TBS: Ubora ‘energy drinks’, pombe kali si tatizo bali kiasi cha unywaji

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Dk Athuman Ngenya

Muktasari:

  • Wananchi wametakiwa kutumia vinywaji kwa kipimo na baada ya kusoma maelekezo ya matumizi na endapo kutakuwa na changamoto watoe taarifa katika Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili zifanyiwe kazi.

Dar es Salaam. Matumizi kupita kiasi kwa wanywaji wa vinywaji vikali na vile vya kuongeza nguvu, yametajwa kuwa sababu ya madhara ya kiafya kwa watumiaji na si ubora wa vinywaji husika.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Aprili 15, 2024, Mkurugenzi wa udhibiti ubora wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Lazaro Msasalaga amesema wananchi wamekuwa na tabia ya kunywa kupita kiasi na bila kuangalia vipimo, huku wengine wakitumia vinywaji hivyo kwa wingi bila kula.

"Zipo bidhaa feki, lakini watu wengine wanakunywa zaidi ya viwango husika, unakuta hajui ni kiasi gani cha pombe au kinywaji cha kuongeza nguvu anywe, vikimzidi analalamika kuwa bidhaa hiyo ni feki," amesema Msasalaga katika mkutano huo na wanahabari, ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Amesema watu hawatakiwi kukimbilia kusema hii bidhaa feki na kuzua taharuki hususani katika mitandao ya kijamii, wakati hawafuatilii kilichoelekezwa.

Amesema unakuta wanywaji wengine wanataka kumaliza chupa ya pombe kali au idadi kubwa ya z 'energy drinks' kwa wakati mmoja bila kuzingatia maelekezo ya matumizi. 

“Tatizo si viwango (vya ubora), ni kiasi mtu anachokunywa, yaani tunasema ni abuse of product (matumizi mabaya ya bidhaa). Mwingine anakuwa ameshakunywa amelewa, akija rafiki yake anamwongezea, naye anaendelea, mwisho wake figo inazidiwa na kupata madhara,” amesema.

Hivyo, Msasalaga amesema udhibiti unafanyika inavyotakiwa lakini watumiaji ndiyo wanatakiwa kufuata maelekezo yanayotolewa kwenye vinywaji ili kuepuka madhara ya kiafya.

"Wapo watu wanakunywa zaidi ya kiwango kilichowekwa na wengine wanakunywa bila kula, hivyo wanajikuta wanaathirika na  ‘cafein’, lakini wangefuata maelekezo ya matumizi ya kinywaji husika wasingepata madhara,”amesema.

Hata hivyo, amesema hiyo haina maana kwamba hakuna bidhaa bandia, suala ambalo wananchi watakiwa kulishughulikia kwa kutoa taarifa za kuzibainisha,  TBS itafanyia kazi haraka na kutoa mrejesho kwa mtoa taarifa.

Kuhusu hilo, amesema tatizo jingine la wanywaji ni pale anapoona ladha ya kinywaji alichozoea imebadilika, lakini yeye anaendelea kukinywa badala ya kutoa taarifa TBS ili bidhaa husika ikaguliwe, mwishowe anapa madhara.

Amesema vinywaji vilivyopo katika soko vimepitiwa na TBS hivyo vipo salama kwenye matumizi, muhimu ni kuzingatiwa matumizi sahihi.

Vilevile, amesema maofisa wa shirika wamekuwa wanapita kufanya ukaguzi na kubaini bidhaa zisizokuwa na ubora, na ndani ya miaka mitatu wameteketeza bidhaa za Sh6 bilioni.

Msasalaga alikuwa anajibu maswali yaliyoibuliwa na wahariri kutokana na kilio cha kuwepo kwa pombe kali na vinywaji vya kuongeza nguvu  ‘energy drinks’ vinavyolalamikiwa.

Baada ya maswali hayo na msisitizo uliowekwa na wahariri hao, Msasalaga amesema “Tunao wajibu wa kufanya ‘food risk assessment’ ili tuweze kupata namna bora ya matumizi ya vinywaji hivyo.”

Tatizo la vinywaji vikali na vya kuongeza nguvu limekuwa likizungumziwa na wataalamu wa afya, wakionya matumizi yake kwa wingi kuwa vinaathiri afya ya figo na moyo.

Aprili 25, mwaka huu, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu aliiagiza  Taasisi ya Magonjwa ya Binadamu  (NIMR) ifanye utafiti zaidi kuhusu matumizi ya ‘energy drinks’ na kutoa ushahidi wa kisayansi kuhusu madhara yake.

Mapema akiwasilisha ripoti ya utendaji ya TBS ndani ya miaka mitatu, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk Athuman Ngenya alisema Serikali imekuwa ikitenga zaidi ya  Sh250 milioni kwa ajili ya kupitisha viwango vya bidhaa za wajasiriamali wadogo bila malipo yoyote.

Amesema katika kipindi cha miaka mitatu jumla ya leseni za ubora wa bidhaa 2,106 zilitolewa kwa wazalishaji mbalimbali nchini sawa na asilimia 105.3, lengo likiwa kutoa leseni 2,000 na kati ya leseni hizo zilitolewa bure kwa wajasiriamali wadogo 1,051.

Pia, amesema wamekuwa na mfumo na utaratibu wa udhibiti ubora wa bidhaa zinazoingizwa nchini kuanzia huko nje na pia kufanya ukaguzi pindi zinapowasili nchini.

"Tunafanya ukaguzi mara kwa mara sokoni na viwandani na hata kwenye mipaka ya nchi, kuhakikisha bidhaa zilizopo zinakidhi matakwa ya viwango husika," amesema Dk Ngenya.

Amesema wamefanya ukaguzi wa shehena 100,851 kabla hazijaingizwa nchini sawa na asilimia 99 ya lengo la kukagua shehena 102,083.

Pia, jumla ya bidhaa 151,570 kutoka nje ya nchi zilikaguliwa baada ya kufika nchini sawa na asilimia 77 ya lengo la kukagua bidhaa 197,417.

Ili kufanya kazi kwa ufanisi wamekuwa wakishirikiana na taasisi nyingine za Serikali ambazo ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Tume ya Ushindani (FCC), Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Jeshi la Polisi pamoja na vyombo vingine vya usalama kufanya ukaguzi ili kubaini bidhaa zisizokidhi matakwa ya viwango na kuchukua hatua stahiki.