Tawa yatoa tahadhari wanaofukuza wanyamapori

Morogoro. Mmalaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imeagiza kutoshirikishwa kwa wazee, wajawazito, watoto na wale waliotumia vilevi kwenye matukio ya kuwafukuza wanyamapori na waharibifu katika maeneo yao hususani Tembo.

Kaimu naibu kamishna wa Uhifadhi wa TAWA Mlage Kabange ametoa maagizo hayo leo Mei 19, 2023 wakati wa warsha ya kujadili utatuzi wa changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu inayoikabili wilaya ya Mvomero.

Kabange amewataka wananchi kuacha tabia ya mazoea ya kutembea usiku na alfajiri ili kuepuka kukutana na wanyamapori hao ambao mara nyingi wamekuwa na tabia ya kutembea nyakati hizo.

"Ni muhimu wananchi wakaacha tabia ya kufanya shughuli za kibinadamu maeneo ya karibu na hifadhi Kwani hatari kwenu," amesema.

Naye mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Judith Nguli akizungumza katika warsha hiyo amesema uwepo wa wanyamapori wakali na waharibifu kwenye maeneo ya vijiji vinavyopakana na hifadhi kumesababisha kuongezeka kwa changamoto ya uharibifu wa mazao, mashamba na makazi ikiwa ni pamoja na kutoelewana  mwanadamu na wanyama.

Nguli amepiga marufuku wananchi wilayani humo, kuacha tabia ya kuchokoza wanyamapori ikiwemo tembo hali ambayo inasababisha kuwatia hasira na hivyo kuwafanya kujeruhi binadamu na hata kuwasababishia vifo.

"Ni lazima tuwaambie ukweli wananchi, wapo baadhi wanawachokoza kwa makusudi, wanawajeruhi, ukimjeruhi tembo anapata hasira hivyo ni lazima afanye vurugu kutokana na kumpandisha hasira," amesema.

Aidha amesema wapo wananchi ambao wamekuwa wakilima katikati ya mapori peke yao hali ambayo inahatarisha maisha yao nanhata mazao wanayolima.

"Shughuli za kibinadamu zikifanywa jirani na hifadhi ni lazima uwe na njia za kudhibiti wanyama wasifanye uharibifu, vinginevyo wakitoka nje ya hifadhi lazima wafanye uharibifu, amesema.

Pia mkuu huyo wa wilaya hiyo aliwatahadharisha wananchi wenye tabia ya kupanda juu ya miti na kuwinda wanyamapori kwa kutumia silaha zisizo na uwezo na hivyo kuishia kuwajeruhi wanyama na kusababisha athari kwa binadamu.

Naye mbunge wa Mvomero, Jonas Van Zeland ameziomba mamlaka zinazohusika na wanyama pori ikiwemo Tawa kuwavuna tembo kwa lengo la kuwapunguza ili kuwapunguzia wananchi adha wanayokumbana nayo.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM, Teophil Jaka amesema ipo haja ya mamlaka hizo kuwaandaa vijana katika vijiji husika ili wawe walinzi katika maeneo hayo.