Sababu kimbunga Hidaya kukosa nguvu ghafla

Muktasari:

Inaelezwa kimbunga kadri kinavyotembea kuelekea ukanda wa Ikweta, kinapunguza nguvu kwa kuwa ili kitembee huwa kinazunguka na uwezo huo hupungua.

Dar/Mikoani. Shughuli za usafiri, usafirishaji na uvuvi zikiwa zimerejea katika baadhi ya maeneo huku athari zaidi za kimbunga Hidaya zikitajwa, wataalamu wa masuala ya hali ya hewa wameeleza siri ya kimbunga hicho kukosa nguvu ghafla.

Kimbunga Hidaya kilichoanza kutolewa taarifa za tahadhari Mei 1 kikiwa na kasi ya kilomita 65 kwa saa, safari yake ilianza Aprili 28 kikiwa na upepo wenye kasi ya kilomita 30 kwa saa, kwa mujibu wa mtandao wa GoogleMap.

Kasi yake iliendelea kuongezeka kila siku hadi kufikia kilomita  150 kwa saa kilipofika karibu na pwani ya Tanzania, kabla ya kupungua ghafla hadi kilomita 90 na hadi jana saa 12 jioni kilikuwa na kasi ya kilomita 55 kwa saa.

Kutokana na mwenendo huo, Wataalamu waliozungumza na Mwananchi wameeleza sababu za kimbunga na vinginevyo kupungua nguvu, wakitaja mazingira ya kijiografia na hali ya hewa, kuwa ndiyo yanaweza kusababisha vipoteze nguvu yake.

Taarifa ya mwisho iliyotolewa na mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) saa 5.59 usiku wa kuamkia jana ilisema kimbunga Hidaya kilipoteza nguvu kabisa baada ya kuingia nchi kavu kwenye Kisiwa cha Mafia.

TMA kupitia mwendelezo wa taarifa zake kuhusu kimbunga Hidaya ilisema:

"Taarifa hii inahitimisha mfululizo wa taarifa za kilichokuwa kimbunga Hidaya, zilizokuwa zikitolewa na TMA tangu Mei 1, 2024, mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa unaonyesha kuwa katika kipindi cha saa sita zilizopita, kimbunga Hidaya kimepoteza kabisa nguvu baada ya kuingia nchi kavu katika Kisiwa cha Mafia."

Taarifa ya TMA ilisema mabaki ya mawingu yaliyokuwa yameambatana na kimbunga hicho, yalisambaa katika maeneo mbalimbali ukanda wa kusini hususani katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Morogoro, hivyo hakuna tena tishio la kimbunga Hidaya.

TMA ilianza kutoa tahadhari ya kimbunga hicho tangu Mei mosi 2024 kilikuwa na mwendokasi wa kilomita 130 kwa saa.

Hii ni mara ya pili ndani ya miaka minne vimbunga kupungua nguvu vikiwa vinakaribia kuingia nchini.

Aprili 25, 2021 kimbunga Jobo kilipoingia Pwani ya Bahari ya Hindi kilipungua nguvu na kutoweka.

Kimbunga ni aina ya dhoruba yenye nguvu kubwa ambayo inaambatana na upepo mkali, mvua kubwa na mawimbi makubwa baharini.

Hutokea katika maeneo ya tropiki na huchukua umbo la mzunguko wenye shinikizo la chini katikati yake.

Sababu kuisha nguvu

Meneja wa Utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk Mafuru Kantamla amesema kuna sababu saba za kitaalamu za kimbunga kupunguza kasi kadri kinapokuwa kinasogelea sehemu ya nchi kavu.

Amesema kimbunga kikienda karibu na ardhi kiwango cha maji yanayotengeneza mvuke hupungua, hivyo chenyewe hurudi kwenye nguvu yake kwa kuwa hakipati msaada kutoka kwenye maji.

Sababu nyingine amesema kadri kinavyotembea kuelekea ukanda wa Ikweta, kinapunguza nguvu kwa kuwa ili kitembee huwa kinazunguka na uwezo huo hupungua.

