Ripoti: Ukatili dhidi ya wanaume waongezeka

Muktasari:

Kasi ya vitendo vya ukatili dhidi ya wanaume inaongezeka, licha ya juhudi zinazofanywa kukabili vitendo hivyo.

Dar es Salaam. Katika kipindi ambacho dunia inapambana kukabiliana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, matukio hayo yanachipukia na kuota mizizi dhidi ya wanaume.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Haki za Binadamu ya mwaka 2023, vitendo vya ukatili kwa wanaume vimeongezeka na kufikia asilimia 10, kutoka asilimia sita ya mwaka 2022.

Ripoti hiyo iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), ikihusisha mikoa 20 ya Tanzania Bara na mikoa yote ya Zanzibar, imetaja mikoa saba Dar es Salaam, Njombe, Geita, Arusha, Kilimanjaro, Mara, Kigoma na Dodoma kuwa inaongoza kwa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu kwa mwaka 2023.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga (wa tatu kulia), akizungumza katika uzinduzi wa Ripoti ya Haki za Binadamu ya mwaka 2023 jijini Dar es Salaam leo

Hayo yameelezwa jijini Dar es Salaam leo, Aprili 24, 2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga alipotoa maelezo kwa ufupi kuhusu ripoti hiyo ambayo ni ya 22 kuandaliwa na kituo hicho.

Henga amesema ripoti kama hiyo ya mwaka 2022 ilionyesha vitendo vya ukatili dhidi ya wanaume ni asilimia sita, lakini mwaka 2023 vimeongezeka hadi asilimia 10.

"Hii inaashiria hali si nzuri kwa wanaume nao, maana ukatili dhidi yao umeongezeka ingawa haujafikia wanaofanyiwa watoto na wanawake," ameeleza.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, robo tatu ya vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu ni kwa watoto, asilimia 30 wanawake, 12 wazee na wenye ulemavu ni asilimia tatu.

Ripoti inaeleza tathmini ya LHRC ya mwaka 2023 inaonyesha hali ya haki za binadamu ilidorora mwaka huo ukilinganisha na mwaka 2022.

Henga amesema ripoti hiyo kwa mwaka 2023 imebaini ukiukwaji wa haki za waandishi wa habari, ukiukwaji wa haki za kesi na mwenendo wa kesi na usafirishaji haramu wa binadamu na watoto.

Mengine yaliyobainika katika ripoti ni ndoa za utotoni, utelekezaji wa watoto, faragha, ulinzi binafsi, ukeketaji na ukiukwaji wa haki ya kumiliki mali na kurithi.

Katika hatua nyingine, ripoti haijabaini tukio lolote la mauaji ya watu wenye ualbino katika mwaka 2023.

Henga amesema mara nyingi matukio hayo hutokea katika kipindi kinachokaribia uchaguzi, akisisitiza elimu inapaswa kutolewa zaidi kwa kipindi hiki.

Mtafiti Mwandamizi wa LHRC aliyesimamia utafiti huo, Fundikira Wazambi amesema matukio yaliyobainishwa yana athari kwa watu binafsi na uchumi wa Taifa.

Amesema kuendelea kutokea kwa matukio hayo, kunasababishwa na kukosekana uwajibikaji katika ngazi zote.

"Wapo wanaoshuhudia matukio lakini hawataki au wanaogopa kuripoti katika mamlaka zinazohusika, mimi nimewahi kushuhudia kiongozi anaogopa kuripoti," amesema.

Rushwa nayo ni sababu nyingine ya kuendelea kwa vitendo hivyo, kwa mujibu wa Fundikira.

Amesema wapo wanaofanya matukio hayo kisha wakawahonga wazazi wa mwathirika ili akafute kesi mahakamani.