Sababu watu kupata magonjwa ya figo zatajwa

Muktasari:

  • Watanzania wametakiwa kuzuia magonjwa ya figo kwa kuweka utaratibu mzuri wa ulaji wa vyakula.

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Mohamed Janabi amesema kwa kiwango kikubwa magonjwa ya figo yanasababishwa na mfumo wa maisha ikiwemo ulaji usiofaa wa vyakula.

Profesa Janabi amesema ulaji huo wa vyakula unachangia ugonjwa wa kisukari ambao ndiyo chanzo kikubwa cha magonjwa sugu ya figo.

Kauli hiyo ameitoa jana, Jumapili, Desemba 10, 2023 wakati wa uzinduzi wa Taasisi ya Profesa Jay Foundation inayolenga kutoa msaada kwa wagonjwa wa figo ambapo amesema kuna uwezekano mkubwa wa kuzuia magonjwa hayo kama watu watakuwa na utaratibu mzuri wa ulaji wa vyakula.

Amesisitiza umuhimu wa kufanya vipimo ili kutoa fursa ya matibabu kufanyika mapema kwa kuwa takwimu zinaonyesha wagonjwa wengi wa figo hufika hospitali katika hatua za mwisho.

“Wagonjwa wengi wanaofanya dialysis (uchujaji wa damu) wanaishia kupata msongo wa mawazo kwa sababu ni saa nne mara tatu kwa wiki siyo kitu rahisi kuona damu yako inatoka inarudi. Hapa ndiyo wengi wanaingia kupoteza maisha

“Tunaweza kuyaepuka hayo kwa kuchukua hatua za mapema kabisa kwa kuwa na mfumo mzuri wa maisha hasa katika eneo la vyakula, changamoto tuliyonayo tunakula mara nyingi,” amesema Profesa Janabi.

‘Mtaalamu huyu wa magonjwa ya moyo amesema ukubwa wa tatizo la figo unazidi kudhihirika kutokana na kuwepo watoto wadogo wanaobainika kuwa na tatizo hilo.

“Pale wodi ya wazazi unaona mtu amejifungua mtoto mwenye kilo 4 ndugu wanasema mashallah, hilo siyo la kufurahia ni tatizo si sahihi kwa mtoto kuzaliwa akiwa na uzito mkubwa kupita kiasi,” amesema Profesa Janabi.

Katika hatua nyingine ameelezea maboresho yaliyofanywa na MNH katika huduma zake akieleza teknolojia iliyowekwa sasa inaweza kumtibu mgonjwa wa kiharusi endapo atafikishwa hospitali ndani ya saa 24 tangu apate ugonjwa huo.

Amesema kuwa kuanzia Januari watafungua jengo linalohusika na huduma za upandikizaji mimba ambapo pia watatoa huduma ya kuhifadhi mayai kwa watu ambao hawahitaji kupata watoto kwa wakati husika.

Akizungumza kwenye halfa hiyo Mwenyekiti wa Profesa Jay Foundation Joseph Haule, alitoa shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha matibabu yake na Watanzania ambao wamemuunga mkono katika jitihada zake za kuanzishisha taasisi hiyo itakayosaidia wahitaji wakiwemo wagonjwa wa figo.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema Tundu Lissu ni miongoni wa waliohudhuria halfa hiyo iliyohusisha harambee ambapo alichangia Sh1 milioni.

Wengine waliochangia ni timu ya Yanga Sh5 milioni, Lady Jaydee Sh5 milioni, Kings Music na Alikiba Sh5 milioni, Weusi Sh1 milioni, Chege, Temba na Juma Nature kwa pamoja wamechangia Sh2 milioni.