Taasisi tisa za elimu kufumuliwa, shule mpya 100 kujengwa Tanzania

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, akizungumza bungeni jijini Dodoma, leo Mei 07,2024.

Muktasari:

  •  Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inakusudia kuzifanyia marekebisho sheria tisa za taasisi tisa za elimu ikiwemo Baraza la Mitihani Tanzania ((Necta).

Dodoma. Serikali imesema itajenga shule mpya 100 za sekondari za amali nchi nzima, kuzifumua taasisi tisa za elimu na imefanya marekebisho ya sheria ya Bodi ya Mikopo kwa lengo la kuongeza ufanishi.

Hayo yamo kwenye taarifa ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2024/2025 yaliyowasilishwa bungeni leo Jumanne, Mei 7, 2024 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda.

Wizara hiyo imeliomba Bunge kuidhinisha Sh1.9 trilioni kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ambapo Sh637.2 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh1.3 trilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Profesa Mkenda amesema kwa mwaka huu wa fedha wizara yake imekuja na vipaumbele vitano kama ilivyokuwa kwa mwaka wa fedha unaomalizika.

Amesema kwa mwaka huu wizara itafanya mapitio ya taasisi zake tisa za Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), iliyoanzishwa kutokana na sheria namba 7 ya mwaka 1986 na ilirasimishwa rasmi mwaka 1988 kama mrithi wa Baraza la Taifa la Utafiti.

Taasisi nyingine itakayofanyiwa mapitio ya sheria ni Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB) iliyoanzishwa kwa Sheria ya Bunge Namba 39 ya mwaka 1963 ikijulikana kama Bodi ya Huduma za Maktaba Tanganyika.

Kwa mujibu wa Profesa Mkenda taasisi nyingine ni Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) iliyoanzishwa Novemba 1973.

Kabla ya wakati huo, Baraza la Mitihani la Afrika Mashariki (EAEC) lilisimamia Tanzania Bara na Zanzibar. Baraza la pili lilijiondoa kutoka (EAEC) mwaka 1970. Serikali ya Tanzania ilianza kuajiri watumishi wa Necta mwaka 1971, na Sheria ya Bunge namba 21 ya mwaka 1973 ilianzisha Necta.

Ameitaja taasisi nyingine itakayofumuliwa ni Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) iliyoanzishwa kwa sheria ya Bunge Na.1 ya 1994 na kupewa majukumu ya kuratibu kusimamia, kutoa, kuendeleza na kugharamia elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini.

Sheria hiyo pia ilianzisha Bodi ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) ambayo inawajibika katika utendaji na uendeshaji wa shughuli za mamlaka.

Taasisi nyingine itakayofumuliwa ni Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) iliyoanzishwa Julai 1, 2005.

Pia, alizitaja Baraza la Taifa la Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Nactvet), Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).

“Vilevile, itafanya marekebisho ya sheria ya Bodi ya Mikopo kwa lengo la kuongeza ufanisi wake ikiwemo kurahisisha ufunguaji wa mashauri na utekelezaji wake,” amesema.

Pia, Profesa Mkenda amesema Serikali katika mwaka ujao wa fedha itajenga shule mpya 100 za sekondari za amali za uhandisi kujengwa nchini. 26 kati ya hizo zitaanza kupokea wanafunzi kuanzia Januari 2025.

Akizungumzia utekelezaji wa bajeti ijayo amesema wizara imepanga kutekeleza vipaumbele vitano vyenye lengo la kuongeza ubora wa elimu kwa kuwezesha vijana wa Kitanzania kupata maarifa, ujuzi, kujiamini, kujiajiri na kuajirika.

Vilevile, vipaumbele vyenye kujielekeza katika kutegemeza tafiti, sayansi, teknolojia na ubunifu katika agenda ya maendeleo ya nchi.

Amevitaja vipaumbele vya Wizara kwa mwaka wa fedha 2024/25 ni kuendelea na utekelezaji wa sera na mitaala, mapitio ya sheria na kuandaa miongozo ya utoaji elimu na mafunzo nchini, kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi (amali na amali sanifu).

Vipaumbele vingine ni kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya msingi, sekondari na ualimu, kuimarisha ubora wa elimu ya juu na kuendeleza tafiti, matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu.

“Serikali itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Toleo la 2023 na Mitaala kwa ngazi ya Elimu ya Msingi, Sekondari na Ualimu.

“Aidha, itaendelea na uandaaji wa zana za utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Toleo la 2023 ambazo ni Miongozo, Mfumo wa Kitaifa wa Tuzo na Sifa Linganifu (Tanzania Qualification Framework – TQF), Sheria na Kanuni.”

“Mfumo wa mtaala wa kitaifa na mfumo wa tathmini wa kitaifa katika ngazi ya elimu ya msingi, sekondari, ualimu, elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi na elimu ya juu kwa lengo la kuwezesha ufanisi katika utekelezaji wa sera,” amesema.

Amesema Serikali itaendelea na maboresho ya mitaala ya elimu ya amali sanifu na elimu ya juu ili kuwezesha nchi kuandaa rasilimali watu yenye ujuzi na maarifa.

“Katika kufikia azma hiyo, Serikali itafanya mapitio ya mitaala 171, kuandaa mitaala mipya 18, kuanzisha programu za vipaumbele 145 pamoja na matumizi ya mbinu bunifu za ufundishaji katika elimu ya juu.

“Aidha, itawezesha ziara za kimkakati kwa wafanyakazi wa sekta ya elimu katika nchi zenye uzoefu wa uandaaji wa rasilimali watu yenye maarifa na ujuzi wenye kuchangia katika ukuaji wa kati wa uchumi,” amesema.

Waziri huyo amesema: “Tutaandaa mtaala mpya katika taasisi 17 za elimu ya juu na itahakiki mitaala 230 ya vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi. Lengo ni kuhakikisha kuwa mafunzo yanayotolewa yanakidhi mipango ya nchi, soko la ajira la kitaifa na kimataifa na kuwawezesha wahitimu kujiajiri na kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira.”

Amesema pia Serikali itaendelea kuhuisha miongozo mbalimbali ya utoaji elimu na mafunzo nchini ili kuendana na maboresho ya Mitaala na Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Toleo la 2023.

Profesa Mkenda amesema Serikali itakamilisha mwongozo wa kuwatambua na kuwaendeleza wanafunzi wenye vipawa na itaandaa mwongozo wa elimu jumuishi wa ufundishaji na matumizi ya teknolojia, kwa lengo la kuongeza ufanisi katika ufundishaji na matumizi ya teknolojia katika elimu na mafunzo.