Njia za kuepuka kulipukiwa na simu janja

Njia za kuepuka kulipukiwa na simu janja

Muktasari:

  • Umewahi kusikia simu janja imelipuka? Unajua unawezaje kuepuka hilo? Wataalamu wa teknolojia ya mawasiliano (IT) wanafafanua.

Dar es Salaam. Umewahi kusikia simu janja imelipuka? Unajua unawezaje kuepuka hilo? Wataalamu wa teknolojia ya mawasiliano (IT) wanafafanua.

Wataalamu hao wametoa ufafanuzi huo ikiwa zimepita wiki chache tangu kutokea kwa tukio la mtu kulipukiwa na simu janja ikiwa mfukoni, jijini Dar es Salaam.

Ingawa wengi hudhani simu inaweza kulipuka wakati wa kuitumia, lakini hii ilikuwa tofauti, kwani ililipuka ikiwa mfukoni.

Pia mkoani Njombe, mtu mmoja akiwa kwenye bajaji simu yake ililipuka, ilikaribia kusababisha vifo kwa abiria wenzake.

Akitangaza tukio hilo, Julai 23, mwaka huu, kamanda wa polisi wa mkoa huo, Hamis Issa alisema, “abiria waliokuwa wamepanda kwenye bajaji mmoja wao simu ililipuka, kukaanza kuwa na taharuki na hatimaye kulikuwa na mshikemshike humo ndani ya bajaji.”

Ingawa matukio hayo hutokea mara chache, wataalamu wa IT wanasema hali hiyo inasababishwa na changamoto katika betri inayotokana na kukiukwa kwa taratibu sahihi za matumizi.

Msomi wa IT anayejishughulisha na ufundi simu eneo la Kariakoo, Dar es Salaam, Nichorous Deus alisema mlipuko wa simu yoyote pamoja na sababu nyingine, lakini betri ndiyo chanzo kikuu.

Hadi simu inalipuka, alisema betri inakuwa imezidiwa uwezo wa kustahimili kiwango cha umeme inachopokea kutoka katika chaja.

“Kuna watu wanatumia chaja zenye uwezo mkubwa zaidi ya betri ‘fast charger’, hii inasababisha betri kuzidiwa na ikitokea hivyo inavimba bila mmiliki kujua.

“Haupaswi kuacha simu yako kwenye chaji usiku wote, hakikisha unaichaji kwa saa tatu tu, kisha ikijaa unaitoa, epuka kuitumia wakati unaichaji maana itazalisha joto,” alisema. Kauli hiyo inaungwa mkono na Osiana Sanga, mtaalamu wa simu janja anayesema baadhi ya michezo ‘games’ ni hatari kwa simu, hasa inayokatazwa kutumiwa na aina fulani ya simu.

“Kuna programu zina uwezo mkubwa zaidi ya simu, hii unaipa simu kazi isiyostahili kwa maana unailazimisha kufanya nje ya uwezo wake, ikishindwa italipuka,” alisema.

Alisema kabla ya kupakua programu tumizi ni vema kuhoji kwa wataalamu iwapo inastahili kuhifadhiwa katika simu husika.