Putin kuapishwa mchana huu akifukuzia miaka 30 madarakani

Muktasari:

  • Wakati Vladimir Putin akiapishwa mchana huu kuendelea kushikilia madaraka nchini Russia, Marekani na baadhi ya mataifa ya Umoja wa Ulaya yamesusia sherehe hizo.

Moscow. Rais wa Russia, Vladimir Putin anaapishwa mchana wa leo Jumanne Mei 7, 2024 kuliongoza tena taifa hilo kwa kipindi kingine cha miaka sita, kitakachokamilisha atafikisha 30 akiwa madarakani.

Putin ambaye ameliongoza taifa hilo kwa miaka 24, alichaguliwa tena Machi 2024 kushika wadhifa huo kwa miaka sita ijayo.

Ataapishwa kushika wadhifa huo katika hafla ya kifahari itakayofanyika huko Kremlin.

Katika uchaguzi huo Putin ameshinda kwa asilimia 87.27 ya kura zote baada ya kufanyika mabadiliko ya katiba yanayoruhusu aweze kugombea urais hadi mwaka 2036.

Kiongozi huyo anarejea katika kiti hicho wakati ambao vita kati ya Russia na Ukraine vilivyoanza Februari 24, 2022, vikifisha miaka miwili.

Duru zinasema ushindi wake wa Machi unamaanisha ana uwezekano wa kuwa kiongozi aliyekaa muda mrefu zaidi nchini humo katika karne moja, akimshinda Joseph Stalin.

Putin mwenye umri wa miaka 71 ataapishwa huku televisheni za nchi hiyo zikirusha moja kwa moja kuanzia mchana huu, wakati msafara wa magari ya kifahari utakapompeleka hadi kwenye Jumba la Grand Kremlin la Moscow.

AFP imesema akishawasili, atapita kwenye korido za Ikulu hadi Ukumbi wa Saint Andrew, ambapo ataapishwa kisha atatoa hotuba fupi.

Lakini, inaelezwa maofisa wa Serikali na wanadiplomasia wa kigeni wamealikwa kwenye sherehe hizo akiwemo balozi wa Ufaransa Pierre Levy anayetarajiwa kuhudhuria.

Aidha, mataifa ya Uingereza na Canada yamesema hayatatuma mtu yeyote, huku msemaji wa Umoja wa Ulaya akiliambia Shirika la Habari la Reuters kuwa balozi wa umoja huo Russia hatahudhuria sherehe kwa kuzingatia msimamo wa nchi nyingi wanachama wa Umoja wa Ulaya.

"Hatutakuwa na mwakilishi wakati wa kuapishwa kwake, kwa hakika hatukuzingatia uchaguzi huo kuwa huru na wa haki lakini yeye ni Rais na ataendelea na wadhifa huo," msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Matthew Miller amenukuliwa na Al Jazeera

Nchi nyingine za Ulaya zikiwemo Poland, Ujerumani na Jamhuri ya Czech zimeonyesha ishara kwamba hazitatuma.