Sikukuu ya Idd na namna ya kuisherehekea

Muktasari:

  • Ni sunna kwenda sehemu ya kusali Idd kwa njia moja na kurudi kwa njia nyengine.

Allah Aliyetukuka ameweka sheria mbalimbali kwa waja wake ili waweze kujikurubisha kwake na kupata ziada ya thawabu katika mizani ya amali zao njema siku ya Kiyama.

Hapa tutataja baadhi ya ibada ambazo Muislamu anatakiwa azipupie punde tu baada ya kumalizika kwa Ramadhani.


Mosi: Kutoa Zakatul–Fitri

Mtume (rehema na amani ya Allah ziwe juu yake) amefaradhisha zaka ya Fitri kwa kila Muislamu mwanamume na mwanamke, mtoto mdogo, muungwana na mtumwa. Muislamu atajitolea zaka ya fitri yeye mwenyewe pamoja na wanawe ambao bado wanamtegemea, wazazi wake, mkewe na wale wote ambao chakula chao cha kila siku kinamuwajibikia yeye.

Mtume ameamrisha zaka hii wapewe mafukara na masikini kabla ya kwenda kusali Idd. Na kiwango kinachotakiwa kisharia kutolewa zakatul– fitri ni pishi moja (kilo mbili na nusu) ya chakula kinachopendwa zaidi na wakazi wa mji husika, kama vile mchele au ngano au tende na mfano wake.


Pili: Kuleta takbira

Hii ni katika sunna kubwa za siku ya Idd kwani Allah Aliyetukuka anasema: “...Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito, na mtimize hiyo hesabu, na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuongoeni ili mpate kushukuru.” [Quran, 2:185].

Takbira zinatakiwa zitolewe baada ya kuzama kwa jua katika siku ya mwisho ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani, yaani usiku wa Idd el Fitri.


Namna ya kuleta takbira

Muislamu anatakiwa alete takbira nyumbani, njiani na misikitini kwa sauti kama utambulisho wa kufika Sikukuu ya Idd.

Takbira ianze kuletwa pale jua tu linapozama katika siku ya mwisho ya Ramadhani. Na takbira hizi zitaendelea hadi katika viwanja vya wazi. Na zitakoma baada ya sala ya Idd.

Imethibiti kutoka kwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) kwamba alikuwa akileta takbira mpaka anapomaliza sala.

Na namna sahihi ya kuleta takbira ni kusema: “Allahu akbar, Allah akbar, Lailaahaillalla, Allahu Akbar, Allahu Akbaru, walillahil hamdu.” (Mwenyezi Mungu ni Mkubwa, Mwenyezi Mungu ni Mkubwa.

Hapana apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu ni Mkubwa, Mwenyezi Mungu ni Mkubwa, na sifa njema zinamsatahiki Yeye).


Adabu za sala ya Idd

Moja ni kuoga kabla ya kwenda kusali. Ni mustahab (inapendeza) kuoga kabla ya kwenda kusali Idd na kujipaka manukato mazuri kwa wanaume, kwani hivyo ndivyo walivyokuwa wakifanya watu wema waliotangulia.

Ni Sunna pia kupiga mswaki na kujipaka mafuta mazuri na manukato kama ilivyosuniwa katika siku ya Ijumaa.

Imesimuliwa hadith sahihi katika Al–Muwatta na kwengineko kuwa Abdullahi bin Umar alikuwa akioga asubuhi ya Idd kabla ya kwenda sehemu ya kusali. Naye Sai’d bin Musayyib (Allah amrehemu) alikuwa akisema: “Sunna za Idd ni tatu; kwenda kusali katika eneo la wazi, kula kabla ya kwenda kusali na kuoga. (Taz: ‘Sheikh Albani katika Ir’waau Al–Ghalili,’ juz. 3, uk. 104).


Kula tende kabla ya kusali sala ya Idul-Fitri

Ni katika sunna kula tende kwa idadi ya witri kabla ya kwenda kusali Idul-Fitri au chakula chochote kile cha halali ikiwa itakosekana tende.

Na huu ndiyo ulikuwa utaratibu wa Mtume wetu. Imesimuliwa na Imam Bukhari kutoka kwa Anas (Allah amridhie), kwamba Mtume hakuwa akienda kwenye eneo la kusalia Idd mpaka kwanza ale kiasi cha tende, na alikuwa akizila kwa witri.

