Simulizi za kusisimua za waathirika wa mafuriko Moshi

Muktasari:

  • Mafuriko yalitokea usiku wa kuamkia jana  Aprili 25, 2024 na kuisababisha vifo vya watu saba wakiwamo wanne wa familia moja

Moshi. “Nimebaki hivi nilivyo, nilichoweza kuokoa ni wajukuu wangu na watoto wangu.”

Ni kauli ya Marry Agusti mkazi wa Mtaa wa Kwakomba, Kata ya Mji Mpya, Manispaa ya Moshi.

Mama huyu ambaye nyumba yake imeanguka na kusombwa na mafuriko, ameachwa bila chochote, nyumba vyakula na mali nyingine zote zimesombwa na maji.

“Ilikuwa saa tisa usiku, nikasikia mtoto ananiita bibi, bibi, maji, wakati naitika kugeuka, nikakuta yamejaa ndani kila mahali, nikawashika wajukuu tukafanikiwa kutoka ndani,” anasimulia Marry huku akibubujikwa machozi.

Amesema wakati wanatoka ndani, tayari upande mmoja wa nyumba yao ulikuwa umeshaanguka na maji yalizidi kujaa.

"Tulitoka ndani mbio kujiokoa wakati nyumba ikiendelea kuanguka, sikuweza kuokoa chochote, nimebaki hivi nilivyo na watoto na wajukuu zangu,” amesema.

Naye Joyce Swai, amesema kapoteza mali zote ndani ya nyumba alichofanikiwa kuokoa ni watoto wake watatu.

“Taarifa za mafuriko tumezipata baada ya kugongewa geti na majirani wakatuambia kuna mafuriko na maji yanaingia ndani, nikanyanyuka kufungua mlango yakaanza kuingia ndani, nikakimbilia kuwatoa wanangu nikawapeleka eneo lenye muinuko ndani ya geti, nyumba yote ilijaa maji na yakawa yanaondoka na vitu,” amesimulia mama huyo.

Baadhi ya waathirika wa mafuriko, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro wakiwa kwenye hifadhi katika Shule ya Sekondari Lucy Lamecky iliyopo Manispaa ya Moshi baada ya nyumba zao kuharibiwa na mafuriko.Picha na Jesse Tunuka

Amesema walikaa eneo hilo huku wakinyeshewe na mvua hadi saa 11 alfajiri, watu wakaja kuwaokoa baada ya kuvunja ukuta wa uzio wa nyumba.

Ronald Swai, mfanyabiashara wa duka la rejareja katika Kata ya Msaranga, amesema wakati mafuriko yanatokea mali zake zote zilikuwa dukani na baada ya kupata taarifa kwamba mafuriko yamesomba mali zake hakuamini.

“Nilikurupuka kukimbilia dukani, lakini unapita wapi kila mahali ni maji tena maji ya maana.

Nilisikia mwili mzima ukitetemeka, nikahisi kuishiwa nguvu, lakini nilijikaza kiume nifike nione na macho yangu kwamba ni kitu gani kimetokea," amesimulia Swai.

Amesema alipofika eneo lilipo duka lake hakuona kitu, alidondoka na akapoteza fahamu.

"Nilikuja kuzinduka baadaye, sikuamini macho yangu, nashindwa hata nielezeje, maumivu niliyonayo ni makali maana nimeachwa mtupu, sina chochote, mali zote zimeenda na nilikuwa na mikopo ya watu, sijui nitafanya nini mimi, sijui nitarajeshaje fedha za watu, Mungu wangu anisaidie," amesema kwa uchungu mfanyabiashara huyo.

Amina Said, mkazi wa Msaranga amesema hakuweza kuokoa chochote kilichokuwepo ndani, zikiwamo tanki nane za mahindi, fedha zilizokuwemo ndani pamoja na mali nyingine baada ya nyumba yake yote kusombwa na mafuriko.

"Ilikuwa ni saa saba za usiku nilishtuka usingizini kutokana na ngurumo kubwa ya maji maana naishi maeneo karibu kabisa na huu mto, nilitoka nje maji yalikuwa ni mengi, kabla ya hayajafika hapa nje, niliingia ndani nikawatoa wajukuu zangu ndani tukakimbia usiku ule, ndio ilikuwa salama yetu,” amesema Amina.

Hata hivyo, amesema mafuriko hayo yamevunja nyumba yake na ndani alikuwa na matanki manane ya mahindi aliyoyavuna mwaka jana yamesombwa yote.

"Sijui tutakuwa wageni wa nani, hatuna chochote, tumebaki hivi tulivyo, mwanangu naye alikuwa na saluni,  imesombwa na mafuriko na alikuwa anaendesha kwa Vicoba, sijui atakayemsaidia mwingine hapa ni nani, hapa nilipo nasumbuliwa na tatizo la shinikizo la damu, sijui hatima ya maisha yangu," amesema.


Mwenyekiti wa mtaa azungumza

Akizungumzia mafuriko hayo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Kwakomba Kata ya Mji Mpya, Jipson Tesha amesema nyumba nne zimesombwa na maji na kuna majeruhi wanne kutokana na mafuriko hayo.

"Katika mtaa huu, nyumba nne zimeanguka na vitu vyote vilivyokuwa ndani vimesombwa na maji, wananchi wameokolewa ila hawakuweza kuokoa chochote, wapo waliojeruhiwa wawili na wawili wamepata mshtuko na nyumba kadhaa zimejaa maji na vitu vimesombwa, vingine vimezama kwenye maji ndani ya nyumba za watu ambazo hazijabomoka,” amesema.

Taarifa aliyoitoa Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoani Kilimanjaro, Jeremiah Mkomagi amesema bado vifo ni saba havijaongezeka.

Kamanda Mkomagi amesema mpaka sasa mafuriko hayo yameleta madhara makubwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi na kata zilizoathirika ni Msaranga na Mji Mpya.

Amesema kaya nyingi zilizoathirika ni zile zilizokando mwa Mto Rau.

Akizungumza Leo Ijumaa Aprili 26, 2024, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema Serikali ya mkoa inaendelea kufanya tathmini ya madhara yaliyotokana na mafuriko hayo.

Amesema wote ambao nyumba zao zimeathirika wameshawapatia hifadhi katika Shule ya Sekondari Lucy Lamecky.

"Wale wote ambao nyumba zao zimeanguka na kuharibiwa na mafuriko tumewapa hifadhi ya muda pale Shule ya Sekondari Lucy Lamecky, tayari nimemwagiza mkurugenzi na mkuu wa wilaya, tunaendelea kuwahudumia kwa kipindi hiki ambacho tunafanya utaratibu mwingine,” amesema Babu.

Amesema miili minne ambayo ni ya familia moja imeshatambuliwa na mitatu bado haijatambulika.

Hata hivyo, Babu amesema mwili mmoja umeharibika sana.

"Tayari Kamanda wa Polisi mkoa ameshatoa taarifa kama kuna mtu atakuwa hajamuona ndugu yake kwa muda atoe taarifa maana miili ipo Hospitali ya Mawenzi,” amesema mkuu huyo wa mkoa.