"Kikisogea kwenye Ikweta, nguvu inayokifanya kizunguke hupungua," amesema Kantamla.

Amesema sababu nyingine ni kuwapo upepo kinzani, hivyo kinapokuwa kinaelekea sehemu fulani, lakini pakawepo na upepo kinzani kinapungua nguvu.

"Kuna vitu kama saba zinasababisha, lakini vya msingi ni hivyo nilivyovitaja, pia kimbunga kinaposogea kuelekea karibu na ardhi nguvu yake hupungua.

Japo alizitaja hizo, mitandao mbalimbali pia inaeleza sababu nyingi zinazoweza kusababisha nguvu ya kimbunga kupungua, baadhi ya hizo ni saba zinazoshabihiana na za Dk Kantamla.

Kuingiliana na ardhi au milima: Wakati kimbunga kinapopita juu ya ardhi au milima kinaweza kupunguza nguvu yake kwa sababu kinakosa joto na unyevu unaohitajika wa kuendelea kuwa na nguvu.

Kuingiliana na baridi au maji baridi: Wakati kimbunga kinapopita juu ya maji baridi au eneo baridi, kinaweza kupoteza joto na unyevu wake, ambao ni muhimu kwa nguvu yake ya kuzunguka.

Kuingiliana na upepo wa juu: Upepo wa juu unaweza kusababisha kimbunga kupungua kwa kuchukua sehemu ya nishati yake.

Kutengana kwa viwango tofauti vya hewa: Wakati kimbunga kinakutana na viwango tofauti vya hewa, kinaweza kupunguza nguvu yake au kufifia kabisa.

Kutembea kwa muda mrefu: Baada ya kusafiri kwa umbali mrefu, kimbunga kinaweza kupoteza nguvu polepole kwa sababu ya kutoa nishati yake kwa muda mrefu.

Kutegemea upungufu wa maji ya bahari: Wakati kimbunga kinapopita juu ya eneo lenye upungufu wa maji ya bahari, kinaweza kupoteza nguvu kwa kukosa unyevu muhimu.

Mabadiliko ya mwelekeo au kasi: Mabadiliko katika mwelekeo au kasi ya kimbunga yanaweza kusababisha kupungua kwa nguvu yake kwa sababu ya mabadiliko ya mazingira yake ya karibu.

Akizungumzia vimbunga na kasi yake, Mhadhiri Mwandamizi wa Idara ya Jiografia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Donald Mwiturubani amesema kimbunga kinasababishwa na mgandamizo mdogo wa hewa katika eneo fulani, hasa katika bahari joto.

“Bahari yenye mkondo wa joto ikijengeka, madhara ya kimbunga yanategemeana na ukubwa wa mgandamizo utakaokuwepo,” alisema.

“Mgandamizo unaendelea kuwepo ni kama vile unavyojaza upepo kwenye tairi. Kwa kawaida upepo huvuma kutoka katika mgandamizo mkubwa kwenda mdogo, sasa mgandamizo mdogo unapojijenga unasababisha kitu kama tufe linaposuka na kuleta upepo unaosambaa kwa kilomita 67 hadi 119 kwa saa kwa vimbunga vya kawaida.”

Dk Mwiturubani amesema inapotokea kasi ya kimbunga imezidi kilomita hizo, maana yake mgandamizo ulikuwa mkubwa na mara nyingi inachukua siku tatu kwa mgandamizo kujengeka hadi tufe na kupasuka.

“Lakini katika kujengeka unaweza kukuta kuna mtawanyiko au eneo lenye mgandamizo mdogo, likawa dogo, kwa hiyo hata madhara hayawi makubwa. Kwa hiyo baada ya siku tatu mgandamizo unasambaa zaidi na upepo unaanza kupungua, hadi siku ya sita tunategemea kimbunga kimeisha kabisa kuanzia kilipoanza,” amesema.