Ama kuhusu hadith ya Buraida kwamba: “Mtume hakuwa akitoka kwenye Idul-Fitri mpaka kwanza ale, na kwenye Idd-al-Adh–haa hakuwa akila mpaka amalize kusali,” pamoja na kuwa hadith hii imetumiwa sana na wanazuoni, sanad yake ina walakini kama alivyoeleza Ibn Hajar kwenye (Al–Fath).


Kuvaa nguo nzuri

Ni sunna kuvaa mavazi mazuri na kujipamba kwa wanaume wanapokwenda kusali Idd. Ama kwa wanawake watakaokwenda kusali Idd hawatakiwi kujipamba wala kujipaka manukato.

Abdullahi bin Umar (Allah amridhie yeye na baba yake) amesema, siku moja Umar alikwenda sokoni akaona juba (nguo ndefu inayovaliwa juu ya kanzu) lililotengenezwa kwa hariri likiuzwa, akalichukua na kumpelekea Mtume wa Allah. Umar akamwambia Mtume: "Ewe Mjumbe wa Allah! Nunua nguo hii na uivae kwa ajili ya kujipamba siku ya Idd na siku ya kupokea wageni maalum."

Mtume akasema: “Hii ni nguo ya watu wasiokuwa na fungu (Akhera).” [Bukhari]. Hadith hii Tukufu inawataka Waislamu kuchunga mipaka ya mavazi, yaani wanaume wasivae mavazi ya kike na wanawake wasivae mavazi ya kiume, wala kusivaliwe mavazi yanayoshabihiana na ya makafiri. Mtume alikataa vazi aliloletewa kwa sababu wanaume wamekatazwa kuvaa hariri.

Imam Ibn Qudama (Allah amrehemu) amesema, kujipamba katika Sikukuu za Idd lilikuwa ni jambo mashuhuri kwa Maswahaba wa Mtume.


Kubadilisha njia ya sehemu ya kusalia

Ni sunna kwenda sehemu ya kusali Idd kwa njia moja na kurudi kwa njia nyengine. Jabir bin Abdillahi (Allah amridhie) ameripoti kuwa, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alikuwa akibadilisha njia siku ya Idd.” [Bukhari].


Kutembea kwa miguu

Ni sunna pia kutembea kwa miguu na kwa utulivu wakati unapoelekea kwenye viwanja vya kusalia Idd ikiwa eneo la kusalia haliko mbali. Sa’ ad (Allah amridhie) amehadithia kuwa Mtume wa Allah (rehema za Allah na amani zimshukie) alikuwa akitembea kwa miguu anapokwenda kusali Idd na kurejea kwa mguu.” (Ibn Maajah, na Sheikh Albani amesema ni hadith sahihi).


Kusali viwanjani

Ni sunna kusali Idd kwenye muswallaa (katika eneo au uwanja ulio wazi), na kama itasaliwa msikitini si makosa – iwapo kuna dharura ya kufanya hivyo. Imepokewa kutoka kwa Abu Sa’id (Allah amridhie) kwamba, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alikuwa akienda kusali Idul-Fitri na Idul-adh-haa kwenye Muswallaa, na jambo la kwanza alilokuwa akifanya ni kusali. [Bukhari na Muslim].


Kupongezana

Waislamu wanapokutana Siku ya Idd, hupongezana kwa dua ya ‘Takabalallahu minnaa waminkum’ Kwa maana, Allah atukubalie mimi na wewe. Na hii ndiyo ilikuwa desturi ya Maswahaba (Allah awaridhie) kila wanapofikiwa na siku ya Idd.

Kuacha mambo yanayomchukiza Allah siku ya Idd

Ni wajibu kwa Muislamu kuacha mambo yanayomchukiza Allah siku ya Idd. Na miongoni mwa mambo yanayomchukiza sana Allah ambayo wengi wetu huyafanya siku ya Idd.


Mosi: Kumshirikisha Allah

Kuna watu wamejenga itikadi kuwa ni lazima kuzuru makaburini siku ya Idd. Watu wenye itikadi hii huyazuru makaburi katika siku ya Idd kwa lengo la kujikurubisha kwa wafu na kuwaomba nusura. Kwa hakika huu ni uzushi na shirk kubwa.

