Serikali kutunga sera ya Taifa ya Haki Jinai

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Wizara ya Katiba na Sheria inalenga kuendelea kuboresha utoaji wa huduma za kisheria na utoaji haki kwa umma ili kuendana na mipango ya sekta ya sheria nchini.


Dodoma. Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2024/2025 imekuja na vipaumbele 15 kutoka 30 vya mwaka 2023/24, ikiwa ni pamoja na kutunga sera ya Taifa ya Haki Jinai.

Wizara pia imeeleza namna ilivyoratibu mchakato wa Katiba mpya.

Hayo yamesema leo Aprili 29, 2024 na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Pindi Chana alipowasilisha bungeni mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya wizara kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Wizara imeliomba Bunge kuidhinisha Sh441.2 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo.


Mkakati elimu ya Katiba

Katika hatua nyingine, Dk Chana amesema wizara imetekeleza mkakati wa kutoa elimu ya Katiba na uraia kwa umma.

Akizungumzia utekelezaji wa vipaumbele vya mwaka wa fedha uliopita, amesema wizara ilifanya kazi ya kuratibu mchakato wa Katiba mpya na elimu ya uraia.

“Katika kipindi cha Julai 2023 hadi Aprili, 2024, Wizara imeendelea kutoa elimu kuhusu masuala ya kikatiba na utawala wa sheria kwa umma kupitia vyombo vya habari vikiwemo redio, televisheni, mitandao ya kijamii na tovuti ya wizara,” amesema.

Amesema jumla ya wananchi 267,323 wamefikiwa na elimu ya Katiba na uraia kwa umma kupitia maadhimisho ya kitaifa, ikiwa ni pamoja na Wiki ya Sheria, Wiki ya Msaada wa Sheria, makongamano, warsha, semina na midahalo.

Dk Chana amesema wizara kwa kushirikiana na wadau wa elimu imeainisha masuala ya kikatiba yanayohitajika kujumuishwa kwenye mitalaa ya elimu.

Aidha, alisema katika kuimarisha mfumo wa utoaji elimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, wizara yake kwa kushirikiana na wizara nyingine na taasisi nyingine imeandaa rasimu ya mkakati wa kitaifa wa kuitoa kwa umma.


Amesema taasisi zilizoshiriki ni Ofisi ya Waziri Mkuu - Sera, Bunge na Uratibu kwa upande wa Tanzania Bar ; na Utumishi na Utawala Bora na Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera Uratibu na Baraza la Wawakilishi za Zanzibar.

Dk Chana amesema mkakati huo unalenga kuhakikisha wananchi wanapata uelewa wa Katiba ikiwa ni pamoja na kufahamu haki na wajibu wao kwa Taifa na kuwawezesha kushiriki katika mijadala ya kikatiba.

“Rasimu hiyo itajadiliwa na kufanyiwa uamuzi ndani ya Serikali kabla ya kuanza kutumika,” amesema.

Wizara katika mwaka wa fedha 2023/2024, iliidhinishiwa na Bunge Sh383.6 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo.

Hata hivyo, fedha zilizopelekwa kwenye wizara hiyo ni Sh273.6 bilioni sawa na asilimia 71.33 ya Sh383.6 bilioni zilizoidhinishwa na Bunge katika mwaka 2023/2024.

Vipaumbele vipya

Dk Chana ametaja vipaumbele 15 vya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/2025, kwamba ni kuendelea kuboresha utoaji wa huduma za kisheria na utoaji haki kwa umma ili kuendana na mipango ya sekta ya sheria nchini; na mipango ya kikanda na kimataifa ili kufikia malengo yaliyopangwa kwa kipindi husika.

Katika kufikia azma hiyo, amesema maeneo ya kipaumbele ni kutunga sera ya Taifa ya Haki Jinai, kushughulikia masuala ya kikatiba ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya Katiba na uraia kwa umma na kusimamia mfumo wa haki na utoaji haki, ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu ya Mahakama, kuharakisha mashauri ya kawaida na kumaliza mashauri ya muda mrefu.