Songwe waomba barabara ya njia nne

Muktasari:

  • Wakazi wa Mkoa wa Songwe wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kusaidia ujenzi wa barabara ya njia nne kuanzia Mlowo hadi Tunduma ili kuondokana na adha ya foleni ndefu ya malori yanayokwenda nchi za Kusini mwa Afrika kupitia Tunduma.

Songwe. Wakazi wa Mkoa wa Songwe wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kusaidia ujenzi wa barabara ya njia nne kuanzia Mlowo hadi Tunduma ili kuondokana na adha ya foleni ndefu ya malori yanayokwenda nchi za Kusini mwa Afrika kupitia Tunduma.

Aidha wameshauri usafiri wa reli ya Tazara kutumika ili kuepuka adha hiyo inayodhorotesha uchumi wa wananchi walioko mpakani mwa Tanzania na Zambia na maeneo ya jirani.

Wametoa maombi hayo leo Februari 24, 2022 kufuatia foleni yenye urefu wa karibu kilometa 13 ikihusisha malori kwa siku ya sita sasa kati ya Vwawa na Tunduma.

Mkazi wa Isangu, mjini Vwawa, Aron Mwashitete amesema usafiri  wa Tazara ukitumika utapunguza  malori ambayo yamekuwa kikwazo kwa biashara kati ya Tunduma na miji ya Vwawa, Mlowo na Mbeya na mikoa mingine ya karibu ikiwemo Iringa na Njombe.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Omary Mgumba amesema Ili kuondoa foleni na hasara za kiuchumi Kwa wananchi ipo haja ya kutengenezwa kwa barabara ya njia nne kutoka Mlowo kwenda Tunduma.

Amesema hayo kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kuwa kwa sasa njia pekee ya kupata ufumbuzi wa kudumu ni kujenga njia nne itakayoweza kuhimili magari hayo na kutoa fursa kwa shughuli nyingine kuendelea .

Kwa upande wake Meneja wa Tazara  wilaya ya Mbeya ,Timothy Andambike akizungumza katika kikao cha kamati ya ushauri cha mkoa Songwe amesema licha ya kukabiliwa na uhaba wa mabehewa lakini wameweza kumudu kusafirisha baadhi ya mizigo na kuifikisha inakohitajika bila shida.