Sababu ndoa kuzidi kuvunjika zatajwa

Muktasari:

  • Malezi yasiyo wezeshi kwa vijana, kuiga mila na desturi za nje, kipato kidogo kwa wanandoa na mfumo dume, vimetajwa kuwa miongoni mwa sababu za migogoro inayovunja ndoa.


Dar es Salaam. Malezi yasiyo wezeshi kwa vijana, kuiga mila na desturi za nje, kipato kidogo kwa wanandoa na mfumo dume, vimetajwa kuwa miongoni mwa sababu za migogoro inayovunja ndoa.

Hayo yalibainika katika kongamano la ndoa na familia jijini hapa jana, lililoandaliwa na Shirika la TaMcare.

Katika kongamano hilo, ilielezwa kuwa mwaka 2021 Mkoa wa Dar es Salaam ulisajili migogoro ya ndoa 13,289 kupitia halmashauri zake, huku 284 kati ya hiyo ikienda mahakamani.

Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa, Nyamara Elisha alisema vijana wamekuwa wakikosa malezi wezeshi ya ndoa na hupatiwa ya misingi ya dini pale tu wanapotaka kuolewa au kuoa.

“Hili la kukosa uelewa na elimu katika familia husika ni moja ya changamoto zinazosababisha kuwapo kwa migogoro mingi katika ndoa,” alisema Elisha.

Alisema baadhi ya watu wamekuwa wakiangalia maigizo ya mitandaoni, namna watu wa magharibi wanavyoishi na kuileta katika familia, jambo linalokinzana na mila na desturi za ndani ya nchi.

“Pia, wengi wanaingia katika ndoa kwa ushabiki, wengine wameona mmoja wakati wa ndoa yake amepewa zawadi hii anaamini na yeye akiingia katika ndoa zawadi zile zitatolewa, lakini linapokuja suala la kuwajibika kama mwanandoa inakuwa ni changamoto inayofanya wanandoa hao kutafuta kutengana,” alisema Elisha.

Kuhusu mifumo dume, alisema baadhi hushindwa kuelewa kama ndoa ni taasisi na haiendeshwi na mtu mmoja, lakini yupo anayetamani kuendesha kila kitu mwenyewe, jambo linaloleta migogoro.

Dk Enock Mlukya, ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Tamcare, alisema mashauri yanayoongoza kuwasilishwa ni ya vijana na mara zote wanaume ndio wanalalamikiwa kushindwa kuwajibika ipasavyo.

“Imefika wakati tukiwawezesha wanawake na wanaume wawezeshwe kwa sababu tunakokwenda si kuzuri,” alisema Dk Mlukya.

“Watu wengi wanatembea na maumivu katika mioyo yao, si jambo zuri kiuchumi, kijamii na kiafya, mtu asiye na furaha hawezi kufanya kazi zake vizuri na hatuwezi kuendelea kimwili, kiuchumi na kiroho; kama hakuna maadili mema yanayompendeza mwanadamu na Mungu.”

Alisema itengwe siku maalumu ya kitaifa ya wanandoa ili kudumisha uhusiano mwema katika wanandoa na iwepo siku maalumu ya maadhimisho ya wanawake wasiokuwa na wenzi ili kutambua mchango wao.

“Pia, yafanyike mapitio ya sheria na kanuni za kuwapanga vituo vya kazi watumishi, tofauti na sasa mke Kigoma, mume yupo Dar es Salaam, hii inasababisha upweke, kuongeza uchumi wa familia; fedha zitafutwe ila zisiwe chanzo cha migogoro katika familia,” alisema Dk Mlukya.

Kauli hiyo imekuja ikiwa ni siku moja tangu Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete kusema matukio ya watu kuuana kwa sababu ya mapenzi yanatokana na utofauti wa binadamu katika kuhimili mambo na kufikia hatua ya kuchukua uamuzi mgumu.

“Sio kwamba sasa hivi ndio yanatokea sana, yalikuwepo tangu zamani, hili ni suala la kuhimili, wengine wana uwezo huo ikitokea amekataliwa basi anaendelea na maisha atatafuta mwingine,” alisema Kikwete, aliyekuwa Rais kati ya 2005-2015.

“Hata haya masuala ya kuvunjika ndoa ni kushindwa kuhimili, kila mtu ana uwezo wake katika kuvumilia na kuyachukulia mambo.”

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima alisema Julai 2021 hadi Juni 2022 wizara imepokea matukio ya changamoto za ndoa na familia 75,873, kati ya hayo, matatizo ya ndoa ni 23,335 sawa ana asilimia 30.7 na mashauri yanayohusu matunzo ya watoto 32,344 sawa na asilimia 42.6.

“Mashauri yanayohusu watoto wa nje ya ndoa ni 20,194 sawa na asilimia 26.6. Takwimu hizi zinaonyesha jinsi gani taasisi ya ndoa ilivyoyumba na kusababisha shida kwa watoto,” alisema Dk Gwajima.

Alisema tatizo ni kubwa kwa taasisi hiyo ya ndoa, hivyo wakubaliane wapi wameyumba na wakubaliane wapi wamekosea ili waweze kuirejesha.