Serikali yaja na mwarobaini mafuriko ya Rufiji

Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi.

Muktasari:

Serikali inakuja na hatua hiyo kipindi ambacho maeneo mbalimbali yameripotiwa kuathiriwa na mafuriko yaliyosababisha vifo vya watu 58 nchini

Dar es Salaam. Serikali imesema inatarajia kujenga mabwawa mawili bonde la mto Rufiji ikiwa ni hatua za muda mrefu za kukabiliana na athari za mafuriko katika eneo hilo.

Mabwawa hayo mawili yanayojengwa Rufiji ni kati ya 127 ambayo Serikali inatarajia kuyajenga katika Mikoa mbalimbali nchini na tayari upembuzi wake yakinifu umeshafanyika.

Ambapo 14 ujenzi wake umeshaanza katika maeneo mbalimbali nchini.

Serikali inakuja na hatua hiyo kipindi ambacho maeneo mbalimbali yameripotiwa kuathiriwa na mafuriko yaliyosababisha vifo vya watu 58 nchini na kuacha wengine bila makazi huku kaya 10,839 katika mikoa ya Morogoro na Pwani zimeathiriwa na mafuriko hayo.

Hayo yameelezwa leo Jumapili, Aprili 14, 2024 na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi alipotoa taarifa ya hali ya maafa ya mafuriko kwa waandishi wa habari.

Moja kati ya mabwawa yatakayojengwa Rufiji ni Ngorongo litakalokuwa na uwezo wa kupokea mita za ujazo milioni 164.15.

Ameeleza matumizi ya maji ya bwawa hilo, yanatafajiwa kuwa mita za ujazo milioni 38.47 kwa mwaka kwa ajili ya shughuli za kilimo na uvuvi.

Matinyi amesema bwawa lingine ni Mbakia Mtuli, litakalokuwa na ukubwa wa mita za ujazo milioni 100.7 na matumizi yanayokadiriwa ni mita za ujazo milioni 25.85.

Sambamba na mabwawa hayo, amesema mabwawa mengine 14 yanaendelea kujengwa katika maeneo mbalimbali nchini.

"Sambamba na hayo 14, kuna mengine 127 ambayo upembuzi yakinifu wake umeshakamilika na Aprili 20, mwaka huu zabuni itatangazwa kumpata mkandarasi," amesema.

Katika kufanikisha kazi hiyo, amesema bajeti ya tume ya umwagiliaji imeongezeka kutoka Sh46 bilioni mwaka 2020/21 hadi Sh364 bilioni mwaka 2023/24.

Athari za mafuriko

Kuhusu athari za mafuriko, Matinyi amesema kati ya watu 58 waliopoteza maisha, 10 kutoka Arusha, wawili Dar es Salaam, wanne Geita, watano Iringa, mmoja Kilimanjaro, Lindi wanne, sita Mbeya, Morogoro watano, Pwani 11 na Rukwa 10.

Ameeleza athari kubwa zaidi zimetokea katika mikoa ya Pwani na Morogoro huku jumla ya nyumba 8,532 na mashamba ekari 76,698 yameathirika.

Amezitaja hatua zilizochukuliwa ni uokoaji wa watu 2,278, kuanzisha kambi nane zenye jumla ya watu 1,529, kutoa huduma ya tiba bure na misaada ya kibinadamu.

"Chakula tani 40 za mahindi, vifaa vya makazi vikiwamo vyandarua 500, mablanketi 400, mahema matano na ndoo 300. Aidha tani 43 za unga na 25 za maharage zipo njiani zinapelekwa," ameeleza.

Ameeleza wataalamu wa afya 20 wamepelekwa na askari mbalimbali pia kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na usalama.