Serikali yacharuka malipo fedha za Tasaf kwa wasiohusika

Waziri wa nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene akizungumza na watumishi mara baada ya kupokea taarifa ya Tasaf mkoani Geita.

Muktasari:

Waziri wa nchi ofisi ya ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene ameagiza kusitishwa kwa fedha zinazotolewa kwa walengwa wasio na sifa wa Mpango wa kunusuru Kaya maskini nchini (Tasaf) na badala yake fedha hizo zipangiwe kazi nyingine.

Geita. Waziri wa nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene ameagiza kusitishwa kwa fedha zinazotolewa kwa walengwa wasio na sifa wa Mpango wa kunusuru Kaya maskini nchini (Tasaf) na badala yake fedha hizo zipangiwe kazi nyingine.

Waziri Simbachawene ametoa maagizo hayo leo Septemba 13, 2023 baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa mpango wa Tasaf Mkoa wa Geita ambapo amewataka wakuu wa mikoa na waratibu wa Tasaf kote nchini kusitisha malipo wanapobaini mapungufu kuhusu taarifa za walengwa.

Ameuagiza uongozi wa Tasaf kutafuta mfumo mzuri wa malipo kwa walengwa kukabiliana na changamoto za udanganyifu unaodaiwa kufanywa na baadhi ya ndugu wa walengwa wakishirikiana na mawakala wa huduma za malipo kwa njia ya simu.

“Mpango wa Tasaf wa kufanya malipo kwa njia ya simu ulilenga kupunguza gharama za uendeshaji, lakini kumeibuka changamoto ya fedha kutowafikia walengwa, hasa wasioweza kutumia simu kutokana na udanganyifu unaofanywa na baadhi ya ndugu na watoa huduma. Lazima tutafute namna ya kudhibiti tatizo hilo,’’ amesema waziri huyo

Amesema Serikali inatoa fedha nyingi kupitia mpango wa kunusuru kaya maskini ambapo kwa Mkoa wa Geita pekee, zaidi ya Sh100 bilioni zimetolewa, hivyo ni dhamira ya Serikali kuona fedha zote zinafika kwa walengwa.

Kwa mujibu wa Katibu Tawala Msaidizi (Mipango na Uratibu), Deodatus Kayango, walengwa 220, 666 kutoka kaya 46,749 za mkoa huo tayari wamepokea zaidi ya Sh35.4 bilioni kutoka Tasaf.

Amesema katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2023, mkoa huo umepokea zaidi ya Sh8.09 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kuondoa umaskini kupitia ujenzi wa miundombinu ya elimu, afya, miradi ya ajira za muda na miradi ya vikundi vya walengwa wa Tasaf.

Ametaja baadhi ya mafanikio ya miradi ya Tasaf kuwa ni kuwezesha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kupata mahitaji ya shule, uhakika wa milo miwili na ujenzi wa makazi bora kwa familia za walengwa.