Rais Samia kushiriki ibada ya kumuingiza kazini Askofu Malasusa

Muktasari:

  • Dk Malasusa alichaguliwa kushika wadhifa wa Mkuu wa Kanisa Agosti mwaka jana katika mkutano mkuu wa KKKT uliofanyika jijini Arusha.


Dar es Salaam. Rais Samia Hassan Suluhu anatarajiwa  kuushiriki Ibada maalumu ya kumuingiza kazini Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),  Dk Alex Malasusa.

Dk Malasusa alichaguliwa kushika wadhifa huo Agosti mwaka jana katika mkutano mkuu wa KKKT uliofanyika jijini Arusha na kufanya kuwa mkuu wa sita wa kanisa hilo tangu kuundwa kwake Juni, 1963.

Akizungumza leo Ijumaa Januari 19, 2024, Katibu Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP), Goodluck Nkini amesema Ibada hiyo itafanyika  Jumapili ya Januari 21, 2024 katika Kanisa la Azania Front, Dayosisi ya Mashariki na Pwani.

"Jumapili hii tutapata neema ya kupokea ugeni mkubwa wa Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na wageni wengine wa ndani na nje ya nchi hii, wanaofikia takriban 1,500.

"Ibada hiyo itaongozwa na Mkuu wa KKKT anayemaliza muda wake, Baba Askofu Dk Fredrick Shoo,  akishirikiana na maaskofu wengine kutoka dayosisi zote 28 za kanisa hili," amesema  katibu huyo.

Kabla ya ibada hiyo, kesho Jumamosi Januari 202024, kutakuwa na ibada ya chakula cha Bwana itakayofanyika katika Usharika wa Mbezi Beach wa kanisa hilo.

Pamoja na mambo mengine, amesema ibada hiyo itatumika kuwasilisha salamu za pongezi kutoka kwa makundi mbalimbali na wageni wa nje ya nchi ambao hawatapata nafasi ya kufanya hivyo katika ibada ya Jumapili.

"Kwa mantiki hiyo tunawakaribisha waumini na wananchi kushiriki matukio haya mawili ya kiimani huku tukiwahamasisha wote kuendelea kuyaombea, ili yawe ya baraka kwa lengo kuu moja la kumuingiza kazini Askofu Malasusa," amesema Nkini.