Pura yawasilisha rasimu ya mwongozo wa CSR

Lindi. Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (Pura) imesema kuwa miradi itakayotekelezwa kupitia uwajibaki kwa jamii (Corporate Social Responsibility – CSR), itakuwa ni ile yenye kuakisi mahitaji ya yatokanayo na vipaumbele vya jamii husika.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Pura, Charles Sangweni, katika kikao cha uwasilishaji wa rasimu ya mwongozo wa CSR wa kampuni zitakayotekeleza miradi hiyo kwa jamii, katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi Julai 19, 2023.

“Huu mwongozo utasaidia, pamoja na mambo mengine, kuhakikisha kuwa miradi ya CSR inayotekelezwa na kampuni zinazofanya shughuli za utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini ina akisi mahitaji ya jamii hizo kulingana na vipaumbele vya jamii husika,” amesema bosi huyo wa Pura na kuongeza;

"Miongoni mwa sehemu kuu za mwongozo huu ni maandalizi ya mpango wa CSR utakaoshirikisha wananchi kupitia uongozi wa Serikali za mitaa. Ushirikishwaji huu utawezesha vipaumbele vya jamii lengwa kuzingatiwa hivyo kuongeza tija katika miradi hiyo."

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Kilwa, Wakili Mary amesema kuwa, Pura imefanya jambo jema kuanzisha mchakato wa kuwa na mwongozo huo kwa kuwa utasaida mawazo ya walengwa kuzingatiwa kabla ya kuanza utekelezaji wa mradi.

"Tunaishukuru sana Pura kwa kulibeba jambo hili na kujitoa kuandaa rasimu ya mwongozo huu. Ofisi ya Mkurugenzi imeupokea kwa mikono miwili na itauboresha kwa namna itakavyoona inafaa kisha kuwashirikisha wadau wengine kabla ya kuuidhinisha na kuanza kutumika. Ni matumaini yetu kuwa ifikapo Septemba 2023 mwongozo huu utakuwa Tayari," amesema Mary.

Kwa mujibu wa Pura, mwongozo huu umeandaliwa kwa kuzingatia Kifungu namba 222(4) cha Sheria ya Petroli ya Mwaka 2015.