Samia atuma ujumbe ALAT

Samia atuma ujumbe ALAT

Muktasari:

  • Mkutano huo unaofanyika jijini Dodoma, pia umehudhuriwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Waziri wa Tamisemi Ummy Mwalimu ambao ndio wasimamizi wakuu wa Serikali za Mitaa nchini.

Rais Samia Suluhu Hassan amefungua mkutano wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) huku akituma ujumbe wa kudumishwa kwa ushirikiano kati ya jumuiya hiyo na wadau wa maendeleo ikiwemo benki ya NMB.


Pia, Rais Samia amepongeza jitihada za NMB kwa kukubali kubeba dhamana ya kufanikisha mkutano huo ambao, wajumbe wanatarajiwa kuwachagua viongozi huku akiwataka kuchagua viongozi sahihi.


Rais Samia ameyasema hay oleo Jumatatu Septemba 27,2021 wakati akifungua mkutano huo na kuwataka wajumbe kuitendea haki kaulimbiu ya mkutano huo isemayo: 'Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu,' akisema ALAT imara ndio msingi mkuu wa maendeleo endelevu yanayochakatwa na Serikali yake.


Pia, amekwenda mbali zaidi kwa kuwataka viongozi wateule wa uchaguzi huo kuisimamia ALAT kufanya kazi kwa kufuata sheria, haki na uadilifu, na kwamba anategemea viongozi wa kada hiyo katika kusimamia makusanyo na matumizi ya fedha za miradi ya halmashauri na kuwataka wajiepushe na ubadhirifu.


"Fanyieni kazi vipaumbele muhimu ambavyo ni pamoja na kutenda haki, kufanya kazi kidijitali, ushirikiano baina ya mameya, wenyeviti wa halmashauri, Wakurugenzi na wakuu wa Wilaya, ili kumaliza tatizo la ubaadhirifu na ufujaji wa fedha.


“Kahakikisheni thamani ya pesa kwa miradi mnayosimamia utekelezaji wake inaonekana," alisisitiza Rais Samia.


Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, amesema wamedhamini mkutano huo kwa Sh150 milioni huku akijivunia makusanyo ya zaidi ya Sh6 trilioni kupitia Mfumo wa Ukusanyaji Mapato ya Serikali Kielektroniki (GePG) katika kipindi cha miaka mitatu iliyoishia Julai, 2021.


Amesema wanajivunia ushirikiano wao na ALAT ambao umekuwa chachu ya udhamini wao mara kwa mara mikutano hiyo na kuwa anaamini jumuiya hiyo itauenzi uhusiano huo, huku wakiendelea kuifanya NMB kuwa namba moja katika makusanyo ya halmashauri zote nchini.


"Matarajio yetu ni kuendekeza uhusiano mwema kati ya ALAT na NMB, pamoja na ushirikiano mzuri na halmashauri zote katika kukamilisha miradi mikubwa inayosimamiwa na halmashauri zetu,” amesema Zaipuna.