Rais Samia: Tutazifanyia kazi ripoti za CAG, Takukuru

Muktasari:

  • Rais Samia Sukuhu Hassan amezipongeza ofisi za CAG na Taasisi ya Kupambana na Kudhibiti Rushwa (Takukuru) kwa kuibua dosari za Serikali, akiahidi kuzifanyia kazi ili zisijirudie.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inakwenda kuzifanyia kazi dosari zilizobainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kupambana na Kudhibiti Rushwa (Takukuru) ili zisijirudie mwaka ujao.

Ameyasema hayo leo Machi 28, 2024 alipokuwa akipokea ripoti za CAG na Takukuru, Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma akisema ripoti hizo zinaleta uwazi na uwajibikaji katika uendeshaji wa Serikali.

“Ripoti hizi zinachangia maboresho ndani ya Serikali na mashirika ya umma. Dosari hizi tutakwenda kukaa tuzifanyie kazi kisawasawa, turekebishe na mwakani pengine hizi hazitajirudia, tutakuwa tumesogea,” amesema.

Mbali na dosari, Rais Samia ameeleza kufurahishwa na ongezeko la hati safi hadi asilimia 99 na hati chafu asilimia moja tu.

“Ripoti hizi zinatusaidia kuongeza mapato, kutokana na vipengele anavyoonyesha CAG na Takukuru, wakienda huko wanasaidia kuziba mianya ya fedha zinazopotea, rushwa na mengineyo na mapato yanarudi serikalini,” amesema.

Ameipongeza Takukuru kwa kuibua kero kwa kushirikiana na wananchi kwa kusikiliza kero zao na kuzipeleka kwenye taasisi husika na hivyo kuisaidia Serikali kushughulikia kero na kuwajibika ipasavyo.

Pia, ameipongeza ofisi ya CAG kwa kuibua mambo kadhaa kupendekeza utekelezaji kwa muda mwafaka.