Kuhusu sababu za tahadhari za kutangazwa likini mwisho wa siku havitokei, Dk Mwiturubani amesema:

“Kunakuwa na sababu nyingi, mfano eneo lililojengeka kimbunga naumbali kilipotopoka hadi nchi kavu.

“Ndiyo maana ukikuta kisiwa kimepigwa kinapigwa haswa, kwa sababu ni karibu na kilipotokea kimbunga. Kimbunga huwa kinasafiri kati kilomita 67 kwa saa hadi 119, lakini kuna vingine vinaenda kilomita 320 kwa saa, ambacho ni hatari zaidi,” amesema.

Hata hivyo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Ladislaus Chang’a amesema kimbunga chochote kikitua nchi kavu kinakwisha kwa kuwa hakiwezi kuhimili mazingira ya nchi kavu.

“Kimbunga kikigusa nchi kavu kinakufa, baharini kinakaa muda mrefu kwa sababu ya mifumo ya hali ya hewa na nguvu kinayopata kutoka katika unyevunyevu, kikigusa nchi kavu uhai wake unakuwa wa muda mfupi, labda kikate kona kurudi baharini,” amesema.

“Tunachoangalia, kitu kikubwa ni je, kimbunga kinaelekea kwetu? Kwa sababu kikigusa nchi kina madhara makubwa sana, nchi zote huwa zinaangalia kimbunga kitaenda kutua wapi?” amesema.

Hata hivyo, Dk Chang’a amesema kadri joto linavyoongezeka katika bahari na dunia, mifumo ya hali ya hewa inaimarika na uwezekano wa vimbunga kutokea moja kwa moja pwani ya Tanzania unaongezeka.

“Miaka yote uwezekano wa kimbunga kuja pwani yetu ilikuwa nadra, lakini kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa hasa ongezeko la joto, vinatokea,” amesema.

“Kwa historia vimbunga havikuwa vinatua pwani ya kwetu bali viliishia baharini au kwenda nchi za Madagascar na Msumbiji,” amesema Dk Chang'a.


Safari ya Hidaya

Kwa mujibu wa tovuti ya Zoom Earth, Kimbunga Hidaya kilianza Aprili 28 karibu na Visiwa vya Ushelisheli kikiwa na mwendokasi wa kilomita 30 kwa saa.

Aprili 29 kiliongezeka kasi na kufikia kilomita 35 kwa saa huku kikiwa bado na nguvu kadiri, kiliendelea kujikusanya zaidi hadi Aprili 30 saa 3.00 usiku kikafikia kasi ya kilomita 45 kwa saa.

Mei 1 kiliendelea kusogelea Pwani ya Bahari ya Hindi huku kasi ikiongezeka hadi kilomita 65 kwa saa na hapo ndipo Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ikatoa tahadhari ya uwapo wa Kimbunga Hidaya.

Kikiwa kinaendelea kuisogelea Pwani ya Bahari ya Hindi, Mei 2 kiliendelea kuimarika zaidi na kufikia kasi ya kilomita 120 kwa saa hadi saa 3.00 usiku.

Mei 3, 2024 hadi saa 3 asubuhi kasi yake iliongezeka zaidi na kufikia  kilomita 150 kwa saa, huku baadhi ya maeneo ya pwani ya Bahari ya Hindi yakianza kupata madhara. Mpaka saa 9 mchana, Mei 3 kimbunga Hidaya kilianza kuikaribia Tanzania huku kikipungua kasi hadi kufikia kilomita 110 kwa saa.

Mei 4 kimbunga Hidaya kilitua katika Kisiwa cha Mafia kikiwa na kasi ya kilomita 95 kwa saa na kusababisha madhara kadhaa kama kuangusha miti, miundombinu ya umeme na mvua kubwa.

Mei 5 kiliifikia Tanzania hususani mikoa ya Lindi, Mtwara na Morogoro kilipungua nguvu hadi kilomita 55 kwa saa na kuwa cha kawaida kisichosababisha madhara.