Simba wala ng’ombe 70 Simanjiro

Muktasari:

Wafugaji katika kata ya Ruvu Remit wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wameitaka Serikali iwaue simba hao ili wasiendelee kula mifugo yao.

Simanjiro. Ng’ombe 70 za wafugaji wa kata ya Ruvu Remit iliyopo Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, wameliwa na simba ndani ya wiki moja, hivyo wameiomba Serikali kuingilia kati kwa kuwaua simba hao ili kuokoa mifugo yao.

Akizungumza kwenye kikao cha Baraza la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, leo Jumatatu Mei 6, 2024, diwani wa kata ya Ruvu Remit, Yohana Maitei (Kadogoo) amesema wafugaji hao wako kwenye wakati ngumu.

Maitei amesema ng’ombe 70 za wafugaji hao wameliwa na simba hao kwa muda wa wiki moja, hivyo wanaomba Serikali kupitia kitengo cha maliasili kuwapiga risasi wanyama hao ili wafugaji wapate ahueni.

“Kuna mfugaji mmoja amepoteza ng’ombe wake 20 kwa kuliwa na simba hao, mwingine ng’ombe 10 au wanane au saba na wengine ng’ombe moja moja, hivyo kusababisha umaskini kwao,” amesema Maitei.

Amesema hata wasafiri wanaopita Ruvu Remit kwenda Hedaru, Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro wakiwa kwenye gari huwa wanawaona simba hao wakiwa kwenye njiani.

“Tunaiomba Serikali ibebe hilo kwani wafugaji wamekuwa kwenye wakati mgumu mno kwa kula mifugo yao hivyo kuwasababishia umaskini,” amesema Maitei.

Amesema simba hao wamekuwa na kawaida ya kuingia kwenye maboma usiku na kula mifugo nyakati za usiku na kuwapa hofu vijana  wanaolinda usiku.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Baraka Kanunga amesema hatua zinapaswa kuchukuliwa kwani inaonyesha kundi hilo la simba linaongezeka hivyo kuwapa hasara wafugaji.

“Kuna simba, chui na fisi wote wanapaswa kudhibitiwa, kwani hivi sasa wafugaji wanachukua mikopo benki kwa ajili ya kunenepesha mifugo, sasa hawa wanyama wakali inakuwa shida kwao,” amesema Kanunga.

Hata hivyo, kaimu mkuu wa kitengo cha maliasili na uhifadhi mazingira wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Joseph Shamba amesema changamoto hiyo wameichukua na wataifanyia kazi.

“Tutafanya mawasiliano na wenzetu wa Tawa ili kuja kukomesha tatizo la simba hao wanaokula ng'ombe za wafugaji wa kata ya Ruvu Remit,” amesema Shamba.