SMZ, kampuni ya Thailand zinavyovutana malipo ya mchele

Muktasari:

  • SMZ inapinga hukumu ya kuilipa Kampuni ya Laemthong Rice Limited ya nchini Thailand, Dola za Marekani 69.04 milioni (zaidi ya Sh165.1 bilioni kwa sasa).

Dar es Salaam. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imepata nafasi nyingine ya kupinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyoiamuru kulipa mabilioni ya fedha kutokana na ununuzi wa mchele kutoka Thailand.

Mahakama ya Rufani imekubali maombi ya Mwanasheria Mkuu wa SMZ kuruhusiwa kufungua shauri la maombi ya mapitio kupinga hukumu nje ya muda.

Inapinga Hukumu ya Mahakama Kuu ya Zanzibar iliyoiamuru kuilipa Kampuni ya Laemthong Rice Company Limited ya nchini Thailand, Dola za Marekani 69.04 milioni (zaidi ya Sh165.1 bilioni kwa sasa).

Katika hukumu iliyotolewa na Jaji Dourado, Mei 16, 1997, Mahakama Kuu ya Zanzibar, iliiamuru SMZ kuilipa kampuni hiyo fedha hizo zikiwa ni malipo ya deni la msingi la mchele ulioagizwa na SMZ kutoka kwa kampuni hiyo kati ya mwaka 1986 mpaka 1988, pamoja na riba ya asilimia 25.

Mwaka 2023 ikiwa ni miaka 26 baada ya hukumu kutolewa, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) alifungua shauri la maombi Mahakama ya Rufani akiomba kuongezewa muda wa kufungua shauri la maombi ya mapitio kupinga hukumu hiyo.

AG Zanzibar alifungua shauri hilo namba 729/15 la mwaka 2023 dhidi ya kampuni hiyo ikiwa mjibu maombi wa kwanza, na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Zanzibar, akiwa mjibu maombi wa pili.

Mahakama katika uamuzi uliotolewa na Jaji Rehema Kerefu, Jumatatu Mei 6, 2024 imekubali ombi la AG akimpa siku 60 tangu tarehe ya uamuzi huo awe amefungua shauri la mapitio ya hukumu hiyo.

“Kwa vigezo hivyo, ninaona kuna hoja katika shauri la maombi na linakubaliwa,” amesema Jaji Kerefu katika uamuzi baada ya kujadili hoja za pande zote na kuamuru:

“Mwombaji anapaswa kufungua shauri la maombi linalokusudiwa ndani ya siku 60 kutoka siku ya kutolewa uamuzi huu. Kwa kuzingatia mazingira ya shauri hili, sitoi amri kuhusu gharama (za kuendesha shauri hilo)”


Historia ya mgogoro

Mwaka 1985, Wizara ya Biashara ya Serikali ya Thailand na Wizara ya Biashara ya SMZ ziliingia mkataba wa kuuziana mchele.

Kuanzia mwaka 1986 mpaka 1988 Kampuni ya Laemthong ilipeleka kwa SMZ tani 39,900 za mchele wenye thamani ya Dola 12.98 milioni za Marekani, lakini inadaiwa SMZ ilikiuka mkataba kwa kushindwa kulipia bidhaa hiyo.

Mwaka 1997, kampuni hiyo ilifungua kesi namba 4 ya mwaka 1997 Mahakama Kuu ya Zanzibar, dhidi ya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ya Zanzibar.

Kampuni ilidai ilipwe Dola 69.04 milioni za Marekani zikiwa ni gharama za bidhaa iliyopeleka kwa wizara hiyo kati ya mwaka 1986 na 1988.

Pia, iliomba ilipwe riba ya asilimia 25 ya kiasi hicho kwa mwaka kuanzia Januari Mosi, 1997 mpaka kukamilika kwa malipo yote na gharama za kesi.

Mahakama ilisikiliza na kuamua kesi hiyo upande mmoja (wa mdai, kampuni ya Laemthong) na kuiamuru SMZ kupitia Katibu Mkuu Wizara ya Fedha kuilipa kiasi hicho cha fedha.

Kutokana na hukumu hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha alifungua shauri la maombi namba 2 la mwaka 1997 akiomba Mahakama itengue hukumu hiyo.

Mahakama katika uamuzi ilirejea tuzo ya awali na kuibadilisha kutoka Dola 69 milioni za Marekani na kuwa Dola 15.5 milioni.

Kampuni hiyo ilikata rufaa namba 91 ya mwaka 1998 Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi huo. Mahakama iliutengua na ikaelekeza tuzo ya awali ya Dola 69 milioni za Marekani itekelezwe.

Mwaka 2017 kampuni hiyo katika kutekeleza hukumu ilikusudia kukamata na kuuza mali za SMZ. Hivyo, ilipeleka kwa Msajili maombi ya utekelezaji.

