Tanzania kunufaika ujio wa kampuni 60 kutoka China

Mwenyekiti wa Kampuni ya Group 6 na Kongani ya Viwanda ya Sino-Tan iliyoko mkoani Pwani, Janson Huang akizungumza na waandishi wa habari jana  jijini Dar es Salaam, kushoto kwake ni  Ofisa Uwekezaji kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Diana Mwamanga.

Muktasari:

  • Kongamano la wafanyabiashara na wawekezaji kati ya Tanzania na China linatarajiwa kufanyika Machi 27, 2024 jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Wafanyabiashara na wawekezaji kutoka kampuni 60 za China wanatarajia kuungana na wenzao 120 nchini katika kongamano la kibiashara linalotarajiwa kuwa na manufaa makubwa kwa Tanzania.

Kongamano hilo litafanyika nchini Machi 27, 2024 na kuzungumzia uwekezaji katika sekta mbalimbali ikiwemo ya madini, viwanda, kilimo, afya na nishati.

Ofisa Uwekezaji katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Diana Mwamanga amesema fursa hiyo itaongeza chachu ya uwekezaji na biashara kwa Watanzania.

"TIC tumeona faida ya makongamano haya ya kibiashara na uwekezaji kwa kampuni za hapa nchini na zipo zilizowekeza kupitia makongamano ya namna hii," amesema Mwamanga alipozungumza na wanahabari leo Machi 20, 2024.

Mwamanga ambaye ni msimamizi wa dawati la China, amesema TIC imeona hiyo ni fursa kubwa kwa kampuni za Kitanzania kupata ubia kutoka China ili kurahisisha upatikanaji wa soko za bidhaa zao nchini humo.

Ameongeza kuwa hiyo ni sehemu ya kuitangaza nchi, hivyo ushiriki wa Watanzania katika kongamano hilo ni muhimu kwa kuwa China kwa sasa ni Taifa linaloongoza kwa uwekezaji nchini.

"Kwa hapa Afrika Mashariki wawekezaji wengi wanaitazama sana Tanzania kutokana vivutio vya  uwekezaji, amani na utulivu hivyo  kampuni hizo 60 zote zina taarifa na Tanzania na zinakuja kuangalia ili kufanya uamuzi kwa ajili ya hatua inayofuata," amebainisha.

Kwa upande wake, meneja maendeleo ya wanachama wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Kelvin Ogodo amesema kampuni hizo zinakuja kuangalia fursa za uwekezaji sambamba na bidhaa za Kitanzania watakazoziingiza nchini mwao.

"Kadhalika, wataangalia bidhaa zilizopo nchini  ambazo tutazipeleka China hususani za madini na mazao ya kilimo yanayohitajika," amesema.

Ogodo ambaye amewawakilisha Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) na Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), ameitaka jumuiya ya wafanyabiashara nchini kushiriki kwa wingi ili kupata fursa hiyo ambayo ina faida katika uchumi wa nchi.

Mwenyekiti wa Kampuni ya Group 6 na Kongani ya Viwanda ya Sino-Tan iliyoko mkoani Pwani, Janson Huang amesema dhumuni lao ni kuwavutia wawekezaji wa China kuja Tanzania.

Amesema uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na watu wa China unazidi kuimarika siku hadi siku na sasa unatimiza miaka 60, hivyo katika kongamano hilo yatasainiwa makubaliano ya uhamasishaji ushirikiano wa kibiashara.

Kongani hiyo (mtaa wa wiwanda) ya Sino-Tan ya Kibaha ambayo ni uwekezaji China, inatarajiwa kutoa ajira takribani 600,000 kwa Watanzania katika kuzalisha bidhaa mbalimbali.

Kongani hiyo itakayokamilika mwaka 2027, itakuwa na viwanda vikubwa, vya kati na vidogo, itatoa ajira hizo huku ikiongeza thamani ya Tanzania katika ushindani wa kibiashara Afrika Mashariki na duniani kwa ujumla.