Serikali yaongeza posho kwa wasimamizi wa uchaguzi

New Content Item (1)

Dodoma. Serikali imefanya maboresho kwa kuongeza viwango vya posho za wasimamizi wa uchaguzi na wasaidizi wao kupitia Waraka wa Utumishi wa Umma uliotolewa Mei 24, 2022.

Naibu Waziri wa Nchi (Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana  na wenye Ulemavu) Patrobas Katambi amesema hayo leo Jumatatu Aprili 22, 2024 wakati akijibu swali la mbunge wa viti maalumu Angelina Malembeka.

Malembeka amehoji kuna mpango wa kuongeza posho kwa askari na maofisa wasimamizi wa uchaguzi.

Akijibu swali hilo, Katambi amesema wakati wa uchaguzi, wasimamizi wa uchaguzi na wasaidizi wa uchaguzi wa ngazi ya jimbo na kata, hulipwa posho za kujikimu wanapokuwa wanatekeleza majukumu ya uchaguzi kwa kuzingatia Waraka wa Utumishi wa Umma kuhusiana na posho za Serikali.

“Kwa sasa, Serikali imefanya maboresho kwa kuongeza viwango vya posho hizo kupitia Waraka wa Utumishi wa Umma uliotolewa Mei 24, 2022,”amesema Katambi.

Amesema kwa upande wa watendaji na walinzi wa vituo vya kupigia kura, utaratibu wa uboreshaji wa viwango vyao vya posho utazingatiwa wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura na bajeti ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Katika swali la nyongeza, Malembeka amehoji hawaoni kama kuna haja ya kuanza kulipa posho hiyo kuanzia mwaka huu ili kuleta motisha katika chaguzi hizo.

Pia, Malembeka amesema upande wa Zanzibar huwa wanasimamia chaguzi mbili ule wa Zanzibar na Tanzania na kuhoji hawaoni sababu ya kulipa posho mbili.

Akijibu maswali hayo,   Katambi amesema waraka umeanza kutumika tangu Mei mwaka jana kwa hiyo zingatio la mbunge huyo la kuanza kulipa nyongeza ya posho hiyo katika uchaguzi wa Serikali za mitaa lipo.

“Maboresho yatafanyika pindi tume itakapokuwa imekaa na kufanya tathimini ikiwa ni pamoja na kupitisha bajeti ya mwaka huu; mazingatio hayo yote yatakuwa ndani ya bajeti hiyo,”amesema Katambi.

Kuhusu kulipa posho mbili kwa Zanzibar, Katambi amesema wanalichukua suala hilo na watazingatia kwa mujibu wa taratibu, sheria na kanuni.