RC Shigella ataka halmashauri kusimamia miradi ya CSR

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini Mpango wa utekelezaji miradi inayotolewa kwa fedha za CSR zinazotolewa na kampuni ya uchimbaji Madini ya Buckreef.

Muktasari:

Kampuni ya Uchimbaji madini ya dhahabu Buckreef iliyopo Wilaya ya Geita imelenga kutumia Sh420 milioni ambazo ni fedha za uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR), kukamilisha miradi ya maendeleo katika sekta ya Maji, Elimu na Mazingira katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa mwaka 2023.

Geita. Mkuu wa mkoa wa Geita, Martine Shigella amezitaka halmashauri za mkoa huo zinazopokea fedha za uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR) kuhakikisha miradi inayotekelezwa inaleta matokeo chanya kwa wananchi na kuinua uchumi wa mkoani humo.

Akizungumza wakati wa utiaji saini Mpango wa utekelezaji miradi inayotekelezwa na fedha za CSR kwa mwaka 2023 zinazotolewa na kampuni ya Uchimbaji madini ya Buckreef, Shigella pia ametaka miradi inayotekelezwa ikamilike kwa wakati.

Amesema utekelezaji wa mpango huo umechelewa kuanza na mwaka wa fedha wa Buckreef humalizika Septemba akidai ni wajibu wa pande zote mbili kuhakikisha wanafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha miradi iliyolengwa ikiwemo ukamilishaji wa kituo cha afya ,ujenzi wa matundu ya vyoo na vyumba vya madarasa inakamilishwa ifikapo Oktoba mwaka huu.

Awali Meneja Mkuu wa mgodi Buckreef,  Gaston Mujwahuzi amesema 2023 Kampuni hiyo imelenga kutumia Sh420 milioni kama sehemu ya uwajibikaji wao kwa jamii inayowazunguka.

Mujwahuzi amesema fedha walizozitoa zitatekeleza miradi katika sekta ya Elimu, Afya na Mazingira akisema kutokana na mazingira mazuri ya uwekezaji waliyoyapata yamewezesha kampuni hiyo kuongeza uzalishaji kutoka wakia tani 15 hadi tani 45 za wakia kwa saa.

“Tupo kwenye maandalizi ya kuweza kufikia uzalishaji wa tani 90 hadi 100 za wakia kwa saa na mpango huu tunataraji kuanza kuutekeleza mwanzoni mwa mwaka ujao hii itakua fursa kwetu lakini ni fursa pia kwa Watanzania kwakuwa kuongezeka uzalishaji itaongeza pia ajira”amesema

Katibu Tawala Mkoa wa Geita, Profesa Godius Kahyarara amesema kutokana na mkoa huo kuwa na umuhimu mkubwa kwenye uchumi wa nchi lazima kuwe na uwajibikaji utakaouwezesha kuendelea kuzalisha kwa wingi.

Kahyarara amesema nusu ya mapato ya fedha za kigeni yanatokana na sekta ya madini ambapo katika mkoa huo kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita uzalishaji wa dhahabu ulikuwa kilo 45.

Amewataka Wakurugenzi wa halmashauri zote za mkoa huo kuhakikisha wanaongeza usimamizi kwa kusimamia miradi ili iwe na ubora unaolingana na thamani ya fedha.