walio wengi.

Akizungumza kwenye ziara ya kikazi ya Naibu Waziri wa Uchukuzi iliyofanyika chuoni hapo leo Septemba 29, 2023, Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Zacharia Mganilwa amesema gari linapaswa kuwa bora na ubora unatokana na ukaguzi wa mara kwa mara ili mtumiaji awe na uhakika.

“Kituo hiki kilijengwa kwa ajili ya kufundishia wanafunzi ukaguzi wa magari kwa waajiriwa wa maofisa wa polisi wakaguzi wa magari na wale waliopo taasisi za bima lakini pia kina kazi ya pili ya kufanya ukaguzi mkubwa wa magari.

“Lazima ujue hali ya gari lako ukitaka kujua ubora wa gari lako lilete tunakagua mifumo zaidi ya 15 muhimu hasa ile inayoendana na usalama wa gari kama breki,” ameweka wazi Profesa Mganilwa.

Awali, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile alisema Mamlaka zinazohusika kukagua magari barabarani ziongeze juhudi ili kunusuru maisha ya watu wasio na hatia yanayopotea kutokana na ajali.

Akigunzumzia changamoto iliyopo Naibu Waziri amesema kwa takwimu zilizopo nchi inamagari zaidi ya milioni mbili na nusu na nusu yake yapo Dar es Salaam, hivyo kituo hicho bado ni kidogo lakini ameagiza uongozi kubuni maeneo mengi zaidi ili watu wapate sehemu za kukagulia magari yao.

Mbali ya hilo Kihenzile ametoa agizo kwa uongozi wa chuo hicho kusimamia ujenzi wa mabweni ya wanafunzi yanayojengwa chuoni hapo kukamilika kwa wakati pia kwa kuzingatia ubora ili wanafunzi wasome katika mazingira bora.

Kutokana na ukubwa wa chuo hicho ambacho kwa sasa kina wanafunzi zaidi ya 15,000 kutoka 2, 000 miaka ya nyuma, Kihenzile ametoa wito kwa uongozi wa chuo kuendelea kubuni ujenzi wa majengo mengi zaidi.

 “Nimetembelea hapa NIT ikiwa ni muendelezo wa ziara yangu ya kikazi nimeona mageuzi makubwa yaliyofanyika hapa na nitoe pongezi ikiwemo miradi ya ujenzi. Nimeridhishwa hata na hatua iliyopo sasa ya kufundisha fani ya matengenezo ya ndege kwa njia ya kidijitali hapahapa chuoni sio hadi watu waende ulaya ni hatua kubwa,” amesema Kihenzile.