Nyani wazua taharuki Moshi, wananchi watelekeza mashamba yao

Muktasari:

  • Nyani na tumbili wanaokula  mahindi machanga na mifugo wamegeuka kero katika Kitongoji cha Nyawenda, Kata ya Makuyuni, Wilaya ya Moshi na kuwalazimisha wananchi  kuyakimbia mashamba yao.

Moshi. Wananchi wa Kitongoji cha Nyawenda Wilaya ya Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro wamelazimika kuyakimbia mashamba yao kutokana na uvamizi wa nyani na tumbili.

Wanyama hao wanaovamia mashamba hayo na kula mahindi machanga na mifugo ikiwamo kuku, bata na mbuzi kwenye makazi yao.

Nyani wazua taharuki Moshi, wananchi watelekeza mashamba yao

Nyani hao ambao hutembea makundi nyakati za asubuhi na jioni, wamezua hofu na taharuki miongoni mwa wananchi kutokana na wingi wao kwenye makazi yao.


Mchungaji Samwel Msacky, mkazi wa Kitongoji cha Nyawenda, Kata ya Makuyuni, Wilaya ya Moshi akizungumzia uvamizi wa nyani kwenye makazi yao. Picha na Janeth Joseph


Wamesema mbali na nyani hao kula mazao mashambani, wakifunga maeneo ya makazi nyani hufungua milango na kuingi ndani na kula chakula chochote wanachokikuta.

Wakizungumza na Mwananchi, wananchi hao wamesema nyani hao wanawasababishia usumbufu mkubwa na kuwafanya washindwe kulima, wakihofia mazao yako kuliwa.

Akizungumzia uvamizi huo, mmoja wa wananchi wa kitongoji hicho, Joyce Mallya amesema amelazimika kutelekeza mashamba yake kutokana na uharibifu unaofanywa na nyani, ikiwemo kung'oa na kula mazao, hususan mahindi.

“Nyani wameniathiri sana, wamenitesa sana, mwaka jana waliingia shambani kwangu wakavunja mahindi yakiwa bado machanga na walivunja shamba zima, karibu ekari moja na sikupata chochote," amesema Mallya.

Amesema pamoja na kula mazao yake, nyani hao walivamia nyumbani kwake na kukamata kuku na bata waliokuwa bandani, wakafungua mlango wa nyumba wakaingia ndani na kula vyakula vyote vilivyokuwamo.

"Cha kushangaza hawa nyani wanaingia ndani wanaiba hadi kuku, wanakula kila kitu wanachokutana nacho. Ukiwafukuza hawaondoki, niliomba msaada kwa jirani mwanaume alipofika kuwafukuza wakaondoka, tatizo ni kubwa,” amesema Mallya.

Amesema msimu huu ameshindwa tena kulima akihofia mazao yake kuliwa na nyani hao.

“Hili shamba langu ndio lilikuwa likinipatia chakula misimu yote, nimebaki hivyo hivyo, nimebaki kuomba chakula kwa watu, naomba Serikali inisaidie na itusaidie kuondoa hawa nyani, maana tunateseka sana, umri wangu sasa hivi umeenda, miaka 68 siwezi kuhangaika huku na huku tena kwenda kutafuta chakula," amesema.

Ameiomba Serikali kuwaangalia kwa jicho la pekee kwa kuwa maisha yao wanayaendesha kwa kulima na kufuga na kilimo ndicho kinawapatia kipato cha kuendeshea familia.

"Isipochukua hatua, tutafia ndani kwa sababu ya njaa, tunataka tuendelee kulima bila hofu na tuvune mazao ya kutosha, lakini hivi sasa hatuwezi kufanya kitu chochote, makundi ya nyani ndiyo yanazidi kuja karibu kila siku,” amesema mama huyo.

Naye Antony Paul, mkazi wa kijiji hicho, pia ameiomba Serikali kuwapatia ufumbuzi wa nyani hao.

"Adha tunazopata  kuhusu hawa nyani ni kubwa mno, wanatusumbua sana, wanakula mifugo ya watu, kuku, mbuzi wanaliwa na hata watu wameshindwa kulima kutokana na hawa nyani,"

“Tunaomba tupatiwe ufumbuzi wa hawa nyani waondoke katika maeneo yetu maana hawakuwepo, wamekuja wakatukuta sisi tukiwa katika maeneo haya, sasa hivi wamezaliana ni wengi mno, tunaomba Serikali itusaidie kuondoa hawa wanyama ili tuendelee na maisha yetu ya kawaida," amesema.

Ameongeza kuwa; "mifugo yangu kama kuku imeliwa, mazao yangu shambani nayo yameliwa, kwa hiyo hatuwezi kulima tena maana nyani wametawala katika maeneo haya, tumetoa taarifa kwa  ofisi za serikali lakini msaada ni mdogo sana,” amesema Paul.

Samwel Msacky, ambaye pia ni mkazi wa kitongoji hicho, amesema nyani hao pia hupanda juu ya bati kucheza na wakati mwingine hunyonyeshea watoto wao juu ya bati.

"Juzi nikiwa na mama hapa nyumbani nilisikia kitu kinagusa eneo la jikoni, nilipoenda kuangalia ni nini, nikakuta nyani ndio wameingia jikoni wanakula chakula ambacho tulikuwa tumekiacha jikoni na hata niliipofika wala hawakushtuka, waliendelea kula tu bila hata hofu yoyote, yaani wamekuwa kama watu," amesema mchungaji huyo wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), usharika wa Ashira Marangu.

Amesema wananapishana nao barabarani kama binadamu na wala hawana woga kuwa hawa ni binadamu, tunaomba Serikali iangalie namna ya kuwahamisha.

Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Zephania Sumaye ameziagiza mamlaka zinazohusika na wanyama hao kwenda kwenye maeneo hayo kuangalia namna ya kuwarejesha nyani hao kwenye maeneo yao ya asili, ili kuondoa usumbufu kwa wananchi.

“Mamlaka ya Wanyama Pori Tanzania (Tawa), waende kwenye maeneo ambayo uharibifu umefanyika na waangalie namna ya kuwarejesha wanyama hao kwenye maeneo yao ya asili na watoe elimu kwa wananchi waweze kujua ni namna gani ya kukabiliana nao wasiendelee kulete uharibifu zaidi,” amesema Sumaye.

Mwananchi ilimtafuta Kamanda wa mfumo wa  Ikolojia kutoka Tawa Mkoa wa Kilimanjaro, Lackson Mwamwezi amesema wamepokea maagizo ya mkuu huyo wa wilaya na watayafanyia kazi mara moja.

"Kwa kuwa mheshimiwa mkuu wa wilaya ametoa maagizo ya kufanya, tutampa ushirikiano na tutawadhibiti hawa wanyama, kwa mfano kule Wilaya ya Rombo kila mwezi tunapeleka vikosi kuwadhibiti, lakini hawa pia tutaenda kupambana nao," amesema Mwawezi.

Hili si tukio la kwanza la nyani kuvamia makazi ya watu mkoani Kilimanjaro, mwaka jana Mwananchi iliripoti malalamiko ya wanaume wanaoishi pembezoni mwa Mto Mlembea, Wilaya ya Rombo, kuwa wake zao walikuwa wanavamiwa na nyani wa kiume na wakati mwingine kuhatarisha usalama wao.

Walisema nyani hao wamekuwa ni tishio kwa wake zao na watoto na kwamba wakati mwingine huwavamia wakiwa mashambani, kuiba watoto wadogo