Tamasha la Kitaifa la Utamaduni kufanyika Songea

Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nicholas Mkapa (kushoto) na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Drum Beats Carnival (T) Limited, Selestine Mwesigwa wakisaini mkataba wa ushirikiano kuhusu uendeshaji wa Tamasha la Kitaifa la Utamaduni katika ofisi za wizara hiyo, Mtumba jijini Dodoma. Wengine kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria wa wizara hiyo, Lugano Rwetaka na Mratibu Aggrey Marealle.

Muktasari:


  •  Miongoni mwa mambo yatakayokuwapo kwenye tamasha hilo ni vyakula vya Kitanzania, zana, mavazi na maonyesho barabarani.

Dodoma. Watanzania wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika Tamasha la Kitaifa la Utamaduni kuanzia hatua za awali hadi ngazi ya kitaifa ili kuimarisha utamaduni ulipo nchini.
Tamasha hilo linalotarajiwa kuanza Agosti 25 hadi 28 mwaka huu Songea mkoani wa Ruvuma, linafanyika kwa ushirikiano wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na Kampuni ya Drum Beats Carnival (T) Limited ya jijini Dar es Salaam.
Makubaliano ya ushirikiano huo yamesainiwa  wizarani jijini Dodoma Jumatatu Machi 25 2024 kati ya Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Nicholas Mkapa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Drum Beats Carnival (T) Limited Selestine Mwesigwa pamoja na viongozi waandamizi kutoka pande zote mbili.
Akizungumza baada ya utiaji saini, Mkapa amesema wizara ina matarajio makubwa kutoka kwa Drum Beats katika kuendesha tamasha hilo la kitamaduni hapa nchini.
Mkapa amesema huo ni mwanzo mzuri wa kushirikiana na sekta binafsi katika kuendesha matamasha ya wizara hiyo pamoja na kupanua wigo kwa wadau wa sekta binafsi kushiriki kikamilifu kuendesha matukio ya kijamii.
“Hii haina maana kuwa, Serikali imeliachia tamasha hili moja kwa moja bali tunatoa fursa kwa sekta binafsi itoe mchango wake, pia kuhakikisha tamasha hili linafanyika kitaalamu zaidi na linakuwa kubwa lakini Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu,” amesema.
Mkapa ametoa wito kwa Watanzania kujitokeza katika hatua zote za tamasha hilo linalolenga kuimarisha utamaduni wa Tanzania.
Mkurugenzi wa utamaduni wa wizara hiyo,  Dk Mnata Resani amesema tamasha hilo litafanyika Songea mkoani Ruvuma huku akisisitiza kuwa, Drum Beats kushirikiana na wizara ni dalili ya tukio hilo kuwa katika viwango vya juu zaidi.
“Kutakuwa na mambo mbalimbali kama vyakula vya Kitanzania, zana mbalimbali, mavazi na maonyesho barabarani yaani street carnival,” amesema Dk Resani. 
Mwesigwa  ambaye ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Drum Beats, amesema kampuni  hiyo ipo tayari kushirikiana na wizara kuhakikisha tamasha hilo linafanikiwa.
“Timu yetu imekamilika na tuko tayari kushirikiana na wizara kuhakikisha malengo yanafikiwa na pengine yanavukwa,” amesema Mwesigwa.
Pia, amesema baada ya utiaji saini, kampuni yake itatoa ratiba nzima ya shughuli zote za tamasha hilo. 
“Tunatoa wito kwa Watanzania watuunge mkono ili kufanikisha jambo hili,” amesema Mwesigwa.