TET yawafunda walimu wa masomo ya ufundi

Baadhi ya walimu kutoka mikoa 10 ya Tanzania Bara na Zanzibar wanaofundisha masomo ya ufundi kwa shule za sekondari.

Muktasari:

Serikali imesema inaendelea kufanya jitihada za kutoa mafunzo mbalimbali kwa walimu ili kuboresha taaluma na utaalamu wao katika masomo mbalimbali yakiwamo masomo ya ufundi.

Tanga. Serikali imesema inaendelea kufanya jitihada za kutoa mafunzo mbalimbali kwa walimu ili kuboresha taaluma na utaalamu wao katika masomo mbalimbali yakiwamo masomo ya ufundi.

Hayo yamesemwa leo Jumatano Aprili 20, 2022 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Ali Khamis wakati akifungua mafunzo kazini kwa walimu wa masomo ya ufundi katika shule za sekondari za Serikali na binafsi wa mikoa 10 ya Tanzania Bara na Zanzibar, yaliyofanyika mkoani Tanga.

Amesema mafunzo hayo ambayo yameandaliwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) yamelenga kuboresha utaalamu wa walimu.

"Napenda niwakumbushe kupitia kwenu taifa linatarajia kupata wahitimu waliobobea na wanaoweza kujiajiri au kuajiriwa katika fani mbalimbali ikiwemo ufundi mitambo, umeme na vifaa vya mawasiliano na ujenzi. Tunatarajia wanafunzi wenu wakiandaliwa vizuri wataweza kujiajiri na kutengeneza ajira kwa watu wengine na matarajio haya hayatafikiwa endapo ufundishaji na ujifunzaji wa masomo haya hautalenga kumjengea mwanafunzi mwelekeo wa kutenda.

"Malengo hayo yakifikiwa, taifa litaweza kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia kwa kuwa litakuwa na vijana wenye uwezo wa kutumia maarifa ya ufundi katika kufikiri, kubuni na kuunda vifaa na nyenzo za kurahisisha utekelezajiwa shughuli za maendeleo kwani kwa ujumla mafunzo haya pia yamedhamiria katika kukuza stadi za karne ya 21 ambazo ni mawasiliano, ushirikiano, ubunifu na fikra tunduizi," amesema.

Kwa upande wa Zanzibar amesema uchumi wa bluu ni fursa ambapo Serikali imedhamiria kuwekeza kwenye miradi kadhaa mikubwa na midogo ya kiuchumi kwa wazawa na wageni katika uvuvi wa samaki, kilimo cha mwani, miundombinu ya uvuvi na usafirishaji wa mazao ya baharini yanayosafirishwa katika kiwango cha kimataifa hivyo Serikali inahitaji kuwa na vijana wengi wenye ujuzi wa kutosha katika uchumi wa bluu.

Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dk Aneth Komba amesema mafunzo hayo yamefadhiliwa na Serikali kupitia fedha za maendeleo zilizotolewa kwa TET ambapo kwa mwaka wa fedha 2021/22 taasisi hiyo imepokea Sh1.24 bilioni.

"Kawaida tunapoboresha mitaala au mihtasari, huwa ni muhimu kuwapitisha walimu kwenye maboresho yaliyofanywa ili kuwawezesha kutekeleza mtaala kwa mafanikio. Hivyo TET imeona ni muhimu kuanza na kundi hili la walimu lakini ni matarajio yetu kuwa kwa kupitia teknolojia na njia nyingine tutawafikia walimu wa masomo yote.

"Matokeo ya mafunzo haya tunatarajia walimu watatumia mbinu bora za ufundishaji wa masomo haya na hatimaye kumwezesha mhitimu wa masomo haya kupata maarifa, stadi za kutenda na uelekeo wa kujitegemea kwa manufaa mapana ya jamii na taifa kwa ujumla." amebainisha.

Naye Mkurugenzi Msaidizi, Elimu ya Sekondari, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hadija Mcheka amewataka washiriki kuyatumia mafunzo hayo waliyopata kwa ufasaha na wasiende kukaa nayo tu bali wakayatumie ipasavyo kwa kuchangia na wenzao waliowaacha vituoni kwani serikali inatarajia wataenda kuyasambaza na kutumia kwa wanafunzi walioko shuleni.