Sababu mihimili mitatu kushindwa kuwajibishana

Muktasari:

  • Kama watu waliopaswa kuijua Katiba hawaijui, watu wanakula kiapo cha kuilinda na kuitetea Katiba ndiyo hao wanaikanyaga, kuivunja na kuikiuka, unategemea nini kwa mwananchi wa kawaida kuijua Katiba?

Katika toleo lililopita, tuliangalia dhana ya “Katiba ndio sheria mama” na kuona mchakato mzima wa Bunge kutunga sheria na namna Bunge linavyoweza kufanya makosa katika kutunga sheria, Serikali ikashindwa kuzitekeleza na pia Mahakama inavyoweza kukosea kutafsiri sheria.

Tuliangalia pia mtu pekee ambaye hana kosa katika hili la sheria batili ni Rais kwa kusaini sheria batili inayokwenda kinyume cha Katiba kuwa sheria halali na kuanza kutumika rasmi, kwa sababu Rais ana wasaidizi anaowaamini, hivyo sheria batili hizo zikifika mezani kwake, yeye anaanguka saini na zinakuwa sheria.

Kama watu waliopaswa kuijua Katiba hawaijui, watu wanakula kiapo cha kuilinda na kujitetea Katiba ndiyo hao wanaikanyaga, kuivunja na kuikiuka, unategemea nini kwa mwananchi wa kawaida kuijua Katiba?

Leo tunaendelea kuangalia ukuu wa Katiba. Wakati fulani baada ya Bunge kutunga sheria batili, kuna mwananchi mmoja mzalendo, akafungua shauri Mahakama Kuu kupinga sheria batili hiyo, akashinda, Mahakama Kuu ikaitangaza ni batili na kutoa amri ifutwe kwenye vitabu vya sheria.

Mzalendo yule hakukubali Katiba yetu inajisiwe, akafungua shauri jingine kupinga mabadiliko hayo, Mahakama Kuu ikampa ushindi, ikatangaza mabadiliko hayo ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni batili.

Serikali yetu haikukubali ikakata rufaa Mahakama Kuu ya Rufaa kupinga uamuzi huo wa Mahakama Kuu, kutamka kipengele cha katiba ni batili.

Mahakama Rufaa ikawaita manguli watatu wa sheria kuwa marafiki wa Mahakama, ambao kisheria huitwa “Amicus Curiae”, na ndio ikatoa uamuzi wa ajabu kabisa kuwahi kutokea kwenye historia ya Mahakama zetu, ambao mimi nauita ni uamuzi sarakasi!

Kama mtakumbuka mwanzo nilisema mihimili hii mitatu ina wajibu wa kuheshimiana na kutoingiliana, lakini pia kila mhimili ni kiranja wa mhimili mwingine kupitia kanuni ya “the doctrine of separation of powers, checks and balance”.

Serikali ikikiuka mamlaka yake inadhibitiwa na Bunge na Mahakama, Bunge lilikiuka mamlaka yake inaadhibitiwa na Serikali na Mahakama, Mahakama nayo ikikiuka mamlaka yake inadhibitiwa na Bunge na Serikali.

Kwa mujibu wa Katiba yetu, vyombo hivyo vyote vitatu viko chini ya Katiba, na vyombo vyote vina wajibu wa kuilinda na kuitetea Katiba ya JMT, hakuna chombo kinachoruhusiwa kuwa juu ya katiba au kutunga sheria batili inayokwenda kinyume cha katiba!

Kitendo cha Serikali kupeleka bungeni muswada wa sheria batili ni kosa, Serikali yetu ilipaswa kuadhibiwa.

Kitendo cha Bunge kutunga sheria batili, Bunge lilipaswa kuadhibiwa. Swali ni nini kinachofanya mihimili hii yetu mitatu isifanyiane “checks and balance” (isiwajibishane)? Hii ni mada inayojitegemea.

Angalau Mahakama Kuu ya Tanzania, ilitimiza wajibu wake kwa kusema sheria hiyo ni batili na mabadiliko ya Katiba kuiingiza batili hiyo ndani ya sheria zetu ni batili.

Mahakama ya Rufani ndio ikatoa kubwa kuliko. Ikasema “The court is not the custodians of the will of the people” (Mahakama siyo mlinzi wa matakwa ya wananchi). Hapa the “will of the people” ni Katiba. Mahakama ya Rufani imejivua jukumu la kuilinda na kuitetea Katiba ya JMT.

Imetungwa sheria batili inayokwenda kinyume cha katiba. Mahakama Kuu imetangaza sheria hiyo ni batili. Serikali ikakata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu kuibadilisha sheria batili hiyo. Serikali ikashindwa, ikafanya mabadiliko ya katiba kwa kuichomekea batili hiyo ndani ya katiba yetu

Mahakama Kuu ikasema mabadiliko hayo ni batili. Serikali ikakata rufaa Mahakama ya Rufaa kupinga uamuzi huo wa Mahakama Kuu.

Mahakama ya Rufani badala ya kushughulika na ukiukwaji wa Katiba yetu kwa kutungwa sheria batili inayokwenda kinyume cha Katiba, yenyewe ikajikita kwenye kuangalia uwezo wa Mahakama kuliingilia Bunge kwenye uchomekeaji ubatili ndani ya Katiba yetu.

Ikatoa uamuzi wa ajabu kabisa kuwa Mahakama Kuu haina uwezo wa kuliingilia Bunge. Hivyo, kama Bunge limetunga sheria batili na kufanya mabadiliko batili ya Katiba, ni jukumu la Bunge lenyewe kutengua sheria hiyo batili na kutengua mabadiliko hayo batili ya Katiba.

Hadi leo ninapoandika makala hii, Bunge letu halijafanya lolote. Sheria hiyo batili bado ipo kwenye sheria zetu, ubatili uliochomekewa kiubatili ndani ya Katiba yetu bado upo. Hivi sivyo alivyodhamiria mtunga Katiba.

Je, sheria hiyo batili ni ipi, ubatili wake ni upi na una madhara gani? Tukutane wiki ijayo kwenye sehemu nyingine ya kuijua Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jicho la mtunga Katiba.

Pia, tutaangalia Mahakama Kuu ya Tanzania ilivyoitengua sheria hiyo, kisha serikali ikakata rufaa, ikashindwa, ikaamua kuuchomekea ubatili huo ndani ya Katiba.