Mwenyezi Mungu anasema: “Na wala usiwaombe wasiyo kuwa Mwenyezi Mungu ambao hawakufai kitu wala hawakudhuru. Ukifanya hivyo basi utakuwa miongoni mwa walio dhulumu. Na Mwenyezi Mungu akikugusisha madhara, basi hapana wa kukuondolea ila Yeye. Na akikutakia kheri, basi hapana awezaye kurudisha fadhila yake. Huifikisha kwa amtakaye katika waja wake, na Yeye ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.” (Qur’an, 10:106– 107)

Muislamu anaruhusiwa kuzuru makaburini siku yoyote katika mwaka na si kutengwa siku maalum kama siku ya Idd.


Pili: Kudharau watu na kutembea kwa maringo

Katika jamii yetu wapo baadhi ya watu ambao hutembea kwa maringo na kiburi katika siku ya Idd; na kibaya zaIdd hujiona wao ndiyo watu bora na wenye hadhi kuliko wengine. Haya yote yameharamishwa katika siku ya Idd na siku nyingine. Allah anasema ndani ya Qur’an: “Wala usitembee katika ardhi kwa maringo. Hakika wewe huwezi kuipasua ardhi wala kufikia urefu wa milima.” [Qur’an, 17:37].

Kadhalika Mwenyezi Mungu anatuambia: “Wala usiwabeuwe watu, wala usitembee katika nchi kwa maringo. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila anayejivuna na kujifaharisha.” [Qur’an, 31:18].

Tatu: Kuhudhuria kumbi za muziki na disko toto

Baadhi ya watu katika siku za Idd huhudhuria katika kumbi za muziki na disko toto, jambo ambalo ni haramu katika Uislamu. Hakika jambo hili limekuwa likisababisha maafa makubwa katika nchi yetu. Tumeshuhudia mara kadhaa watoto wengi wakipoteza maisha kwa kukakanyagana katika kumbi za disko toto.


Nne: Kuchanganyika wanaume na wanawake

Kukusanyika na kuchanganyika wanawake na wanaume katika fukwe za bahari na maziwa au mito na kisha kuoga pamoja, kusikiliza muziki, ngoma, kuvaaa mavazi yanayopingana na sharia na kunywa vinywaji vya haramu ni baadhi tu ya mambo yanayofanywa na baadhi yetu katika siku ya Idd.

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ametutahadharisha kwa kusema: “Watakuja watu katika umma wangu watakaozini, wanaume watavaa hariri, wengine watakunywa pombe, na muziki utahalalishwa.” (Bukhari, Abu Daudi na Bayhaqi)


Tano: Wanawake kuacha hijab

Wapo wanawake wanaotoka nje ya nyumba zao wakiwa hawajavaa vazi la sitara la hijab wakidhani kwamba wameruhusiwa kufanya hivyo katika sherehe za Idd. Kufanya hivyo ni dhambi na chukizo mbele ya Allah ‘Azza Wajallah’. Dini tukufu ya Uislamu imeharamisha wanawake kujipamba na kuonyesha mapambo yao mbele ya wanaume wasiyo maharim katika siku ya Idd na nyinginezo.


Sita: Kufanya ubadhirifu na israfu

Kufanya ubadhirifu na israfu hususan upande wa chakula na mavazi ni katika mambo yenye kuchukiza ambayo baadhi ya Waislamu huyafanya katika Sikukuu za Idd. Allah analionya hilo kwa kusema: “Wala msitumie kwa fujo. Hakika Yeye (Allah) hawapendi watumiao kwa fujo.” (Quran, 6:141).


Saba: Kuacha kuwasidia masikini na mafukara

Waislamu wengi waliojaaliwa kipato hujifaharisha kwa mavazi mbalimbali na mchanganyiko wa vyakula, ilihali kuna uhitaji mkubwa wa chakula na mavazi kwa ndugu na majirani waliomzunguka. Mjumbe wa Allah amesema: “Hatoamini mmoja wenu mpaka ampendelee nduguye kile anachoipendelea nafsi yake.” (Bukhari na Muslim).


Imeandikwa na Seif Ruga