Msajili alitoa hati ya Dola za 5.7 milioni za Marekani kuwa ndiyo kiasi inachostahili kulipwa badala ya Dola 69 milioni za Marekani.

Kampuni ilipinga uamuzi huo Mahakama Kuu kupitia shauri la maombi ya mapitio namba 50 la mwaka 2017. Mahakama Kuu ikaunga mkono uamuzi wa msajili.

Kampuni ilikata rufaa namba 259 ya mwaka 2019, Mahakama ya Rufani, kupinga uamuzi huo.

Mahakama katika hukumu ya Novemba 9, 2022 ilitengua uamuzi wa Msajili na kurejea hukumu na tuzo iliyotolewa awali na Mahakama Kuu ya Dola 69 milioni.

Kutokana na uamuzi huo, mwaka 2023 Mwanasheria Mkuu wa Serikali alifungua shauri la maombi akiomba aruhusiwe kufungua shauri la maombi ya mapitio dhidi ya hukumu ya awali ya Mahakama Kuu.

AG anadai hukumu hiyo imegubikwa na kasoro za kisheria zinazohitaji kushughulikiwa kwa njia ya shauri la mapitio akibainisha kasoro saba.

Kampuni ilipinga shauri hilo ikidai mkataba unaodaiwa haujaonyeshwa kwenye hati ya madai na kwenye uamuzi unaopingwa, basi hauwezi kutumiwa na Mahakama kukosoa uamuzi wa Mahakama ya awali.

Inadai kasoro zinazodaiwa, kama zipo haziko dhahiri katika uso wa kumbukumbu, bali zinahitaji mjadala na mchakato mrefu wa kuzibainisha, kinyume cha kanuni zilizowekwa kisheria.

Ilidai utekelezaji wa tuzo ya Dola 69 milioni za Marekani na riba ya asilimia 25 ulishakatiwa rufaa katika Mahakama hiyo bila mafanikio, hivyo ikaomba Mahakama itupilie mbali maombi ya AG kwa kutokuwa na mashiko.

Wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, mwombaji (AG) aliwakilishwa na mawakili wa Serikali wakuu Ali Ali Hassan na Said Salum Said ambao walifafanua kasoro za kisheria zinazodaiwa katika hukumu hiyo.

Laemthong iliwakilishwa na wakili Juma Nassoro, huku mjibu maombi wa pili, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha akiwakilishwa na Wakili Hussein Migoda Mataka.

Kuhusu kasoro za kisheria katika hukumu inayobishaniwa, wakili Hassan alidai kifungu cha 12 cha mkataba baina ya pande hizo kinaeleza mgogoro baina yao utatatuliwa kwa njia ya usuluhishi, hivyo jaji hakuwa na mamlaka kusikiliza na kuamua kesi hiyo.

Alidai kesi ya msingi ilifunguliwa takribani miaka 14 baada ya mgogoro kuibuka kinyume cha Sheria za Zanzibar zinazoelekeza kesi za madai ya namna hiyo zinapaswa kufunguliwa ndani ya miaka mitatu.

Wakili Hassan alidai Jaji hakuzingatia kanuni ya uthibitisho wa madai, akidai aliamua kesi kwa kusikiliza hoja za wakili wa mdai pekee bila kumtaka mwenyewe kuthibitisha madai yake, kinyume cha matakwa ya Sheria ya Ushahidi ya Zanzibar.

Wakili Nassoro alidai mwombaji ameshindwa kuonyesha sababu thabiti za kuongezewa muda wa kufungua shauri la mapitio na kwamba, sababu zilizotolewa si miongoni mwa sababu za kuongezewa muda.

Alidai kasoro zilizodaiwa katika hukumu inayopingwa hazina sifa ya kustahili kuongezewa muda kufungua shauri la mapitio, kwa kuwa si hoja za kisheria bali za kiushahidi.

Alidai ingawa AG hakuwa sehemu ya kesi ya msingi na hana haki ya rufaa ya moja kwa moja, lakini alishindwa kuonyesha namna gani masilahi yake yaliathirika katika hukumu hiyo.

Alidai kwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha alishaikatia rufaa hukumu hiyo mara mbili, 1998 na 2019, basi AG hawezi kuruhusiwa kuingia kwenye hukumu kwa mlango wa nyuma.

Jaji Kerefu amesema kwa kutambua ukweli kwamba katika hatua hii hapaswi kuchimba sana na kuhitaji mwombaji kuweka wazi zaidi kuhusu kasoro zilizoainishwa, anaona kuna sababu ya kustahili kukubali maombi hayo.

Jaji Kerefu amesema kama mwombaji (AG) akipewa nafasi anaweza kufafanua zaidi kasoro zinazodaiwa na kutatoa fursa kwa wadaiwa wote wanaohusika kusikilizwa kikamilifu kuhusu kasoro za kisheria zinazodaiwa katika hukumu hiyo.