Nyumba zazingirwa maji Karatu, wananchi wakosa makazi

Muktasari:

  • Kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali wilayani humo, zimesababisha athari kubwa kwa wananchi baada ya maji kuzingira na kujaa katika makazi yao,hali iliyowalazimu wengine  kwenda kupanga,kuhamia kwa ndugu

Karatu.Mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini zimeleta athari katika wilaya ya Karatu mkoani Arusha, baada ya baadhi ya nyumba kufunikwa na kuzingirwa na maji, hivyo baadhi ya wananchi kukosa makazi.

Kutokana na changamoto hiyo, wengine wamelazimika kwenda kutafuta nyumba za kupanga, wengine wakienda shule na baadhi kuhamia kwa ndugu na jamaa zao.

Akipotafutwa na Mwananchi Digital kuzungumzia athari za mvua hizo, Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Dadi Kolimba amesema yuko msibani na kwamba atatoa taarifa baadaye.

Mvua hizo zilizonyesha tangu wiki iliyopita zinatajwa kuathiri maeneo mbalimbali wilayani humo, ikiwemo Kata ya Qurus na  Karatu.

Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne Aprili 16, 2024, baadhi ya wananchi wameiomba Serikali kuangalia namna ya kuwasaidia kwa haraka kabla madhara hayajawa makubwa.

Jeneth Mfanya, mkazi wa Mtaa wa Bwawani amesema amelazimika kwenda kuupanga kutokana na nyumba yake kujaa maji.

Amesema mvua hiyo iliyoanza kunyesha tangu wiki iliyopita imeleta athari kubwa kwao, kwani mbali na nyumba yake kujaa maji, pia saluni aliyokuwa anaitegemea kama kitega uchumi nayo imejaa maji na amefanikiwa kuokoa vifaa vichache.

Amesema mvua hiyo iliyoanza kunyesha tangu wiki iliyopita, imeleta athari kubwa kwao.

Mfanya amesema maji hayo yamejaa hata kwenye saluni yake ambayo ndiyo kitega uchumi chake na vifaa vyake vyote vimeharibika.

“Tumepata hasara kubwa, maji yamejaa nyumbani kwangu nilikuwa naishi na watoto wangu wawili, mume wangu amesafiri. Ninavyoongea na wewe hata gari nimeshindwa kulitoa limezingirwa na maji,”amesema.

Ameiomba Serikali iwasaidie wapate hata mahitaji ya msingi, licha ya baadhi ya wasamaria wema kuanza kujitokeza kuwasaidia, lakini bado hali si nzuri.

Naye Hans Minja, mkazi wa Karatu amesema alikuwa akiishi katika chumba kimoja pamoja na mkewe na watoto wao wadogo watatu, hivyo  wamelazimika kuhama tangu jumapili Aprili 14, mwaka huu.

“Na hivi tunavyoongea hapa bado maji yanazidi kuongezeka,” amesema Minja.

Amesema tangu aanze kuishi eneo hilo hajawahi kushuhudia mafuriko ya aina hiyo. “Nakumbuka Jumapili maji yalijaa ndani kiasi cha kunifika shingoni, nilichoweza kuokoa ndani kabla maji hayajaongezeka ni godoro na vyombo vichache ila vitu vingine vyote vilibaki.”

Amesema karibu eneo lote limezingirwa na maji hali ni mbaya; “Tunahangaika mtaani nilikuwa fundi ujenzi kwa sasa hata kazi siwezi kufanya kutokana na hali iliyopo, hapa sina hata mawasiliano na ndugu zangu, simu yangu ilipotelea kwenye maji wakati najaribu kuokoa vitu vyangu.”

Mkazi mwingine, Joseph Alphonce, anasema baadhi ya maeneo yakiwemo ya Uwanja wa Mbowe, yameathiriwa huku watu wakikosa makazi ya kuishi ambapo wengine walitakiwa na uongozi wa wilaya wahamie kwenye vyumba vya madarasa  vilivyotengwa katika baadhi ya shule wilayani humo.

“Tunaomba haya maji ni mengi na baadhi ya nyumba zimefunikwa yamebaki mapaa tu yanaonekana kwa juu, wanafunzi wanashindwa kwenda shule, kiujumla hali ni ngumu,” amesema mkazi huyo.

Naye Damian Patrick anasema nyumba yake ilikuwa haijajaa maji, ila leo yanaingia kwa kasi  na amefanikiwa kuhamisha vitu karibu vyote.

Kauli ya Diwani Karatu

Diwani wa Karatu, Joseph Lolo alipoulizwa amekiri kuwa hali ni tete, lakini hawezi kuzungumzia hilo kwa kina kwa kuwa mkuu wa wilaya atatoa taarifa.

“Hali si shwari, lakini mtoa taarifa ni DC mwenyewe, bado tunasubiri kauli yake, kuna kaya nyingi zimedondoka na nyingine kuzingirwa na maji,” amesema diwani huyo.

Maeneo mengi mkoani Arusha tangu wiki iliyopita yanapata changamoto ya mafuriko. Miongoni mwa maeneo hayo ni pamoja na lile la Kisongo.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Emmanuela Kaganda wiki iliyopita, Mkuu wa Wilaya ya Longido, Marco Ng'umbi alisema madhara waliyopata baadhi ya wananchi wa eneo hilo yalikuwa makubwa.

Alisema mali zao ziliharibika yakiwamo mazao, maeneo wanayofanyia biashara yalijaa maji na matope yaliingia kwenye nyumba na kusababisha familia nyingi kukosa makazi.

Alisema katika tathimini ya awali waliyofanya ilionyesha kaya 157 ziliathirika, lakini nyumba moja iliyokuwa inaishi familia yenye watu zaidi ya 10, iliharibika kiasi cha kutofaa tena kukaliwa na watu.

Mbali na wilaya hizo mbili, Wilaya ya Arusha, ilipata athari baada ya gari la Shule ya Msingi ya Ghati Memorial lililokuwa na wanafunzi kusombwa na maji katika Kata ya Sinoni na kusababisha vifo vya wanafunzi wanane na msamaria mmoja aliyekuwa akijaribu kuwaokoa wanafunzi hao.