Sababu ATCL kutopeleka ndege Pemba

Muktasari:

  • Kwa kutumia ndege ndogo safari za Pemba zinatarajiwa kuanza Mei, 2024.

Dodoma. Idadi ndogo ya abiria imetajwa kuwa sababu ya Serikali kutopeleka ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) Pemba, Zanzibar ili kuepuka hasara.

Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile amesema hayo alipojibu swali la nyongeza la mbunge wa Shaurimoyo, Ali Juma Mohamed.

Mbunge huyo amesema Februari, 2024 ATCL ilitangaza kuanzia Machi ingeanza safari za kwenda Pemba, walianza matayarisho ya kuuza tiketi lakini hadi leo Aprili 17, 2024 safari hizo hazijaanza.

“Nataka kufahamu ni kipi kimezuia hadi leo safari hizo hazijaanza,” amehoji.

Kihenzile amesema ndege waliyokuwa wameiandaa ni kubwa na mwitikio wa abiria ulikuwa mdogo, hivyo endapo ndege ingeanza safari ingekuwa ni hasara kwa shirika.

“Hivyo ndege nyingine ndogo itakapoingia, baada ya Mei tutaanza kupeleka abiria (Pemba),” amesema.

Katika swali la msingi, Mohamed amehoji ni sababu gani zinafanya ATCL lisitumie fursa ya kubeba watalii wanaotoka nchi mbalimbali duniani kuja nchini.

Naibu Waziri Kihenzile amesema ATCL inatumia fursa iliyopo ya kusafirisha abiria, wakiwemo watalii kwa kuanzisha vituo vilivyo karibu na vya utalii nchini.

Amevitaja vituo hivyo kuwa vya Kilimanjaro na Arusha kwa watalii wanaotembelea Hifadhi za Ngorongoro, Ziwa Manyara, Tarangire na Mlima Kilimanjaro.

Vingine ni cha Mwanza ambako kuna Hifadhi ya Serengeti; Zanzibar kuna fukwe za bahari, Hifadhi ya Ghuba ya Johazi, msitu wa Pogwe na maeneo ya kihistoria.

Kituo kingine ni cha Kigoma ambako kuna Hifadhi ya Gombe; Kituo cha Mpanda ambako kuna Hifadhi ya Katavi; na Kituo cha Iringa kwenye Hifadhi za Mikumi, Ruaha na Kitulo.

Kihenzile amesema ATCL imeingia mikataba ya ushirikiano wa kibiashara na mashirika makubwa ya ndege kama vile Qatar, Emirates, KLM, Air India, Ethiopia na Oman Air ambayo huleta watalii Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) na KIA.

Amesema ndege za ATCL huwasafirisha watalii hao kwenda katika maeneo ambayo mashirika hayo hayafiki.