Takukuru: Wananchi msiogope, toeni taarifa mtalindwa

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa mkoa wa Songwe, Edings Mwakambonja

Songwe. Mkuu wa Taasisi ya Kuzuai na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Songwe, Edings Mwakambonja amesema kuwa programu ya Takukuru Rafiki imesaidia kutoa hofu na mtazamo wa jamii kuhusiana na taasisi hiyo huku akiwataka wananchi wasiogope kutoa taarifa za rushwa kwa kuwa watalindwa.

Amesema kuwa Takukuru Rafiki imesaidia kuwaweka karibu wananchi na taasisi hiyo kutokana na elimu wanayoitoa ambayo imesaidia wananchi kuondoa hofu na mtazamo waliokuwa nao awali.

Akitoa taarifa ya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo kwa kipindi cha mwezi Aprili hadi Juni mwaka huu kwa waandishi wa habari leo Alhamisi Agosti 3, 2023, Mkuu huyo wa Takukuru Mkoa wa Songwe amesema kuwa pamoja na ufuatiliaji wa utekulezaji wa miradi ya maendeleo lakini wamefanikiwa kufikia na kutoa elimu katika kata 15 katika programu ya Takukuru Rafiki.

“Katika kipindi cha Aprili mpaka Juni tumefanikiwa kufika katika kata 15 kutoa elimu na kusikiliza kero za wananchi. Kero 84 zilitolewa na kati ya hizo kero 41 zilishatatuliwa na zilizobaki zinaendelea kushughulikiwa” amesema Mwakambonja na kuongeza;

“Kweli wananchi walikuwa na hofu wakisikia Takukuru lakini kutokana na elimu tunayotoa kwa jamii, wananchi wameelewa na wanakuwa rafiki. Kuhusu kuwalinda wanaotoa taarifa za rushwa kuna sharia za kuwalinda hivyo wananchi wasiogope watupe taarifa” amesisitiza Mwakambonja huku akitoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano wanapobaini kuna viashiria vya rushwa katika maeneo yao.

Ili kuendelea kuzuia rushwa katika jamii, Mwakambonja amesema taasisi hiyo ipo kwenye utekelezaji wa kutoa elimu kupitia Takukuru Rafiki katika kata zote 94 za mkoa wa Songwe ambapo mpango huo ni endelevu.



 Miradi saba yabainika kuwa na mapungufu

Akizungumzia kuhusu miradi ya maendeleo, Mwakambonja amesema Taasisi hiyo imefuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo 10 katika kipindi cha Aprili hadi Juni mwaka huu yenye thamani ya Sh3.8 bilioni ambapo kati ya miradi hiyo, miradi saba ilibainika kuwa na mapungufu.

“Jumla ya miradi 10 ilifuatiliwa. Katika ufuatiliaji wa miradi uliofanyika, miradi saba yenye thamani ya Sh1.7 bilioni ilibainika kuwa na mapungufu ya kiufundi ambayo maofisa wetu waliyatolea ushauri wa kurekebisha” amebainisha.


Mwakamboja ameitaja miradi iliyobainika kuwa na mapungufu kuwa ni pamoja na mradi wa ujenzi wa nyumba mbili za walimu Shule ya Sekondari Mpande Halmashauri ya Mji Tunduma, Ujenzi wa nyumba ya mwalimu Shula ya Msingi Machinjioni Halmashauri ya Mji Tunduma, Ujenzi wa Kituo cha Afya Hezya na Ujenzi wa jengo la wagonjwa mahututi (ICU) katika Hospitali ya Wilaya ya Itumba Halmashauri ya Wilaya ya Ileje.

Miradi mingine ambayo Mwakambonja ameitaja kuwa ilibainika na mapungufu ni pamoja na ujenzi wa jengo la maabara katika Hospitali ya Itumba-Ileje, ujenzi wa wodi 3 hospitali ya Ileje na Ujenzi wa jingo la mionzi katika Hospitali ya Wilaya ya Ileje.

Mkuu huyo wa Takukuru Mkoa wa Songwe amesema kuwa maofisa wa taasisi hiyo walitoa ushauri wa kufanyika marekebisho kwa wakurugenzi watendaji wa halmashauri husika.



 Yashinda kesi nne

Akizungumzia juu ya uchunguzi na mashtaka katika kipindi hicho cha miezi mitatu, Mkuu huyo wa Takukuru Mkoa wa Songwe amesema kuwa kati ya kesi mpya 14 zilizofunguliwa mahakamani kesi nne zimeamuliwa na kesi zote nne washtakiwa walitiwa hatiani.

Amesema kuwa taasisi hiyo ilipokea malalamiko 33 ambapo 23 yalikuwa yanahusu rushwa huku 10 yakiwa hayahusu rushwa katika kipindi cha miezi mitatu.

“Kesi mpya 14 zilifunguliwa mahakamani ambapo kesi 10 zinaendelea na kesi nne ziliamuliwa. Kesi zote nne washtakiwa walitiwa hatiani na kurejesha fedha” amebainisha