Serikali inakabili changamoto ya dawa kuharibika kabla ya matumizi

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Dk Festo Dugange akizungumza wakati akijibu maswali kwenye kipindi cha maswali na majibu leo Mei 8,2024.Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Katika mwaka wa fedha 2022/23 Serikali ilitoa Sh266.7 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa za afya katika ngazi ya afya ya msingi.

Dodoma. Katika kukabiliana na changamoto ya dawa kuharibika kabla ya kutumika, Serikali imesema zinazopelekwa hospitali huchukua angalau miezi 12 kabla ya muda wa matumizi kuisha.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Festo Dugange, amesema hayo leo Mei 8, 2024 alipojibu maswali ya mbunge wa viti maalumu, Ghati Chomete.

Katika swali, mbunge huyo amesema Bohari Kuu ya Dawa (MSD) imekuwa na tabia ya kupeleka dawa kwenye zahanati na hospitali ambazo zimekaribia kuisha muda wake wa matumizi.

“Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha jambo hili linamalizika ili lisilete madhara kwa wananchi?” amehoji mbunge huyo.

Dk Dugange amesema wamekaa na Wizara ya Afya kujadili suala hilo, kuhakikisha wanapeleka dawa zenye muda mrefu wa kuisha matumizi yake.

“Tayari katika mwaka wa fedha 2021/22 kwa sehemu kubwa angalau zimebakisha miezi 12 kabla ya kumalizika muda wake. Na tutaendelea kufanya hivyo,” amesema.

Mbunge huyo pia ameeleza Kituo cha Afya cha Mara kinahudumia wananchi wa kata tano ambao idadi yao inazidi 73,000 lakini Serikali imekuwa ikipeleka dawa za kuhudumia wananchi 14,000.

Kutokana na hilo, ametaka kujua Serikali ina mpango gani wa kupeleka dawa katika kituo hicho.

Katika swali la msingi alihoji Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha dawa zinapatikana kwa viwango vya kukidhi mahitaji katika zahanati, vituo vya afya na hospitali za Mkoa wa Mara.

Naibu Waziri, Dk Dugange amesema mwaka 2022/23 Serikali ilitoa jumla ya Sh266.7 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa bidhaa za afya katika ngazi ya afya ya msingi.

Amesema kati ya fedha hizo Sh200 bilioni zilikuwa za ununuzi wa dawa na vitendanishi, na Sh66.7 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na vifaatiba.

Dk Dugange amesema Mkoa wa Mara ulitengewa Sh4.67 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vitendanishi kupitia MSD na washitiri.

Amesema mwaka 2023/24 Serikali imeendelea kuongeza bajeti ya dawa na vifaatiba kwa kutenga Sh322.3 bilioni kwa ajili ya vituo vya kutolea huduma ngazi ya afya ya msingi.

Amesema kati ya fedha hizo Sh205 bilioni ni kwa ajili ya dawa na vitendanishi na Sh117.3 bilioni kwa ajili ya vifaa na vifaatiba.

Amesema hadi kufikia Februari 2024 Mkoa wa Mara umepokea Sh2.7 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa dawa na Sh5.5 bilioni kwa ajili ya vifaa na vifaatiba.

Amesema kumekuwa na ongezeko la upatikanaji wa dawa kwenye vituo katika Mkoa wa Mara kutoka asilimia 88 mwaka 2022/23 hadi asilimia 90.01 mwaka 2023/24.