TIC yasajili miradi ya Sh305.7 trilioni ndani ya miaka 27

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo akizungumza wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara yake kwa mwaka 2024/25 bungeni jijini Dodoma leo. Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Mipango na Uwezeshaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema hayo leo Aprili 22, 2024 wakati akiwasilisha maombi ya kuidhinishiwa Sh121.32 bilioni kwa mwaka 2024/25

Dodoma. Ofisi ya Rais Mipango na Uwezeshaji imesema miradi ya uwekezaji 12, 381 iliyosajiliwa katika kipindi cha kati ya mwaka 1996 hadi mwaka jana, ilitarajiwa kuajiri watu milioni 1.77 nchini.

Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Mipango na Uwezeshaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema hayo leo Aprili 22, 2024 wakati akiwasilisha maombi ya kuidhinishiwa Sh121.32 bilioni kwa mwaka 2024/25.

Amesema katika kipindi hicho cha miaka 27, tangu Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kianze kuweka rekodi, miradi hiyo imeingiza mtaji kutoka nje wa jumla ya Dola  117.827 bilioni za Marekani (Sh305.7 trilioni).

“Katika kipindi cha miaka 27 (1996 hadi 2023) tangu TIC ianze kuweka rekodi za miradi ya uwekezaji, jumla ya miradi 12,381 imesajiliwa iliyotarajiwa kuajiri watu milioni 1.77,”amesema Profesa Kitila.

Profesa Kitila amesema katika mwaka 2020 ajira zilizopatikana kutokana na uwekezaji zilikuwa ni 17,385, mwaka 2021 zikiwa ajira 53,025, mwaka 2022, 40,889 huku mwaka jana ikiajiri watu 137,010.

Kitila amesema kwa kipindi cha mwaka jana TIC, ilisajili miradi mipya 509 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 112.1 ikilinganishwa na miradi 240 iliyosajiliwa kwa kipindi kama hicho mwaka 2022/23.

“Miradi hiyo inatarajiwa kuwekeza jumla ya Dola za Marekani Milioni 4,490.24 na kutengeneza ajira 229, 282 na kutengeneza ajira 229, 282,”amesema.

Vipaumbele vya bajeti

Kwa upande wa vipaumbele, Profesa Kitila amesema katika mwaka 2024/25 ofisi yake itatekeleza vipaumbe 10 ikiwemo kukamilisha sheria ya uwekezaji wa umma na kanuni zake na kukamilisha maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Vingine ni kuanza utekelezaji wa mradi wa kielelezo wa ukanda maalumu wa kiuchumi wa Bagamoyo kwa kuzingatia Mpango kabambe wa mwaka 2024.

Ametaja kipaumbele kingine ni kufanya utafiti wa urahisi wa ufanyaji biashara na uwekezaji Tanzania kwa mwaka 2024, lengo likiwa ni kuchochea ushindani na uwekaji wa mazingira bora ya biashara ndani ya nchi.

“Kuanza ushindanishi katika sekretariati za mikoa na mamlaka za Serikali za Mitaa kuhusu kuvutia wawekezaji na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na ufanyaji wa biashara,” amesema.

Pia, ametaja kipaumbele kingine ni kuhuisha Mpango wa Maboresho wa Mazingira ya Biashara na Uwekezaji utakaoainisha changamoto mpya za uwekezaji na biashara nchini na kuendelea kuboresha mazingira ya kufanyia biashara.

Mazingira ya biashara

Profesa Mkumbo amesema mwaka juzi Serikali iliajiri mtaalamu mwelekezi kufanya tathimini ya utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (Mkumbi) maarufu kama Blue Print.

Amesema lengo lilikuwa ni kubaini hatua iliyofikiwa na changamoto zilizojitokeza katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

Ameongeza kuwa mbali na mafanikio yaliyopatikana, taarifa ya tathimini hiyo imebaini changamoto kadhaa ambazo zinaendelea kukwamisha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

Ametaja changamoto hizo ni tozo, ada na faini mpya pasipokufanya tathimini ya kina kuhusu athari zake katika mazingira ya biashara na uwekezaji.

Nyingine ni kukosekana kwa utaratibu wa ukaguzi wa pamoja kwa mamlaka za urekebu na Mkumbi kutofahamika ipasavyo kwa wafanyabiashara na wadau kwa ujumla.

Aidha, akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, Mjumbe wa kamati hiyo, Dk Alice Kaijage ameshauri Serikali ihakikishe inaboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini.

Ametaka kuboresha mazingira kwa kutoa huduma kwa wafanyabiashara na wawekezaji kwenye eneo maalum katika kila mkoa.

Pia, ameshauri Serikali iongeze mitaji kwenye taasisi na mashirika ya umma, ili kuleta tija na kuongeza faida.

Mbunge wa Vunjo, Dk Charles Kimei amesema amefurahishwa kuona kuwa Blue Print imetekelezwa kwa kiasi kikubwa.

Hata hivyo, ameshauri kuwepo kwa uhuishaji wa mpango huo ili kuona ni jambo gani lililobakia ama kimekuwepo kinyume na kilichotarajiwa.

“Kupunguza tozo sio kusaidia uwekezaji, unaweza kupunguza tozo, unaweza ukatoa tozo zote usipate hata mwekezaji. Kuna vitu vingine vinahitajika ili uwekezaji uweze kuonekana katika nchi hii,” amesema.

Ameshauri kuanzishwa kwa kitengo kitakachoshughulika na wajasiriamali ndogondogo kwa kuhamasisha na kuatamia miradi midogomidogo.