Rukwa yapata Sh6.5 bilioni za dharura kurejesha miundombinu ya barabara

Makandarasi wakiendelea na kazi ya kujenga moja ya madaraja

Muktasari:

  • Mkoa wa Rukwa wapokea Sh6.5 bilioni kutoka Serikalini kwa ajili ya kufanya matengenezo ya dharura kwa miundombinu ya barabara na madaraja yaliyoharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha

Dar es Salaam. Serikali imetoa Sh6.5 bilioni kwa Mkoa wa Rukwa kwa ajili ya kufanya matengenezo ya dharura ya kurejesha miundombinu ya barabara iliyoharibika kutokana na mvua za El Nino zilizonyesha mkoani hapo.

Fedha hizo zimepitia Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), taasisi yenye jukumu la kuhakikisha mawasiliano yanapatikana na kuwarahisishia mawasiliano wananchi.

Akizungumza jana Jumatatu, Mei 6, 2024 Meneja  wa Tanroads, Mkoa wa Rukwa Mgeni Mwanga aliipongeza Serikali kwa kukubali kutoa kiasi hicho cha fedha ambacho kimewezesha kurejesha miundombinu iliyoharibiwa.

Mwanga amesema hayo baada ya kutembelea na kukagua miundombinu iliyoharibika likiwemo Daraja la Solola katika Barabara ya Ilemba – Kaoze ambalo barabara unganishi ilisombwa na maji na kusababisha upana na kina cha mto kuongezeka.

“Tangu tumepata athari ya mvua hizi tumekuwa tukifanya matengenezo endelevu ya kuhakikisha kwamba kila kunapotokea athari barabara inafunguka na magari yanapita, tumeendelea kufanya hivyo na mpaka sasa Serikali imeshatuletea Sh6.5 bilioni kwa ajili ya kufanya marekebisho na kufungua njia pale inapojifunga,’’ amesema Mwanga

Mwanga amesema kuanzia wiki ya tatu ya Aprili 2024, mvua ilianza kupungua na walianaza kufanya maboresho ya muda wa kati kwa kurudishia madaraja yaliyobomoka wakianza na barabara unganishi ambazo madaraja hayakusombwa na maji.

Amesema maeneo yaliyoathirika zaidi na mvua hizo zilizonyesha kuanzia Desemba 2023 hadi Aprili 2024, ni barabara ya kutoka Kasansa – Muze hadi Kilimatundu ambako madaraja 18 yalipata athari, kati ya hayo sita ndio yaliyoharibika zaidi.

Msimamizi wa Kitendo cha Matengenezo Tanroads mkoani hapo, Galasiano Tovagonze alisema kutokana na athari hizo, wamepata makandarasi saba ambao wanafanya kazi ya matengenezo ya muda wa kati.

Amesema makandarasi wawili wapo katika barabara ya Kasansa – Muze, mmoja yupo kipande cha Muze – Mtowisa na wanne kipande cha Mtowisa –Ilemba; wote wanafanya kazi ya kurejesha miundombinu iliyoharibika.

Mwanga ametoa wito kwa watumiaji wa barabara hasa wakati huu wa mvua kuwa na subira na umakini pale wanapoona maji yamepita juu ya barabara au daraja, ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.